Afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na maswala ya kibinadamu ameonya Alhamis kuwa kuwatenganisha Waislam na Wakristo katika Jamhuri ya Afrika ya Kati sio suluhu la mgogoro wa kidini na kikabila nchini humo.
John Ging,mkurugenzi mkuu wa operesheni za idara ya maswala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, alisema Waislam nchini humo ambao ni wachache wanahisi wamenaswa na wanahitaji kuhamishwa kwa sababu wanaona maisha yao yametishiwa na kundi la wanamgambo wa Kikristo.
Ging ambaye majuzi alikuwa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa ziara yake ya pili katika muda wa miezi mitatu, anasema hali inaendelea kuzorota na katika kiwango cha kutisha.
Takriban watu milioni moja wamelazimika kutoroka manyumbani mwao kufuatia ghasia za wanagmabo wanaojiita anti-balaka ambao wanawashambulia waasi wa Kiislam kutoka kundi la Seleka.
Kundi la Seleka lilipindua serikali zaidi ya mwaka mmoja uliopita, na kutokana na ghasia hizo Umoja wa Mataifa unasema nusu ya wananchi wanahitaji msaada.
Katika mji wa Boda ambao Ging alitembelea, Waislam wapatao elfu 24 wanaomba kuhamishwa. Na katika ishara inayoonyesha kwamba hali ya wasiwasi imeongezeka baina ya makundi hayo baadhi ya viongozi wa Kikristo wameomba Umoja wa Mataifa kuwasaidia Waislam hao kuondoka nchini humo.
CHANZO VOA SWAHILI