Nchini Tanzania Shirika la Afya Duniani WHO linashirikiana na serikali ya nchi hiyo kusaidia kudhibiti ugonjwa wa homa ya Dengue au Kidingapopo ambao tuka uzuke mwezi Januari mwaka huu umesababisha vifo vya watu watatu na wagonjwa 400.
Afisa wa udhibiti na uzuiaji wa magonjwa WHO Dkt. Grace Saguti amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kile wanachofanya sasa ni kuhakikisha miongozo ya udhibiti inazingatiwa ikiwemo kuelimisha umma, kuweka utaratibu na ushirikiano wa kisekta badala ya kuachia wizara ya afya pekee.
Mwongozo mwingine ni kudhibiti mbu anayeambukiza ambaye ni Aedes anayeng'ata asubuhi na mchana na kujenga uwezo katika udhibiti wa ugonjwa huo.
Katika siku za hivi karibuni ripoti zinaeleza kuwa kumetokea mlipuko wa ugonjwa wa homa ya dengue katika baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ambapo nchini Tanzania Wizara ya Afya imetangaza kuwa watu karibu 400 wamekwishagunduliwa kuugua ugonjwa huo.
CHANZO RADIO IRAN SWAHILI