HABARI KUU ZA LEO na OSCAR SAMBA
print this page
HABARI NA Oscar Samba

KWA HABARI ZA INJILI, NENO LA MUNGU, MAHUBIRI, TEMBELEA BLOGU YA UKOMBOZI GOSPLE www.ukombozigosple.blogspot.com

AMANI YA KRISTO YESU IPITAYO AMANI ZOTE IWAIFADHI NIA ZENU NA MIOYO YENU, PIA USIFADHAIKE MOYONI MWAKO MUAMINI YESU NA TENA USIJISUMBUWE KWA JAMBO LOLOTE BALI KWA KUSALI NA KUOMBO, Wafilpi 4:6-- na Yohana 14, Ninakutia Moyo wewe unayepitia Mazingira magumu ya kwamba usife Moyo kwani Yesu anakujua na atakushindia. Kwa Ushauri wa Kiroho na maombezi wasiliana nasi Email: ukombozigosple@gmail.com Simu +2557 598 592 87

0 Toa maoni yako.

ni matokeo ya serikali dhaifu,kuwafukuza wanafunzi walioingia vyuoni kimakosa

NA WAANDISHI WETU, DODOMA/DAR

NI kizaazaa. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya migomo na fukuzafukuza ya wanafunzi kutawala katika vyuo vikuu nchini hali ambayo inaonekana kuibua hisia miongoni mwa Watanzania.

Kufuatia kurudishwa nyumbani kwa wanafunzi 7,802 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Jumuiya ya Wanataaluma wa chuo hicho, imevunja ukimya na kubaini mikakati yenye shaka dhidi ya uongozi.

Kutokana na hali hiyo wanataaluma hao wamelaani kitendo cha kurudishwa nyumbani kwa wanafunzi hao wa programu maalumu ya ualimu wa msingi na sekondari bila kupewa muda wa kutosha kujiandaa kwa kuzingatia umri wao na mazingira waliyokuwa wanaishi.

Tamko la jumuiya hiyo lilitolewa jana na kusambazwa kwa vyombo vya habari na katibu wake, Lameck Thomas, ambaye alisema lawama zimekuwa zikitupwa kwa walimu kutokana na taarifa hizo kutolewa na upande mmoja wa utawala pekee kwenda serikalini bila uwepo wa ushirishwaji wowote wa wahadhiri kupitia jumuiya yao.

Kutokana na hali hiyo, Thomas alisema si busara wao kama jumuiya kukaa kimya kwa jambo hilo bila kueleza usahihi wake kwa kina, hasa katika madai ya fedha ambapo kumekuwa na uchezewaji wa tarakimu.

“Si kweli kuwa walimu tuligoma kufundisha programu hii kama inavyoelezwa sehemu mbalimbali,” alisema Thomas.

Alisema tatizo kubwa ni kutokuelewana kati ya walimu na menejimenti ya chuo kutokana na mazingira mabovu ya uendeshaji wa programu hiyo chuoni hapo, ambapo malalamiko hayo waliyatoa tangu iliponzishwa.

“Na kumekuwa hakuna dalili yoyote ya ufumbuzi huku wakiendelea kufundisha kwa uzalendo mkubwa. Jumuiya ya Wanataaluma inapata hisia kuwa wizara imeamua kwa makusudi kushirikiana na uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kupotosha uhalisia wa jambo hilo kwani hakuna hata wakati mmoja ambapo wamefanya mawasilianao na walimu kupata taarifa kutoka upande wao,” alisema.

Katibu huyo alisema kuwa katika kutafuta ufumbuzi kuhusu mgogoro huo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stella Manyanya, alikutana na menejimenti ya chuo hicho Mei 19, mwaka huu chuoni hapo ambapo katika kikao hicho wajumbe walikubaliana kwa pamoja kuundwa kwa kamati ndogo ya kufuatilia suala hilo.



UTATA WA MADAI

Alisema madai yanayoelezwa na menejimenti si sahihi na taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, imepotosha kwani haijaeleza ukweli wa madai yaliyowasilishwa na chuo husika.

“Mfano katika Kitivo ‘Koleji’ cha Sayansi Asilia na Hesabu taarifa inasema yaliwasilishwa madai ya shilingi milioni 367.88 na kupungua mpaka shilingi milioni 90. Wakati uhalisia ni kwamba madai hayo hata kama yangebanwa kwa namna gani yasingepungua mpaka chini ya shilingi milioni 223.78,” alisema Thomas.

Alisema kuwa Kitivo cha Kompyuta taarifa inasemwa waliwasilisha madai yanayozidi sh milioni 100 wakati taarifa za Koleji zinasema madai halisi ni Sh milioni 53.7.

“Kwa nini utaratibu wa malipo uliotumika mwaka jana haukutumika wakati ulifanyika bila ya kuleta matatizo yanayoonekana wakati huu? Kama tatizo ni uhakiki wa madai kwa nini mpaka sasa tunapoongea walimu wa Koleji za Ualimu na Sayansi Asilia na Hesabu hawajalipwa hata senti moja ambapo ni katikati ya muhula huu wakati walifundisha muhula uliopita?’’ alihoji Thomas.

Katibu huyo alipinga kile alichodai kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alitoa kauli ya upande mmoja Mei 30, mwaka huu suala ambalo haliwezi kuleta utatuzi wa kudumu kwani walimu hao wana mambo mengi ya kuzungumza ikiwamo mgogoro wa madai yao.

“Mfano mpaka sasa katika Koleji ya Sayansi Asilia na Hesabu kuna upungufu wa walimu 128 waliokuwa wanahitajika kufundidha programu hiyo kwa ufanisi, kwa muhula uliopita ni walimu 72 tu ndiyo waliobeba mzigo wa upungufu huo na kwa muhula huu hali ilikuwa inaelekea kuwa mbaya sana,” alisema.

Alisema kuwa wingi wa wanafunzi na uhaba wa walimu ulisababisha upangaji wa ratiba ya kufundisha kuwa ngumu kutokana na kozi kugawanywa katika mikondo mingi ambayo walimu walilazimika kuifundisha huku wakiwa na majukumu ya kufundisha kozi za shahada na majukumu mengine.



RAIS MAGUFULI

Akizungumza jana katika sherehe za utoaji tuzo za rais kwa wazalishaji bora viwandani kwa mwaka 2015, Rais Dk. John Magufuli alisema kuwa anashangazwa na wanasiasa wanaotetea watu waliopata daraja la nne kutaka waachwe wasome chuo kikuu.

