WAKATI Waislamu kote duniani wakiwa katika simanzi kuu kutokana na vifo vya mahujaji zaidi ya 700 katika mji mtakatifu wa Makka, Saudia Arabia, imethibitika kuwa zaidi ya mahujaji 50 wa Tanzania, hawajulikani walipo.
Aidha, idadi ya mahujaji wa Tanzania waliokufa katika tukio la kukanyangana katika mji huo mtakatifu, imefikia watano, baada ya mtu mmoja zaidi kuthibitika kufa na mwingine kupatikana akiwa majeruhi.
Kutokana na ongezeko hilo la vifo, idadi ya Watanzania waliokufa wakiwa katika ibada ya Hijja, moja ya nguzo kuu ya Kiislamu, sasa imefikia watu watano. Hayo yamethibitishwa jana na Mufti wa Tanzania, Shehe Abubakari Zuberi katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoituma akiwa Makka.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa “Bakwata kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania Saudi Arabia, tumepata taarifa kwamba maiti mmoja amepatikana, ametambulika kwa jina la Shafi Khamisi Ali. Pia Nasra Nassor Abdallah amepatikana akiwa amepata majeraha. Mwenyezi Mungu atawapa tahfif Insha Allah.
“Kadhalika tumepokea taarifa ya kutopatikana kwa Watanzania 50 ambao walikuwapo Makka wakati wa tukio hilo. Kati yao 30 walisafiri kupitia taasisi ya Ahlu Daawa, taasisi ya Khidma watu 17 na TCDO watu watatu.”
Taarifa ya Mufti Zuberi imekuja ikiwa ni mwendelezo wa taarifa juu ya tukio la kuhuzunisha, lililotokea wiki iliyopita huko Mina, Saudi Arabia, ambako mahujaji zaidi ya 700 walikufa na wengine kujeruhiwa wakati wakielekea kwenye Jamaraat, ambapo palitokea msongamano mkubwa.
Alisema anatambua uwepo wa mkanganyiko wa taarifa, ambazo zinazidisha taharuki kwa ndugu na jamaa wa mahujaji. Hata hivyo, aliwaomba Waislamu kuwa na moyo wa subira, kwani juhudi za kuwatafuta mahujaji wengine zinaendelea.
Aliwaombea dua wale waliotangulia mbele ya haki na Mwenyezi Mungu, apokee ibada zao, awasamehe madhambi yao na awakusanye katika kundi la waja wema peponi.
“Kutokana na mtihani huu kwetu sote, nawaombea dua wafiwa Mola awape subra na ustahmilivu na kuwaombea wagonjwa wapate tahfif.Pia nawaomba Waislamu wote Tanzania kuwaombea dua waathirika wa mtihani huu.
“Mwisho nichukue fursa hii kuwaomba wale wote wenye nafasi ya kuwafariji na kuwasaidia wanafamilia, ambao katika ajali hii wameondokewa na nguzo katika familia hizo wafanye hivyo.
"Tuwasaidie wanafamilia hawa kwa hali na mali katika wakati huu mzito sana kwao ili tuwapunguzie majonzi na unyonge walionao,” ilisema taarifa hiyo ya Mufti.
TAIFA STARS HAZARANI
-
Kaimu kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Etiene Ndairagije ametangaza
kikosi cha timu ya taifa chenye wachezaji 30 ambao wanajiaandaa na mchezo
wa kuwania ...
5 years ago