Wanajeshi wa jeshi la serikali ya Sudan Kusini SPLA wamefanya mashambulio makubwa dhidi ya waasi na kufanikiwa kuingia kwenye miji miwili iliyoko kaskazini mwa nchi iliyokuwa ikidhibitiwa na waasi wanaoongozwa na Riek Machar makamu wa zamani wa rais wa nchi hiyo changa barani Afrika. Philip Aguer msemaji wa jeshi la Sudan Kusini amesema kuwa, vikosi vya serikali vimeshambulia na kuukalia mji wa Nasir, moja kati ya ngome muhimu za waasi. Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini amesema kuwa, wanajeshi wa serikali jana walifanikiwa pia kuingia kwenye mji wa Bentiu wenye utajiri mkubwa wa mafuta ulioko katika jimbo la Unity. Hayo yanajiri katika hali ambayo, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amemuambia Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kwamba iwapo itathibitika kwamba kuondoka kwake madarakani ni kwa maslahi ya wananchi wa nchi hiyo, basi atafanya hivyo.