“Ukigeuka hivi unakutana na wanafunzi hewa, ni nchi hii tu ambapo mtu unaweza kupata Divisheni 4 ya form 4 ukaingia chuoni na ukapata mkopo wa Serikali wakati wa form 6 hawapati mkopo. Ni nchi hii tu na anatoka mtu mwanasiasa mmoja anasema hawa wangesoma tu… kama tulifanya makosa ni lazima tuyamalize.

“Ninyi mnafahamu mtu ukimaliza form four (kidato cha nne) ukifeli sana sana utakwenda kuanzia certificate (cheti), ukifaulu then (halafu) unakwenda kuchukua diploma, baada ya miaka kadhaa tungejikuta ni Taifa la watu wa ajabu sana, ninasema haitawezekana, kama tuliyafanya makosa ni lazima tuyarekebishe na wakati ni sasa. Tuache siasa kwenye makosa,” alisema Rais Magufuli.



WANAFUNZI WAFUNGUKA

Baadhi ya wanafunzi waliorudishwa nyumbani katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wameelezea kushangazwa na tangazo lililotolewa la kutakiwa kurudi nyumbani huku wakiwa hawana kosa lolote.

Mmoja wa wanafunzi hao aliyejitambulisha kwa jina la Praygod Emmanuel, alisema kuwa aliyekuwa chuoni hapo mwaka wa pili akichukua Diploma ya Sayansi ya Ualimu, alisema anashangaa wao kufukuzwa mithili ya wanyama huku kosa likiwa si la kwao.

“Tunashangazwa kufukuzwa mithili ya wanyama, sasa hivi tunaishi kwa hofu na hatujui hatma yetu kwani tunaambiwa tutaona katika vyombo vya habari na kwenye mtandao wa chuo,’’ alisema.

Naye Joshua Meshack alisema kwa sasa hawajui hatima yao na kuiomba Serikali kuwaangalia kwani hawana wanachotegemea zaidi ya elimu waliyokuwa wakiipata ili ije iwasaidie katika siku za usoni.

Meshack alisema kinachowaumiza zaidi ni kutofanya kosa lolote, lakini wamejikuta kwenye adhabu na mateso makubwa ikiwamo kukosa fedha za kuwawezesha kurudi makwao.

“Sisi hatuna kosa, kosa ni la watu wengine vipi tuumie sisi? Maisha yetu ni ya shida, mimi sijarudi nyumbani nipo na sina hata nauli ya na sijui nitafikaje nyumbani,” alisema.



PROFESA NDALICHAKO

Juzi jioni akitoa taarifa ya Serikali bungeni, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Ndalichako, aliahidi kupitia upya mfumo wa utoaji wa mafunzo ya stashahada maalumu kwa walimu wa sayansi Udom ili kuondoa matatizo yaliyopo.

Alisema Serikali imeamua kupitia mfumo huo ili kuufanyia marekebisho na kuweza kuwasaidia wanafunzi wa kada hiyo.

“Serikali itashirikina na uongozi wa chuo cha Udom kupitia upya mfumo wa utoaji wa mafunzo hayo ya diploma ya sayansi, tutaangalia utaratibu mzuri zaidi ambao utakuwa na tija kwa wanafunzi, wahadhiri na Taifa kwa ujumla,” alisema Profesa Ndalichako.

Aliongeza kuwa walimu wanaofundisha stashahada ya ualimu wa masomo ya sayansi walianza mgomo Mei 9, mwaka huu kutokana na madai ya malipo ya muda wa ziada wanaotumia kuwafundisha wanafunzi hao.

Alisema baada ya malalamiko uongozi wa chuo uliamua kuhakiki madai yao na yalipohakikiwa yalionekana yapo juu kwa mujibu wa sera ya chuo na uzito wa kazi, yaani walipaswa kulipwa posho hiyo.

Profesa Ndalichako alisema kuwa kiasi cha madai kilichowasilishwa ni Sh milioni 934 wakati fedha zilizohakikiwa ni Sh milioni 252 kiasi ambacho waajiri wamekipinga.



UAMUZI WAPINGWA

Hata hivyo uamuzi huo wa Serikali kuwaondoa wanafunzi wa Udom chuoni uliotolewa bungeni na Profesa Ndalichako umepingwa kila kona na wadau mbalimbali wakiwamo walimu, wazazi wa watu wa kawaida.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimemuomba Rais Magufuli kumaliza sakata hilo la wanafunzi bila kuendelea kuwaathiri.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Helen Kijo- Bisimba, alisema Dar es Salaam jana kuwa Rais Magufuli anapaswa kuliangalia kwa jicho la karibu tatizo la wanafunzi hao kwa sababu wananyanyasika na kudhalilishwa.

“Kimsingi mgogoro ulipofikia Rais Dk. Magufuli aone umuhimu wa kusuluhisha kwani kwa taarifa zilizopo wanafunzi hawa wanadhalilika, kunyanyasika wakati waliowapeleka chuoni hapo ni Serikali yenyewe,” alisema Dk. Helen ambaye pia ameutaka uongozi wa Bunge kuwarejesha wabunge wote waliosimamishwa waendelee na vikao ili kuwawakilisha wananchi wao.

Dk. Helen alisema kuwaondoa wanafunzi hao bila kuwapa nauli, kuwaandalia mazingira salama ni hatari kwa kuwa wengi wametoka kwenye familia masikini na hawakuja kimakosa katika chuo hicho bali ilikuwa mpango wa Serikali.

Alisema mgomo wa walimu wa kudai masilahi haukupaswa kuwaadhibu vijana hao na badala yake Serikali ichukue nafasi ya kuzungumza na walimu hao ili kumaliza tatizo hilo kwa njia ya amani.

“Inasikitisha watoto hao kufukuzwa chuoni, tena kwa kupewa saa 24 kama wahalifu wa makosa ya jinai wakati waliingia chuoni hapo kwa taratibu na vigezo vya Serikali kupitia Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).

“Watoto hawa wametimuliwa kama wakimbizi au wahalifu kwa kupelekewa polisi wenye mabomu ya machozi bila kujali hali yao ya kiuchumi, kisaikolojia wala utu, huu ni ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa ndani ya nchi ambayo inajinasibu kutekeleza demokrasia, sheria na haki za binadamu.

“Kwa maana hiyo kiongozi huyo haoni haja ya maisha ya wanafunzi hao hata kama wakibakwa, kutekwa, kuuawa kwani kwake hilo si jambo la dharura na halihitaji muda wa kujadiliwa,” alisema Dk. Helen.



