CHAMA cha ACT – Wazalendo kimesema hadi sasa wamejitokeza wagombea katika majimbo 203 ya uchaguzi nchini huku kura za maoni za kupata wagombea katika majimbo mbalimbali zikiendelea.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Samson Mwigamba, hadi kufikia Ijumaa iliyopita, chama hicho cha upinzani nchini kilikuwa na wagombea 298 katika majimbo 203 nchini kati ya majimbo 265 yaliyopo.
Mwigamba aliuambia mtandao huu kuwa chama hicho ambacho Kiongozi Mkuu wake ni aliyewahi kuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chadema, Zitto Kabwe, kitasimamisha mgombea kwa kila jimbo la uchaguzi nchini.
“Chama chetu kitasimamisha mgombea katika kila jimbo nchini.Na hadi kufikia Ijumaa iliyopita, tulikuwa na wagombea 298 katika majimbo 203. Kwa sasa kura za maoni zinaendelea katika sehemu mbalimbali nchini na baadhi yao wamekwisha kamilisha uteuzi wa wagombea,” alisema Mwigamba.
Alitaja baadhi ya majimbo yaliyopata wagombea kuwa ni Kigoma Mjini ambako ameshinda Zitto, Kasulu Mjini alikoshinda aliyekuwa Mbunge kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, Moses Machali na Kasulu Vijijini ambako ameshinda Thomas Matatizo ambaye ni mwanasheria wa chama hicho.
Alisema majimbo mengine yalitarajiwa kufanya kura za maoni jana ikiwamo Singida Mjini ambako anagombea Mwenyekiti wa Taifa wa ACT – Wazalendo, Anna Mghwira, huku majimbo mengine yakitarajiwa kufanya leo na kesho ikiwamo Ubungo ambalo litafanya kesho na ambako Mwigamba amejitosa kuwania uteuzi huo.
“Majimbo mengine yanaendelea na kura za maoni kwa sasa. Kwa mfano, Tarime Mjini, Tarime Vijijini, Bukombe, Singida Mjini yanatarajiwa kufanya kura hizo kati ya leo (jana) na kesho (leo). Geita Mjini walifanya, lakini kulitokea ukiukwaji wa taratibu na wakaomba zoezi hilo lilirudiwe,” alieleza Mwigamba.
Aidha, alisema wanaendelea kupokea baadhi ya wanachama waliokuwa katika vyama vingine vya upinzani ambao wanajiunga na chama hicho, akitaja baadhi yao kuwa walikuwa wagombea katika majimbo ya Musoma Mjini, Bunda Mjini, Tarime Mjini (wote wametoka Chadema) na Mtama (ametoka CCM).
Kuhusu wagombea wa urais, alisema hadi sasa amejitokeza mgombea mmoja, ingawa wapo wanawake wawili walioonesha nia lakini hawajachukua fomu ambazo zitatolewa mpaka Agosti 11, mwaka huu.
Katibu Mkuu huyo wa ACT – Wazalendo alisema vikao vya uteuzi vitaanza Agosti 12 kwa kukutana na Sekretarieti itakayofuatiwa na Kamati Kuu Agosti 14, Halmashauri Kuu ya Taifa Agosti 15 na Mkutano Mkuu utafanyika Agosti 16, mwaka huu kupitisha Mgombea wa Urais na kufanyia marekebisho Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho.
ACT - Wazalendo ilipata usajili wake wa kudumu Mei, 2014, na mapema mwaka huu, Zitto alijiunga nacho na kutangazwa kuwa Kiongozi Mkuu. Ni chama kinachoamini katika misingi ya Ujamaa Demokrasia.
TAIFA STARS HAZARANI
-
Kaimu kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Etiene Ndairagije ametangaza
kikosi cha timu ya taifa chenye wachezaji 30 ambao wanajiaandaa na mchezo
wa kuwania ...
5 years ago