NEEMA TFF, TAIFA CUP YA MABINTI YAPATA UDHAMINI

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KAMPUNI ya Proin Promotions ya hapa nchini jana imesaini mkataba na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya kudhamini mashindano ya Kombe la Taifa kwa wanawake yatakayofanyika kati ya mwezi Septemba na Oktoba mwaka huu.
Akizungumza leo mjini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kampuni hiyo, Johnson Rukaza, alisema kuwa makubaliano hayo waliyoingia na TFF yatakuwa ni ya miaka miwili na yatawagharimu zaidi ya Sh. milioni 150 ili kufanikisha michuano hiyo.

Mabinti wamepata udhamini

Rukaza alisema kuwa kupitia mashindano hayo ya Kombe la Taifa wanaamini vipaji vya wachezaji wanawake vitaonekana na baadaye kuisaidia timu ya Taifa ya jinsia hiyo (Twiga Stars) kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ambayo inashiriki.
Alisema kwamba wao wamefungua njia kudhamini mashindano hayo na wanawaomba makampuni na taasisi nyingine kujitokeza kudhamini mashindano hayo ikiwamo na vituo vya televisheni lengo likiwa ni kutangaza soka la wanawake.
"Leo ni siku ya kihistoria, tumedhaminia kuleta maendeleo katika mpira wa wanawake na tunaahidi tutasimama kidete kupeleka mbele kitaifa na kimataifa soka la wanawake," alisema Rukaza.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi, alisema kuwa uongozi wake unawashukuru wadhamini hao wapya na inaahidi uongozi wake utahakikisha soka la wanawake linasonga mbele.
Malinzi alisema kwamba wanawaomba wazazi na walezi kuwaruhusu watoto wa kike kushiriki mchezo huo kwa sababu utawasaidia kiafya, kupata burudani na kuinua hali zao za kichumi pale watakapofanikiwa kupata klabu za kucheza.
"Wanawake wa Tanzania wanatakiwa kuiga mafanikio yanayopatikana kupitia mchezo huo, tuache dhana potofu kwamba katika soka wachezaji wanajifunza vitu vibaya," Malinzi aliongeza.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Soka la Wanawake Tanzania (TWFA), Lina Kessy, alisema kwamba wanaamini sasa mpira wa wanawake utacheza na jana ilikuwa ni siku ya kihistoria kwenye medani ya mchezo huo kwa upande wa wanawake.
Kessy alisema kwamba TFF na TWFA itahakikisha jitihada za kusaka wadau wengine zinaendelea ili mchezo huo uchezwe sehemu zote hapa nchini.
Alisema kwamba zaidi ya mikoa 17 inatarajiwa kushiriki mashindano hayo ambayo mara ya mwisho yalifanyika mwaka 2008.
CHANZO BIN ZUBEIRY BLOG
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company