WABUNGE KUTIMULIWA

Aidha Dk. Helen alizungumzia kusimamisha wabunge saba wa upinzani wasihudhurie vikao vya bunge vikiwamo vya bajeti.

Alisema miezi sita tangu bunge la 11 lianze hakuna jipya ndani ya Bunge hilo mbali ya kushuhudia likiendeshwa kibabe na kisiasa.

“Katika kuonyesha ubabe wa kiti cha Spika wa Bunge hilo, tumeshuhudia wabunge saba wakipewa adhabu ya kutohudhuria vikao kwa vipindi tofauti kwa madai wamekidharau kiti katika kikao cha Januari 27, mwaka huu,” alisema.

Wabunge waliosimamishwa ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Esther Bulaya (Bunda Mjini), Pauline Gekul (Babati Mjini), Godbles Lema (Arusha Mjini), Halima Mdee (Kawe, John Heche (Tarime Vijijini) na Zitto Kabwe (Kigoma Mjini).



KAGERA

Mwenyekiti wa Chama Cha Walimu (CWT) Mkoa wa Kagera, Paul Kosta alisema uamuzi wa Serikali kuwarudisha nyumbani wanafunzi wa Udom kwa muda usiojulikana hauna nia njema kwa mustakabali wa elimu nchini.

Kosta ambaye pia ni mwalimu wa hisabati katika Shule ya Sekondari Rutabo iliyopo Tarafa ya Kamachumu wilayani Muleba, alisema lengo la Serikali kuweka utaratibu wa kusomea shahada kwa wanafunzi hao si wa bahati mbaya kwani ulitokana na nia yake ya kupunguza pengo la walimu wa sayansi linalolikabili taifa kwa sasa.

“Tumesikitishwa na hatua hiyo, mahitaji ya taifa kwa walimu wa sayansi bado ni makubwa kwa shule za msingi na sekondari, tunaambiwa Serikali ya sasa imevunja rekodi ya ukusanyaji kodi, kwanini inashindwa kuwalipa wahadhiri? alihoji.

Sunday Bubelwa ambaye ni mjasiriamali katika Mji mdogo wa Kamachumu alipiga simu MTANZANIA akisema hakuona sababu ya Naibu Spika kupinga hoja na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari bungeni juzi.

“Vijana wetu tunasikia wamegeuka ombaomba na machangudoa katika mji wa Dodoma, Sisi tunajua mawaziri na baadhi ya wabunge wa CCM wanafanya hivyo kwa sababu watoto wao hawako katika mazingira kama hayo,” alisema Bubelwa.



DAR

Athman Mwamtemi ambaye ni dereva teksi katika Mtaa wa Samora jijini humo alisema: “Dk. Tulia amepotoka, hayo ni matumizi mabaya ya kiti kwa kukiuka haki ya msingi ya Bunge hilo kujadili suala zito kama hilo la elimu kwa watoto wa Tanzania.

“Ni haki ya wabunge kutetea masuala ya wananchi, hakuna sababu ya kuwafungia, haya ni matumizi mabaya ya kiti na hapa Naibu Spika amepotoka, anapaswa kukubali hilo na anapaswa kusahihisha makosa na kuacha ubabe,” alisema Chande.



WANAFUNZI UDSM WAGOMA

Wanafunzi wa shahada ya kwanza wanaonufaika na mkopo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), sehemu ya Mlimani, wameingia kwenye mgomo kutokana na kucheleweshwa kwa fedha za kujikimu, huku wakimtaka RaisMagufuli kuwatumbua viongozi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB).

Pia wanafunzi hao wamekumbusha ahadi za Rais Magufuli wakati wa kampeni kuwa katika Serikali yake hatomvumilia kiongozi wa bodi atakayechelewesha fedha za kujikimu za wanafunzi wa elimu ya juu.

Vuguvugu la mgomo huo lilianza juzi usiku katika hosteli za wanafunzi hao zilizopo Mabibo ambapo inadaiwa walikuwa wanapiga kelele za kudai fedha hizo wakilalamika kuwa wana njaa.

Akizungumza na MTANZANIA jana katika eneo linalotumika kwa mikutano ya wanachuo maarufu kama ‘Revolution Square’, mmoja wa wanafunzi ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini kwa kuhofia kufukuzwa chuo, alisema juzi walikutana na Rais wa Serikali ya Wanafunzi (DARUSO) ambaye aliahidi kuitisha mkutano wa wanafunzi wote kujua hatima ya malipo yao.

“Tumekusanyika hapa kutokana na agizo la rais wetu kuwa atakuja kuzungumza juu ya madai yetu ya kucheleweshewa fedha, jana (juzi) tulianza harakati hizo katika hosteli za Mabibo na leo (jana) hatujaingia darasani na hatutaingia hadi tupate fedha zetu,” alisema mwanafunzi huyo.

MTANZANIA ilifika katika eneo hilo jana saa 4 asubuhi na kushuhudia baadhi ya wanafunzi wakiwa wamekusanyika huku wengine wakipita kuelekea madarasani kuendelea na masomo kama kawaida.

Ilipofika saa 7 mchana rais wa DARUSO, Erasmi Leoni, aliwasili katika eneo hilo ambapo aliwataka wanafunzi hao kuwa na subira wakati akiendelea kuwabana utawala kutoa majibu huku akiwataka waendelee kubaki katika eneo hilo hadi watakapopata majibu ya kuridhisha.

“Naungana na ninyi kuendelea kukaa hapa hadi tutakapopata fedha zetu na tunatoa nusu saa kwa uongozi wa chuo kutupa majibu ya kupata fedha hizo leo (jana) na kama hawatatoa majibu ya kuridhisha tutachukua hatua zaidi,” alisema.

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Mikopo Tanzania ambaye pia ni Waziri wa Mikopo mstaafu wa UDSM, Evance Shitindi, alisema atashangaa kuona wanafunzi wanafukuzwa kwa mgomo huo badala ya kufukuzwa viongozi wa bodi huku akikumbushia ahadi ya rais kwa kuweka katika kipaza sauti, sauti iliyorekodiwa ya Rais Magufuli iliyokuwa katika simu yake.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Rwekaza Mkandala, aliliambia MTANZANIA kuwa chuo hakina mamlaka ya upatikanaji wa fedha hizo, lakini wanashirikiana na bodi kuhakikisha zinapatikana kwa wakati.

“Sisi kazi yetu ni kuhakiki majina ya wanafunzi wanaopokea mikopo ili kusiwepo hewa, lakini mpaka wakati huo waliwasiliana na bodi ya mikopo kwamba wamepeleka fedha hizo benki,” alisema Profesa Mkandala.

