Ndugu zangu,
Ninachokiona Bujumbura si kipya Afrika, mfano, Obote wa Uganda kwa matatizo aliyoayaacha nyumbani ikiwamo ugomvi na wananchi, mwaka 1971 alifunga safari ya kwenda kwenye Mkutano wa Jumuiya ya Madola, huku nyuma Idd Amin akatangaza kumpindua. Waganda wakaingia mitaani kushangilia wakiwa wameshika matawi ya miti.
Niliandika juma la jana, kuwa Pierre Nkurunziza ni kielelezo cha marais wa Afrika ambao, wakiwa madarakani, huwa hawajiandai na maisha mengine nje ya Ikulu. Kwamba walipaswa kufahamu kuwa kuna maisha mengine zaidi ya kuwa Rais. Na Nkurunziza bado kijana kabisa, angeweza kufanya mengi mengine nje ya Ikulu na bado akaheshimika kama ' Rais Mstaafu'.
Inasikitisha, kuwa tulichokihofia ndicho kinachotokea. Niliandika, kuwa Nkurunziza anatembea na kibiriti mfukoni. Ni kwa Nkurunziza kung'ang'ania msimamo wake wa kuendelea na awamu ya tatu.(P.T)
Tuna tatizo Afrika, kuwa viongozi kutokuwa na mikakati ya kuandaa warithi wao. Na hata vyama, huwa havina mikakati ya kuwaandaa viongozi wa kesho. Afrika hatuwekezi kwa vijana viongozi wa kesho.
Tumeshasikia, kuwa Nkurunziza amekwama Dar es Salaam. Hawezi kurudi Bunjumbura, maana anga na viwanja vya ndege vimefungwa. Hivyo, hawezi kurudi na kuingia kwenye Ikulu yake ya Bujumbura. Na Afrika Rais ni Ikulu, naam, ' Mkulu Wa Nchi Na Ikulu Yake!' Kama huna Ikulu ya kuingia, basi, wewe si rais. Nkurunziza hawezi kuwa Rais anayeishi Ikulu ya Serena Hotel, Dar Es Salaam.
Nkurunziza alipaswa kusoma alama za nyakati. Kuwa dunia imebadilika. Afrika ya jana si ya leo. Kama Nkurunziza ameongoza Burundi kwa mihula miwili na bado anadhani hakuna mtu mwingine wa kuweza kuongoza Burundi isipokuwa yeye, basi, hapo tatizo ni Nkurunziza mwenyewe. Kuwa ameshindwa kuandaa mazingira mazuri ya kimfumo, ndani na nje ya chama chake, ya kumpata mrithi wake, na bado nchi ikasonga mbele.
Na kwa kuziangalia taswira zile za raia wa Burundi wanaoshangilia mitaani, unaona kabisa, kuwa hata Nkurunziza akifanikiwa kurudi na akaendelea na msimamo wake wa kuendelea na awamu ya tatu. Basi, moto aliouwasha unaweza kuwa mkubwa zaidi na kusambaa mpaka nje ya mipaka ya Burundi.
Tanzania, kama ' Kaka Mkubwa' kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu, ina lazima ya kuongoza juhudi za kuuzima moto aliouwasha Nkurunziza kule Burundi.
Kikao cha jana alichokiitisha Rais Jakaya Kikwete pale Ikulu ya Dar es Salaam hakikuwezekana. Lakini, tumemsikia Rais Kikwete akisema kuwa atawaita tena Marais wenzake ndani ya wiki mbili zijazo, ni jambo jema.
Ni Neno La Leo.
Maggid.
TAIFA STARS HAZARANI
-
Kaimu kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Etiene Ndairagije ametangaza
kikosi cha timu ya taifa chenye wachezaji 30 ambao wanajiaandaa na mchezo
wa kuwania ...
5 years ago