Serikali imesema kuwa Sudan sio nchi ya kwanza kutekeleza sheria za kiisilamu
Mahakama nchini Sudan imemhukumu kifo mwanamke mmoja anayedaiwa kubadili dini yake na kuolewa na mwanamume mkristo.
Daktari Mariam Yahya Ibrahim Ishag, ambaye babake ni muisilamu alishitakiwa kwa kosa la kuasi dini pamoja na kufanya zinaa kwa kuolewa na mwanamume mkristo , kitu ambacho dini ya kiisilamu imeharamisha kwa wanawake.
Mariam mwenye umri wa miaka 28 pia ni mjamzito na ataadhabiwa kwa kuchapwa mijeledi miamoja kwa kosa la zinaa.
Maafisa wakuu wanasema kuwa licha ya Mariam kulelewa kwa njia ya kikristo yeye bado ni muisilamu kwa sababu hiyo ndiyo dini ya babake.
Alipewa siku tatu baada ya kuhukumiwa aweze kurejea katika dini ya kiisilamu lakini akakataa na ndio maana adhabu ikasalia.
Kwa kawaida wanawake waisilamu hawaruhusiwi kuolewa na wanaume wakristo ingawa wanaume waisilamu wanaruhusiwa kuwaoa wanawake wakristo.
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International linasema kuwa Bi Ishag alilelewa kama Mkristo muorthodoxi kwa sababu babake hakuwepo naye maishani mwake.
'Kesi ya kwanza'
Kesi ya Ibrahim ni ya kwanza ya aina yake kusikika nchini Sudan , kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.
Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu, wamelaani uamuzi huo wa mahakama na kuitaka serikali ya Sudan kuheshimu haki na uhuru wa watu kuabudu.
Maafisa wa balozi za mataifa ya magharibi pia wamekemea vikali kesi hiyo na kuelezea asiwasi wao kuihusu.
Maafisa hao wamewataka maafisa wa sheria nchini humo kuangalia kesi hiyo upya na kuhakikisha kuwa Mariam anatendewa haki.
Waziri wa mawasiliano amesema kuwa sio Sudan peke yake ambako sheria za kiisilamu zinafuatwa na ambako sio sawa kwa mtu kubadili dini yake, hali hiyo pia ipo nchini Saudi Arabia na katika nchi zingine zinazofuata sheria za kiisilamu.
Serikali ya Rais Omar al-Bashir inakabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi na kisiasa hasa baada ya kujitenga na Sudan Kusini ambako mafuta yake yalikuwa yanatoka mwaka 2011.