Mkurugenzi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo, Cosmas Mwaisoga, alisema mchakato wa malipo umekwishafanyika na hundi za malipo hayo zimepelekwa benki.

“Siku ya malipo ilikuwa ni Mei 28 mwaka huu ambayo ilikuwa Jumamosi na sisi siku hiyo hatufanyi kazi ndiyo maana sasa tunapigana kuharakisha mchakato ili wapate fedha zao haraka iwezekanavyo,” alisema.



CHUO CHA MAJI

Zaidi ya wanachuo 40 wanaosoma shahada ya uhandisi wa maji na umwagiliaji katika Chuo Kikuu cha Taasisi ya Maji (WDMI) nao wameandamana kwenda Bodi ya Mikopo wakilalamikia kucheleweshewa fedha za chakula na kujikimu.

Akizungumza na MTANZANIA kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, mmoja wanachuo hao alisema wamefikia hatua hiyo baada ya bodi hiyo kushindwa kutoa fedha zilizotakiwa tangu Mei 20, mwaka huu.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho, Joseph Ikingu alisema taarifa waliyoipata kutoka kwa ofisa mikopo wa chuo hicho ni kwamba taratibu za kusaini hundi kwa ajili ya kutolewa fedha hizo zilikwishakamilika.

Meneja Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo nchini, Omega Ngole aliliambia MTANZANIA kuwa wanafunzi hao wanachokifanya ni upotoshaji kwani tarehe waliyopaswa kuanza kupokea mikopo yao ni Mei 26, mwaka huu hivyo hakukuwa na ucheleweshwaji.

Habari hii imeandaliwa na LEONARD MANG’OHA (MSJ), CHRISTINA GAULUHANGA NA FROLIAN MASINDE (DAR ES SALAAM), Ramadhan Hassan, Aziza Masoud (Dodo
0 Toa maoni yako.

JPM awatangazia vita wafanyabiashara ‘wajanja’

Rais John Magufuli kwenye hafla ya utaoji wa Tuzo ya Rais ya wazalishaji bora wa viwandani kwa mwaka 2015 zilizofanyika jijini Leo Dar es Salaam.
Kwa ufupi

Rais Magufuli ameyasema hayo leo kwenye hafla ya utaoji wa Tuzo ya Rais ya wazalishaji bora wa viwandani kwa mwaka 2015 zilizofanyika jijini Dar es Salaam.By Raymond Kaminyoge, Mwananchi rkaminyoge@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema Serikali yake itaendelea kupambana na wanaoingiza bidhaa zilizochini ya kiwango na wale wanaokwepa kodi.

Amesema kwa kufanya hivyo, wanachangia kuviua viwanda vya ndani ya nchi.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo kwenye hafla ya utaoji wa Tuzo ya Rais ya wazalishaji bora wa viwandani kwa mwaka 2015 zilizofanyika jijini Dar es Salaam.

Tuzo hizo zimeandaliwa na Shirika la Wenye Viwanda Nchini (CTI).

Rais amesema pia hatawavumilia watendaji wote watakao wakwamisha wafanyabiashara wenye nia ya kuanzisha viwanda nchini kwa sababu zisizo za msingi na kuwaahidi kuwasaidia waweze kufanikisha ndoto zao.

Pia, amesema ni vizuri wafanyabiashara wote nchini wakatumia fursa zipatikanazo katika awamu hii ya uongozi wake, ili wasije kuzijutia baadaye.

“Nasema kwa dhati kutoka moyoni, you have my support, mkishindwa katika kipindi cha awamu ya tano basi hamtaweza tena,” alisema.

Rais Magufuli alisema nchi inapokuwa na viwanda vingi vitatoa ajira kwa Watanzania, vitaongeza mapato kwa Serikali na kuingiza fedha za kigeni kwa kuuza bidhaa nje ya nchi.

“Nina dhamira ya dhati ndani ya moyo wangu kuwasaidia wenye nia ya kuanzisha ya viwanda, siwachukii matajiri nawapenda matajiri,” alisema.

Rais Magufuli aliwapa moyo wafanyabiashara wenye viwanda kuanzisha vingine ili Serikali iweze kunufaika zaidi.

Alisema Tanzania ina rasilimali nyingi kama maliasili na madini na akawahakikishia wawekezaji kuwa lipo soko kubwa la bidhaa watakazozitengeza lenye watu milioni 160 katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Magufuli alisema sekta ya viwanda ni muhimili mkubwa wa uchumi katika nchi huku akitolea mfano wa nchi za China, India, Korea Kusini, Malaysia, Thailand na Vietnam ambazo zimekuwa kwa kasi kwa sababu ya uwepo wa viwanda.

Alisema viwanda vinapoanzishwa nchini badala ya kuuza mali ghafi kwa bei ndogo zitatengenezwa bidhaa ambazo zitauzwa nje ya nchi na kutoa ajira kwa Watanzania.

“Badala ya kuuza ngozi tutengeneze viatu hapa hapa nchini au badala ya kuuza ng’ombe Comoro tumepeke nyama iliyosindikwa,” alisema.

Alisema nchi kama ya Sudan Kusini ina mahitaji makubwa ya unga wa mahindi.

“Lakini wanaofaidika na soko hilo ni Wakenya ambao wanakuja nchini wananunua mahindi, wanasaga na kuyapeleka huko,hivi wafanyabiashara tunashindwa hata kuanzisha viwanda vya kusaga mahindi,” alisema

Alisema Mkoa wa Arusha una ng’ombe wa maziwa lakini yananunuliwa na Wakenya ambao wanayasindika kwenye viwanda vyao na kuja kuyauza hapa nchini.

Hata hivyo, alisema Serikali inaangalia uwezekano wa kuanzisha benki ya maendeleo ya viwanda kwa lengo la kutoa mikopo yenye masharti nafuu na riba ndogo.

Kuhusu kuondoa kwa changamoto mbalimbali zinazokwamisha maendeleo ya viwanda nchini, Magufuli alisema Serikali imeshatenga Sh1trilioni katika mwaka wa fedha ujao kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kati kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.

Pia, Serikali imeunda kamati maalumu itakayoangalia mazingira ya ufanyaji biashara nchini ikiwamo kodi na tozo mbalimbali.

“Nchi yetu inakuwa na kodi za ajabu ajabu, mfano zao la kahawa kulikua na zaidi ya kodi 30. Haya ndiyo tunayoyaangalia,” alisema.

