UFISADI WA BIL. 200/-BoT: CCM kung’oka kama KANU

KASHFA nzito ya ufisadi wa dola za Marekani milioni 122 (sawa na sh bil. 200) inayowakabili vigogo sita wa serikali, huenda ikaking’oa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama ilivyotokea kwa chama tawala cha KANU cha nchini Kenya mwaka 2002.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, mmiliki wa Kampuni ya PAP inayodai kuinunua Kampuni ya IPTL yenye mgogoro na Tanesco, Habinder Singh Sethi, anatajwa kuhusika katika kashfa kubwa ya ufisadi nchini Kenya ya Goldenberg, uliogharimu takribani dola milioni 600.
Ufisadi huo pia ulihusisha mahakama, watendaji, viongozi na wanasiasa wakubwa nchini humo, ikiwemo familia ya aliyekuwa Rais wa wakati huo, Daniel arap Moi.
Wiki iliyopita, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), aliwataja vigogo sita wa serikali, wakiwemo mawaziri kadhaa kuwa wamehusika na ufisadi wa fedha hizo zilizokuwa zimewekwa katika akaunti ya Baraza la Usuluhishi la Migogoro ya Kibiashara (Escrow) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Waliotajwa ni Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospiter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi, Waziri wa Fedha Saada Mkuya, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Beno Ndullu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Mhandisi Felchesmi Mramba.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Tanzania Daima Jumatano, kashfa hii ya pili baada ya ile ya EPA ya sh bilioni 133 katika BoT, huenda ikaiweka pabaya Serikali ya CCM kwenye uchaguzi mkuu ujao 2015.
Itakumbukwa kuwa kashfa ya ufisadi kama huu ya Goldenberg ndiyo ilisababisha kuanguka kwa Chama tawala cha KANU nchini Kenya chini ya Rais Moi aliyekuwa akimpigania Uhuru Kenyatta kurithi mikoba yake, lakini akashindwa na Mwai Kibaki.
Bilionea huyo, Sethi, mwenye asili ya Singasinga, ndiye anatajwa kuvuruga mfumo wa serikali kwa muda mfupi katika sakata hilo la ufisadi wa BoT.
Akizungumza na gazeti hili, Kafulila alisisitiza kwamba kwa jinsi hali ilivyo sasa, anathubutu kusema kuwa Sethi ameiweka Serikali ya CCM mfukoni.
“Ufisadi wa akaunti ya Escrow ni lazima mbivu na mbichi zifahamike. Siungi mkono uamuzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza kwa kuwa hili jambo linagusa mamlaka kubwa na ya juu sana katika dola.
“Ndiyo maana nilisisitiza kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge ili kuepuka majibu ya ubabaishaji kama yalivyotolewa na Waziri Mkuu bungeni,” alisema Kafulila na kutaja sababu tano.
Moja, alisema Waziri Mkuu kusema ameagiza CAG na Takukuru wachunguze, lakini wakati huo huo anasema fedha za Escrow hazikuwa za Tanesco wala serikali kabla ya ripoti za uchunguzi, ni sawa na kuingilia uchunguzi kwani inazifanya mamlaka hizi zikose uhuru na badala yake yeye angesubiri matokeo ya uchunguzi.
Pili, alisema CAG amewahi kutoa ripoti ya aibu alipopewa jukumu la kukagua ufisadi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, hivyo hana imani kama atafanya tofauti.
Tatu, Kafulila anasema kuwa Takukuru nayo kwenye ufisadi wa Richmond walitoa ripoti dhaifu na hivyo hajui kama wameshajifunza.
Katika sababu ya nne, anasema kuwa fedha za Escrow zote ni za Tanesco kwani hukumu ya awali ya ISCID ilieleza gharama za malipo ya umeme kati ya Tanesco na IPTL ifanyike upya kwani ilikuwa juu kuliko kawaida na kwa misingi ya ukomoaji, kiasi ambacho tayari Tanesco ilikuwa imetozwa zaidi na IPTL kuanzia mwaka 2002, ni zaidi ya dola milioni 150, hivyo hiyo fedha yote iliyokuwa Escrow ingekuwa mali ya Tanesco.
“Tano, hili jambo lote ni mchezo mchafu. Kwa mfano, anadanganya umma kuwa eti amekuja kuiuzia Tanesco umeme kwa bei ya chini kabisa, na hivyo lazima Watanzania wajiulize huyu mtu ni wapi amepata rekodi ya biashara ya kuuza umeme hata ahaidi.
“Pia kama anasema amenunua asilimia 30 za IPTL zilizokuwa chini ya VIP kwa dola milioni 75, ina maana asilimia zote 100 atakuwa amenunua kwa zaidi ya dola milioni 200?” alihoji.
Kafulila alifafanua kuwa inawezekanaje mtu aje anunue IPTL yenye migogoro na madeni ya miaka mingi wakati mitambo yake ni chakavu yenye zaidi ya miaka 20 ilhali mitambo kama hiyo mipya ingeweza kununuliwa kwa dola milioni 100?
“Huyu Singasinga wa PAP ukweli hajanunua asilimia 70 ya Mechmar na ndiyo maana hana ‘share certificate’ ya Mechmar. Na serikali hii inaingia hasara kubwa sana muda si mrefu kulipa deni la Standard Bank pamoja na Liquidator wa Mechmar au Mechmar mwenyewe,” alisema.
Kwa mujibu wa Kafulila, uamuzi wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, uliobarikiwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda wa kuzielekeza taasisi za serikali za Takukuru na CAG kuchunguza ili kujiridhisha kuhusu uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Escrow umeibua shaka.
Akaunti hiyo ilifunguliwa mwaka 2004 kutokana na mgogoro wa kibiashara kati ya IPTL na Tanesco ambapo Tanesco ilipeleka shauri hilo kulalamikia gharama kubwa wanazotozwa na IPTL.
Hivi karibuni baraza hilo lilitoa uamuzi wa awali wa kutaka Tanesco kukaa pamoja na IPTL kupitia upya malipo hayo, lakini Tanesco imekataa kufanya hivyo.
Kwa mujibu wa Kafulila, uchunguzi alioufanya na ushahidi alionao, fedha hizo zimeshachotwa katika akaunti hiyo kwa ushirika wa vigogo hao.
Alisema kuwa fedha hizo zilihifadhiwa katika akaunti hiyo kusubiri hatma ya mgogoro huo ambao kwa sasa umekuwa mkubwa zaidi baada ya Kampuni ya PAP kudai imeinunua IPTL.
PAP inadai kuinunua IPTL kutoka kwa Mechmar iliyokuwa ikimiliki asilimia 70 ya hisa na VIP iliyokuwa na umiliki wa asilimia 30.
Kwa mujibu wa Kafulila, ushahidi wa cheti unaonyesha kuwa PAP imenunua asilimia 30 ya hisa za VIP, lakini haina ushahidi wa ununuzi wa hisa asilimia 70 za Mechmar.
Baraza la Usuluhishi wa Migogoro ya Wawekezaji (ISCID), lilitoa hukumu ya awali Februari 2014 na kutoa siku 90 kwamba Tanesco ikae na IPTL wapige upya mahesabu ya bei ya umeme kwani inatoza zaidi.
Kafulila alisisitiza kuwa suala hilo liko wazi kwa vile limethibitishwa na Gavana Ndullu alipoitwa kwenye Kamati ya Bunge, alisema kuwa alipewa maelekezo ya kushinikizwa kutoa fedha hizo.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company