Chuo kikuu cha al-Alzhar nchini Misri kimewafukuza wanafunzi 76 kwa madai kwamba wamekiuka kanuni za chuo hicho. Wakuu wa al-Azhar wamesema wanafunzi waliofukuzwa wamehusika kwenye ghasia na fujo katika miezi ya hivi karibuni. Wanafunzi wa chuo hicho wanaopinga serikali inayoungwa mkono na jeshi wamekuwa wakiandamana na mara kadhaa polisi wa kuzima fujo wamekuwa wakitumia mkono wa chuma kukabiliana na wanafunzi hao.
Hadi kufikia sasa makumi ya wanafunzi wameuawa na polisi wakati wakiandamana kuipinga serikali. Tangu jeshi la Misri liipindue serikali ya Muhammad Mursi mwezi Julai mwaka uliopita, hali imeendelea kuwa mbaya katika sehemu mbalimbali ya mji mkuu na miji mingine ya nchi hiyo. Wanafunzi waliofukuzwa wanatoka katika vitivo mbalimbali vya chuo hicho ambacho mbali na umashuhuri wake, kinahesabiwa kuwa kikongwe zaidi miongoni mwa vyuo vikuu vya Misri.