Kuhusu upatikanaji wa mitaji na riba kubwa zinazotozwa na benki, alisema katika kukabiliana na matatizo hayo Serikali inajiandaa kuanzisha benki ya viwanda itakayowasaidia wenye wawekezaji.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema Serikali imejikita katika kuhamasisha ujenzi wa viwanda vingi zaidi nchini.

“Tumeandaa mkakati wa pamba hadi inakuwa nguo, alizeti hadi mafuta na tunaendelea kufufua viwanda vilivyokufa,” alisema.

Akizungumzia changamoto zinazowabiri wenye viwanda nchini, mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Samuel Nyantahe alisema uchakavu wa miundombinu ya umeme na miundombinu ya barabara imekuwa ikiongeza gharama za uzalishaji.

Pia, alilalamikia uwapo wa utitiri wa kodi, mamlaka za usimamiaji biashara na uwapo wa bidhaa bandia zinazotishia bidhaa za ndani.



0 Toa maoni yako.

WWF:Mbuga ya Selous Tanzania kupoteza Tembo wake

Rushwa ni moja ya sababu iliyochochea vita dhidi ya ujangili kutokwisha

Hifadhi ya wanyama pori ya taifa ya Selous Kusini mwa Tanzania inatajwa kuwa huenda ikapoteza tembo waliosalia ndani ya miaka sita ijayo iwapo hali ya ujangili itaendelea kwa kiwango kilichopo sasa.

Ripoti ya mfuko wa hifadhi ya wanyamapori na mazingira duniani,wwf imesema hifadhi Selous imepoteza asilimia tisini ya tembo wake,ambapo miaka 40 iliyopita kulikuwa na maelfu ya tembo.

Mahitaji makubwa ya nyara hizo na nchi ya China,kwa mjibu wa ripoti hiyo inatajwa kuwa ni hali inayochochea ujangili na mauaji ya idadi kubwa ya tembo.

Rais wa awamu ya tano wa Tanzania John Pombe Magufuli katika utawala wake ametanga kukomesha rushwa ambayo ndiyo imekuwa ikichangia kukua kwa vitendo vya ujangili.

"hifadhi hiyo ya Selous ni moja kati ya urithi wa dunia kufuatia kuwa na eneo kubwa la wanyama pori lililosalia Barani Afrika.
0 Toa maoni yako.

Ukawa kuzunguka nchi nzima

Na Khamis Mkotya, Dodoma

VYAMA vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vinakusudia kufanya ziara ya kuzunguka nchi nzima kuwaeleza wananchi kilichotokea bungeni hadi wabunge wa upinzani wakafukuzwa.

Mpango huo ulitangazwa jana na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe katika viwanja vya Bunge alipozungumza na waandishi wa habari.

Alifanya hivyo ikiwa ni siku moja tangu wabunge saba wa upinzani wasimamishwe kuhudhuria vikao vya Bunge, baada ya kukutwa na makosa ya kudharau kiti na kufanya fujo bungeni.

Uamuzi huo wa Bunge ulitolewa kwa kuridhia mapendekezo ya adhabu yaliyotolewa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, baada ya kuwahoji wabunge hao kutokana na kufanya vurugu katika mkutano wa pili wa Bunge wa Januari 27, 2016 kuhusu matangazo ya Bunge ‘Live’.

Wabunge waliowekwa kifungoni kwa vipindi tofauti ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul.

Wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee wote kutoka Chadema na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe wa Chama cha ACT- Wazalendo.

Mbowe alisema baada ya kutoka bungeni, wabunge wa kambi hiyo watakutana kujadili na kupanga mikakati ya pamoja kufanya siasa nje ya Bunge, kutokana na mwenendo wa kiongozi huyo wa Bunge na hatua ya wabunge wa upinzani kufukuzwa.

“Siasa haifanywi ndani ya Bunge pekee, siasa inafanywa pia nje ya Bunge na tutafanya siasa nje ya Bunge, tutakwenda kuwashitaki kwa wananchi juu hiki kilichotokea bungeni wananchi waelewe,” alisema.

Alipoulizwa anazungumziaje habari ya kufanya siasa bungeni wakati kinachopaswa kufanywa ndani ya Bunge ni hoja, Mbowe alisema: “Mimi sijui hoja ni nini na siasa ni nini? Lakini kwangu mimi kinachofanyika bungeni ni siasa kwa asilimia 100, tunakwenda kukutana na wenzetu kupanga,” alisema.

Hiyo itakuwa mara pili kwa vyama vya upinzani kwenda kwa wananchi. Mwaka 2007 aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe wakati huo akiwa Chadema, aliwahi kusimamishwa kwa miezi mitatu kuhudhuria vikao vya Bunge kutokana na hoja ya Buzwagi.

Kutokana na adhabu hiyo, Chadema kwa kushirikiana na vyama vingine vya upinzani kiliratibu na kufanya ziara nchi nzima kuwaeleza wananchi kuhusu adhabu ya Zitto.

Zitto aliibua hoja binafsi akituhumu liyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi kwamba alisaini mkataba wa Buzwagi hotelini Uingereza kinyume na utaratibu.

Waanza kumsusia Dk. Tulia

Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni jana ilianza kutekeleza azimio lake la kutokuwa na imani na Naibu Spika, Dk. Ackson Tulia.

Hatua hiyo ilijitokeza jana asubuhi wakati wabunge wa kambi hiyo walipotoka nje baada ya Naibu Spika kumaliza kusoma dua ikiwa ni ishara ya kuanza kwa shughuli za Bunge.

Juzi kambi hiyo ilitangaza kutokuwa na imani na Naibu Spika kwa kile kilichoelezwa kuwa kiongozi huyo analiyumbisha Bunge katika kutekeleza majukumu yake.
0 Toa maoni yako.

Wanasayansi China watumia nguruwe kutibu upofu

Wanasayansi wa Uchina wamefaulu katika tiba yao mpya ya majaribio ya kutibu upofu.

Walitumia nguruwe katika majaribio hayo ya tiba ya kuondoa upofu, ambapo walitumia konea kutoka kwa wanyama hao.

Sasa wamesema wana imani kwamba hilo litafaa sana kutokana na uhaba wa konea za binadamu.

Inakisiwa kuwa Wachina wapatao 5 milioni wanakabiliwa na matatizo ya konea, sehemu ya mbele ya jicho iliyo ngumu na inayowezesha miali ya mwanga kupenya.

Lakini ni konea 5,000 pekee ambazo hupatikana kila mwaka.

