Makubaliano ya amani yaendelea kukiukwa S/Kusini

   Rais Salva Kiir na hasimu wake Riek Machar
Vita na mapigano ya ndani nchini Sudan Kusini, vinaendelea licha ya pande hasimu kutiliana saini makubaliano ya amani, huku kila upande ukimlaumu mwenzake kwa kuvunja makubaliano hayo. Mapigano nchini humo, yanaendelea katika hali ambayo, mashirika na taasisi tofauti zimeonya kwamba nchi hiyo itakumbwa na uhaba mkubwa wa chakula ikiwa mapigano na vita vitaendelea. Habari zinaeleza kuwa, mapigano kati ya askari watiifu kwa serikali na waasi wanaomuunga mkono Rieck Machar, makamu wa rais wa zamani wa nchi hiyo, yameshadidi zaidi katika maeneo yenye utajiri wa mafuta likiwemo jimbo la Upper Nile. Shughuli za uzalishaji mafuta zimebakia katika jimbo la Upper Nile pekee, kufuatia kufungwa visima kadhaa vya mafuta katika jimbo la al-Wahdah baada ya kushadidi mapigano kati ya pande mbili hizo. Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini, Philip Aguer na msemaji wa waasi Lul Ruai Koang, kwa nyakati tofauti wamethibitisha kuendelea mapigano makali katika eneo la Dolib Hil kusini mwa mji wa Malakal, katikati mwa jimbo la Upper Nile na pia katika eneo la Rank kaskazini mwa jimbo hilo. Aguer amesema kama ninavyomnukuu: “Sisi tutatekeleza makubaliano ya amani, lakini kamwe hatutakubali waasi watumie mwanya huo katika kuendeleza mashambulizi dhidi ya maeneo yetu.” Mwisho wa kunukuu. Hii ni katika hali ambayo, kwa upande wake msemaji wa waasi, Ruai Koang amenukuliwa akisema kuwa, vikosi vya jeshi la serikali viliushambulia mji wa waasi wa Dolib kwa mashambulizi makali hapo jana Jumatano.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company