Matatizo ya konea husababisha watu wengi kuwa kipofu.Image copyrightGETTY

Njia hiyo mpya ya kutibu upofu imeanza kutumiwa baada ya kuidhinishwa na serikali mwaka jana.

Konea kutoka kwa nguruwe hutibiwa na kutolewa bakteria na virusi, pamoja na kutolewa DNA ya nguruwe, kabla ya kupandikizwa katika jicho la mwanadamu.

Wakosoaji wa mpango huo wanasema Uchina inaenda kwa kasi sana, bila kuangazia madhara ya mpango huo kwa kipindi kirefu
0 Toa maoni yako.

Trump apata wajumbe wa kutosha Marekani

Mgombea wa urais kupitia tiketi ya chama cha Republican Donald Trump amefikisha idadi ya wajumbe ya kupata uteuzi wa chama hicho kulingana na chombo cha habari cha AFP.

Bw Trump ambaye aliwashinda wagombea wengine 16 wa chama hicho ameripotiwa kupata wajumbe 1,238 mmoja zaidi ya inavyohotajika.

Chama cha Republican kinataraijiwa kukamilisha uteuzi wao katika mkutano wa chama hicho utakaofanyika huko Cleveland mnamo mwezi Julai.

Iwapo atathibitishwa ,bw Trump atakabiliana na aliyekuwa waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani Hillary Clinton au seneta wa Vermont Bernie Sanders ambao wanashindania uteuzi wa chama cha Demokrat.

Siku ya Jumatano,bilionea huyo wa New York alipanga kufanya mjadala na Bernie Sanders katika runinga mjini California kabla ya uchaguzi wa mchujo wa tarehe 7 mwezi Juni.

Bw Sanders alikubali kushiriki katika mjadala huo katika ujumbe wake wa Twitter uliosema: ''Game on''.
1 Toa maoni yako.

MAGAZETI YA LEO MEI 27 2016











































































ULIMISS HII KAULI MPYA YA DIAMOND PLATNUMZ, BAADA YA SOUTH AFRICA
0 Toa maoni yako.

Mawaziri Yona na Mramba Waanza Kutumikia Kifungo cha nje...Wakabidhiwa Vifaa vya Usafi

Mawaziri wa zamani Basil Pesambili Mramba na Daniel Yona wameripoti leo katika hospitali ya Sinza Palestina na kukabidhiwa vifaa kwa ajili ya kufanya usafi.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliridhia Mawaziri hawa wastaafu kutumikia adhabu ya kifungo cha nje kwa kufanya usafi katika maeneo ya kijamii ikiwemo Hospitali ya Sinza Palestina.
0 Toa maoni yako.

Dk. Manyaunyau Ahukumiwa Jela Miaka 3 Kwa Kushindwa Kufufua Maiti

Mkazi wa Dar es Salaam, Dunia Salumu maarufu kwa jina la Dk. Manyaunyau, amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela pamoja na kulipa fidia ya Sh milioni 10 baada ya kupatikana na hatia ya kujipatia fedha Sh milioni 29.6 kwa njia ya udanganyifu.

Manyaunyau anadaiwa kujipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kwa mlalamikaji, Tekra Modesta kama malipo ya kazi ya kumfufua marehemu kaka yake aliyefahamika kwa jina moja la Modest ambaye alifariki dunia miaka kadhaa iliyopita.

Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Flora Haule, alisema mtuhumiwa huyo ametiwa hatiani baada ya ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka kujitosheleza.

“Mahakama inatoa hukumu kwa mtuhumiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa fidia ya Sh milioni 10 baada ya kumaliza kutumikia kifungo chake ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo,” alisema Hakimu Flora.

Upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi wanne ambao wote waliithibitishia mahakama juu ya mtuhumiwa kujipatia kiasi hicho cha fedha kwa njia za udanganyifu.

Awali Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Estar Kyala, aliiambia mahakama kuwa hakuna kumbukumbu za makosa ya nyuma dhidi ya mshtakiwa na hivyo kuiomba kutoa adhabu kali ili kuwa fundisho kwa wote wenye tabia kama hizo.

Katika maelezo ya awali, ilidaiwa kuwa mtuhumiwa alijipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kwa mlalamikaji kama malipo ya tukio la kutaka kumfufua kaka wa mlalamikaji.

Ilielezwa kuwa mtuhumiwa alipokea fedha hizo kwa awamu mbili tofauti ambapo awali Mei 2007 jijini Dar es Salaam alipewa kiasi cha fedha ambacho hakikufahamika.

Mei Mosi, mwaka 2008 mtuhumiwa alipokea kiasi kingine cha fedha kama malipo kwa ajili ya kumalizia kazi yake ya kumfufua marehemu ambaye ni ndugu wa mlalamikaji jambo ambalo alishindwa kulitekeleza.

Manyaunyau amejizolea umaarufu mkubwa katika maeneo mengi nchini kwa kile kinachodaiwa kuwa anao uwezo wa kutibu na kuwafichua wachawi popote walipo sambamba na staili yake ya kunyonya damu ya paka akiwa katika shughuli zake za uganga.

Katika tukio lililovuta wakazi wengi wa Dar es Salaam, Manyaunyau anadaiwa kumwibua nyoka ambaye alikuwa tishio na kuzusha hofu kubwa kwa wakazi wa maeneo ya Manzese Midizini ambapo ilidaiwa kuwa alikuwa akiwagonga watu katika mazingira ya kutatanisha katika njia inayopita kwenye makaburi.

Inaaminika kuwa baada ya kuitwa, Dk. Manyaunyau aliweza kumuibua nyoka huyo na kuonekana hadharani tukio lililohisiwa kuwa ni la kimazingara zaidi.
0 Toa maoni yako.

Kesi ya Ubunge wa David Kafulila Yaahirishwa Hadi Jumatatu Novemba 30 Baada ya Mlalamikiwa Kutofika Mahakamani

Kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila, kupinga matokeo ya ubunge yaliyomtangaza mshindi Husna Mwilima, katika jimbo hilo, imeahirishwa hadi Novemba 30, mwaka huu.
Kesi hiyo ipo mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, John Utamwa.

Jaji Utamwa alisema mlalamikiwa (Mwilima), katika madai hayo, hakupelekewa wito wa mahakama, hivyo anaamuru wito utolewe ili mlalamikaji aende mahakamani kujibu madai hayo ambayo anatetewa na mwanasheria wa serikali, Juma Masanja.

Akizungumza baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, Wakili wa mlalamikaji, Daniel Rumenyela, alidai mlalamikiwa (Mwilima), hakupatikana kwa ajili ya kuitwa shaurini hata akipigiwa simu hapokei.

“Kutokana na mlalamikiwa wa kwanza kutopatikana, Mahakama Kuu Kanda ya Tabora inatoa siku tatu hadi Novemba 30, mwaka huu, (Jumatatu), ajibu madai hayo,” alisema Rumenyela.

Kesi hiyo namba 2 ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo, pia ina washtakiwa wengine ambao ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Uvinza ambaye alikuwa Msimamizi wa Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika kesi hii ndogo ya awali kabla ya kesi ya msingi, Mahakama itaamua gharama ambazo Kafulila atatakiwa kulipa kama gharama za dhamana ambayo kisheria kwa washtakiwa watatu haizidi Sh. milioni 15.

Katika kesi ya msingi, Kafulila anaomba Mahakama imtangaze mgombea aliyepata kura nyingi kwani aliyetangazwa siye mbunge halali kutokana na kupata kura chache.

Katika shauri hilo, Kafulila alimtaja Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya na Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mrisho Gambo, kama wahusika waliofikisha ujumbe huo toka juu Oktoba 28, mwaka huu, saa 8:00 mchana kwa Msimamizi wa Uchaguzi kushinikiza matokeo batili kutangazwa.
0 Toa maoni yako.

MAZISHI YA MAWAZO BADO KIZUNGUMKUTI. CHADEMA KUTINGA MAHAKAMANI.

Na:George Binagi-GB Pazzo @BMG
Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema kimesitisha shughuli za mazishi ya aliekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoani Geita marehemu Alphonce Mawazo, baada ya jeshi la polisi Mkoani Mwanza kuzuia zoezi la kuuaga mwili wake lililokuwa limepangwa kufanyika juzi jumamosi Jijini Mwanza.

Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Freeman Mbowe alibainisha hayo jana wakati akizungumza na Wanahabari Mkoani Mwanza, ili kutoa msimamo wa Chama baada ya kuwepo kwa mazungumzo baina yake na familia ya marehemu Mawazo.

Alisema kuwa baada ya mazungumzo hayo, Chadema pamoja na familia ya marehemu Mawazo wamekubaliana kwenda Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kufungua shauri la kuomba tafsiri ya Kimahakama juu ya zuio hilo la jeshi la polisi kuzuia mwili wa marehemu Mawazo kuagwa Jijini Mwanza kabla ya Kwenda kuzikwa Kijijini kwake Chikobe katika Wilaya ya Busanda Mkoani Geita.

Nae Mchungaji Charles Lugiko ambae ni baba mlezi wa marehemu Mawazo, alisema anasikitishwa na hatua iliyochukuliwa na jeshi la polisi ya kuzuia mwili wa marehemu Mawazo kuagwa Jijini Mwanza ambapo ameeleza kuwa na matumaini makubwa ya kwamba mahakama itatenda haki juu ya suala hilo.

Frederick Sumaye pamoja na Edward Lowasa ambao ni Viongozi Waandamizi wa Chadema, walisema hatua ya jeshi la polisi kuzuia mwili wa Mawazo kuagwa Jijini Mwanza si sawa na kwamba inaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza kupitia kwa Kamanda wake Charles Mkumbo, lilizuia zoezi la mwili wa marehemu Mawazo Kuagwa Jijini Mwanza, kwa madai kwamba limepokea taarifa za kiitelejensia za kuwepo baadhi ya vikundi vya watu kutumia mwanya huo kufanya fujo na hivyo kuhatarisha usalama wa raia na mali zao.

Aidha Kamanda Mkumbo aliitaja sababu nyingine kuwa ni uwepo wa mlipuko wa Ugonjwa wa Kipindupindu Mkoani Mwanza, ambao umesababisha jeshi hilo kutoruhusu mikusanyiko ya aina yoyote inayoweza kusababisha ugonjwa huo kuenea zaidi kwa mjibu wa wataalamu wa afya ambapo lilishauri zoezi la kuaga mwili huo kufanyika Mkoani Geita ambapo mazishi ya marehemu Mawazo yatarajiwa kufanyika.

Katika uchaguzi uliomalizika hivi karibuni, marehemu Alphone Mawazo alikuwa mgombea ubunge Jimbo la Busanda Mkoani Geita kupitia Chadema, akiwa pia ni Mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo ambapo aliuawa kikatili kwa kukatwa mapanga na mashoka na watu wasiojulikana jumamosi iliyopita ya Novemba 14 mchana huku kifo chake kikihusishwa na uhasama wa kisiasa.
0 Toa maoni yako.

Saed Kubenea Kumburuza Mahakamani Spika wa Bunge Job Ndugai Kwa Kuvunja Kanuni Na Kuwaruhusu Polisi Kuingia Bungeni

Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea amesema atamfikisha mahakamani Spika wa Bunge, Job Ndugai kwa kuvunja kanuni baada ya kuwaingiza polisi ndani ya ukumbi wa chombo hicho.

Polisi hao waliingia ndani ya ukumbi huo wiki iliyopita wakati Rais John Magufuli alipofika kwa ajili ya kuhutubia Bunge.

Kubenea alisema kitendo cha askari kuingia ndani ya Bunge kwa mara ya mwisho kilitokea nchini Uingereza mwaka 1930 na hakijawahi kutokea tena isipokuwa nchini.

Alisema kuwa kesi hiyo anatarajia kuifungua Mahakama Kuu wiki ijayo kwa ajili ya kutaka tafsiri ya kanuni hiyo.

Hata hivyo, mkurugenzi wa shughuli za Bunge, John Joel alisema hakuna kanuni iliyovunjwa kwa askari hao kuingia ndani ya Ukumbi wa Bunge.
   Wakati Kubenea akiandaa mpango huo, Kamati ya Wabunge CUF imesema Spika Ndugai ndiye chanzo cha yaliyotokea bungeni.

Ijumaa wiki iliyopita wakati Rais akiingia kutoa hotuba ya kuzindua Bunge, wabunge hao walipiga kelele wakitaja jina la mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kuonyesha msimamo wao dhidi ya uamuzi wa kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa visiwa hivyo.

Walipiga kelele hizo wakati Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein akiingia kwenye ukumbi huo na baadaye wakati Dk Magufuli akiingia ukumbini na wakagoma kunyamaza hadi walipotakiwa kutoka nje na askari kuitwa ndani.

Wabunge wa upinzani wanadai kuwa Dk Shein si Rais wa Zanzibar, wala makamu wake wa pili, Balozi Seif Ali Iddi na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho kwa madai kuwa muda wao uliisha Novemba 2, baada ya Uchaguzi Mkuu.

Jana wabunge wa CUF chini ya Mwenyekiti wake, Juma Hamad Omary walitoa tamko lililokemea na kutoa tahadhari kwa mambo mawili huku wakimtaka Ndugai kutoyumbishwa na Serikali.

Katibu wa Umoja huo, Hamudu Hassan Bobal alisema vurugu zisingetokea endapo Bunge hilo lingezingatia tamko la barua ya Ukawa na kusikilizwa hoja ya mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu aliyeomba mwongozo akitaka kujua Dk Shein na wenzake wanaingiaje bungeni wakati madaraka yao yaliisha tangu Novemba 2.
0 Toa maoni yako.

Wabunge Wagonga Mwamba Kwa Rais Magufuli......Agoma Kuwaongoza Hela Ya Posho,Apunguza Mikopo Ya Mashangingi

Wakati Serikali ikihaha kutafuta fedha kwa ajili ya kuendeshea shughuli zake, wabunge wameingia kwenye mvutano na ofisi ya Bunge kuhusu fedha ambazo wanastahili kupewa kwa ajili ya kununulia magari yao.

Mwaka 2010, wabunge walilipwa Sh90 milioni kwa ajili ya ununuzi wa magari hayo aina ya Toyota Land Cruiser (hardtop), ambayo ni vitendea kazi vyao. Wabunge hutakiwa kulipa nusu ya fedha hizo wkati nyingine ni mchango wa Serikali.

Lakini wakati gharama za maisha zikipanda huku thamani ya Shilingi ikiporomoka kulinganisha na Dola ya Marekani na hivyo kusababisha bidhaa kupanda bei, wabunge wamekataa kulipwa kiasi hicho cha fedha mwaka huu na badala yake wanataka walipwe kulingana na bei ya sokoni ya magari aina hiyo.

Wabunge wanataka walipwe Sh130 milioni ambazo wanasema ni bei ya magari hayo kwa sasa baada ya kupanda bei. Hata hivyo ombi hilo limegonga mwamba

Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina, baadhi ya wabunge walisema mara baada ya kujisajili bungeni kwa ajili ya uzinduzi wa Bunge la Kumi na Moja, katibu wa chombo hicho, Dk Thomas Kashililah alifanya kikao na wabunge wote ili kuwapa taratibu lakini pia kuwafahamisha stahili wanazopaswa kupata kama wabunge.

“Katibu alitujulisha kuwa hakuna ongezeko lolote la posho, hivyo tunapaswa kulipwa kiasi kilekile cha Sh300,000 kwa siku .

"Lakini pia alisema tutapewa Sh90 milioni kwa ajili ya mkopo wa garibadala ya milioni 120 ,” alisema mmoja wa wabunge hao.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, suala hilo liliibua mjadala na kusababisha wabunge kuhoji iweje kiwango hicho kitumike katika Bunge la Kumi na Moja, miaka mitano baada ya wabunge wa Bunge la 10 kupewa kiasi hicho.

“Unajua magari tunayotakiwa kununua ni Toyota Land Cruiser Hardtop, na ukweli sasa thamani ya magari hayo imepanda sana huwezi kuifananisha na mwaka 2010 wakati wa Bunge la 10,” alisema mbunge mmoja.

Wabunge hao walitaka walipwe kiasi cha Sh130 milioni kwa madai kuwa ndiyo bei ya sokoni ya magari aina hiyo.

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Anatropia Theonest amesemahawajakataa fedha hizo, lakini thamani ya Dola imepanda hivyo kusababisha thamani ya magari hayo kupanda pia.

“Hakuna asiyejua kwamba thamani ya Dola imepanda na kwa kawaida kila Bunge kunakuwa na ongezeko la Sh30 milioni. Mfano Bunge la Tisa walipewa Sh60milioni la 10 wakapewa Sh90milioni, hivyo ilipaswa sasa iwe Sh 120mililioni ili kuendana na soko,” alisema mbunge huyo.

Akizungumzia sakata hilo,naibu katibu wa Bunge, John Joel alisema jukumu la ununuzi wa magari ya wabunge, lipo chini ya Serikali na siyo ofisi yake hivyo ni bora wangeulizwa wenye jukumu hilo.

“Tunachofamu sisi mbunge anatakiwa apewe vitendea kazi likiwemo gari, lakini wanaohusika na hilo ni Serikali,” alisema.

Alisema ofisi ya Bunge hushauriana na Serikali namna ya kutoa huduma kwa wabunge na kwamba kwa jinsi anavyofahamu, mpaka jana watunga sheria hao walikuwa hawajapewa fedha yoyote ya kununua magari kwa awamu hii, hivyo wanasubiri utaratibu.

Wakati Joel akisema Serikali ndiyo inahusika, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue aliurudisha mpira kwenye ofisi hiyo ya Bunge, akisema uongozi wa bunge umekwisha pewa maelekezo yote na serikali juu ya ununuzi wa magari hayo, hivyo akamtaka mwandishi akawaulize wao ( uongozi wa bunge)

Katika kukusanya fedha za kuwezesha kutekeleza mipango ya Serikali na ahadi alizotoa wakati wa kampeni, Rais John Maguguli alitangaza hatua mbalimbali za kudhibiti matumizi, na akawaeleza wabunge mwishoni mwa wiki kuwa hataweza kufanikiwa iwapo hatapata ushirikiano wao.

Katika kuonyesha kuwa anatoa kauli thabiti, Dk Magufuli aliagiza fedha ambazo zilichangwa na taasisi mbalimbali za fedha kwa ajili ya hafla za kuwapongeza wabunge, zielekezwe kwenye ununuzi wa vifaa tiba kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Tayari Rais ameshafuta safari za nje isipokuwa kwa kibali cha Ikulu baada ya mtu anayetaka kusafiri kutimiza masharti kadhaa, likiwamo linalomtaka aeleze faida ya safari yake na kama iwapo hatasafiri, nchi itaathirika vipi.
0 Toa maoni yako.

Ziara ya Papa Francis Kenya

Serikali ya Kenya imethibitisha kukamilika kwa maandalizi ya kumpokea kiongozi wa kanisa katoliki papa Francis.

Imebaki siku tatu tu kwa kiongozi huyo wa kanisa kuwasili nchini Kenya, huku viongozi wa kanisa la katoliki nchini humo pia wakithibitisha hilo.

Hii ni ziara ya kwanza ya Papa Francis barani Afrika, ambapo mbali na Kenya, pia ataitembelea Uganda na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
0 Toa maoni yako.
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company