Wanamgambo wa kundi la kigaidi la Al Shabaab nchini Somalia
Ripoti ya kimataifa ya kila mwaka ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani kuhusiana na ugaidi ilitolewa siku ya Jumatano iliyopita, bila ya kuelezea nafasi ya Washington katika kuyaanzisha makundi ya kigaidi katika pembe mbalimbali za dunia. Ripoti hiyo imeeleza kuwa, licha ya kutopungua vitendo vya kigaidi ulimwenguni, vitendo hivyo hatarishi vimeongezeka kwa asilimia 40 kati ya mwaka 2012 hadi 2013. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa kwenye ripoti ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani, katika mwaka 2013 yalitokea mashambulio 9,700 ya kigaidi duniani kote na kusababisha watu wasiopungua elfu kumi na nane kuuawa, elfu thelathini na mbili na mia tano kujeruhiwa na wengine wasiopungua elfu tatu kukamatwa mateka. Watayarishaji wa ripoti hiyo waliendelea kukariri madai yao yasiyo na msingi kwamba, baadhi ya nchi ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni waungaji mkono wakubwa kwa baadhi ya makundi ya kigaidi. Kwa utaratibu huo, tunaona kuwa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani imeamua kuzitupia mzigo wa matendo ya kigaidi serikali zilizoko mstari wa mbele katika kuikosoa serikali ya Marekani, huku serikali ya Washington ikijinadi kuwa ni bingwa wa mapambano dhidi ya ugaidi kwa kukabiliana na kundi la al Qaeda. Amma kile ambacho hakikuzungumzwa kwenye ripoti hiyo ni nafasi ya Marekani katika kuyaanzisha makundi ya wanamgambo wenye misimamo ya kufurutu ada katika nchi mbalimbali duniani. Wanamgambo ambao Marekani leo hii inawataja kuwa ni magaidi, wamekuwa wapiganaji kwenye vita kwa niaba ya nchi hiyo, kwenye vita vinavyopiganwa maeneo mbalimbali ulimwenguni. Marekani imekuwa ikiyatumia makundi hayo ya wanamgambo katika matukio mengi yanayojiri katika pembe za dunia kwa kuyapa suhula, silaha na miongozo pale inapoona imeshindwa kukabiliana ana kwa ana na mahasimu wake wakuu kwenye maeneo mbalimbali duniani. Ushahidi wa wazi kuhusiana na uhakika huo ni pale Marekani ilipoamua kuanzisha makundi ya Jihadi nchini Afghanistan kwa shabaha ya kukabiliana na hasimu wake katika vita baridi yaani Umoja wa Kisovieti wa Urusi ya zamani. Kwa mujibu wa mkakati uliopangwa na Mshauri wa zamani wa Usalama wa Taifa wa Marekani, Shirika la Ujasusi la Marekani CIA lilifanya propaganda kubwa kwa nchi za Kiarabu za kuwapeleka wapiganaji wa Kiarabu nchini Afghanistan kwa lengo la kupambana na majeshi ya Urusi ya zamani ambayo wakati huo yalikuwa yameivamia Afghanistan. Katika hatua nyingine, Marekani iliyapatia makundi hayo silaha za kisasa bila ya malipo yoyote. Matokeo yake makundi hayohayo ya Jihadi yalijipanga upya na kuunda kundi la Taleban na kujitokeza kuwa dhidi ya Waafghani wenyewe na baadhi ya nchi nyinginezo. Nchini Iraq nako pia, mara baada ya uingiliaji wa kijeshi wa Marekani na kuangushwa utawala wa kidikteta nchini humo na kukosekana serikali kuu kwa muda mrefu, kuliandaa mazingira ya kuibuka makundi kadhaa ya kikoo na hatimaye makundi hayo yaligeuka na kuunda mtandao wa al Qaeda. Makundi hayo ya kigaidi yamesababisha nchi hiyo kukosa amani na utulivu kwa muda wa miaka kadhaa sasa. Wafadhili wa kifedha na kisiasa wa makundi hayo, ni washirika wa karibu wa Marekani katika eneo la Ghuba ya Uajemi. Nchini Libya, Marekani iliyaandaa makundi ya wanamgambo ambayo yalikuwa hayana utambulisho wowote kwa kuyapatia silaha na kuanzisha machafuko yaliyopeleka kuangushwa utawala wa Muammar Gaddafi; ingawa wanamgambo hao hao wakawa ndiyo chanzo kikuu cha ukosefu wa amani kwa wananchi na utawala ulioingia madarakani. Syria ni mfano mwingine wa siasa za kigaidi za Marekani katika nchi hiyo ya Kiarabu. Nchini Syria, Washington ilikumbana tena na uzoefu mchungu na uliofeli wa kuyapatia silaha makundi ya kigaidi. Marekani ilianza kuwakusanya watu wenye fikra za kijihadi kutoka pembe mbalimbali za dunia na kuwapeleka huko Syria. Washington ilishindwa kuyadhibiti makundi hayo na matokeo yake yakabadilika kuwa sehemu ya jeshi la al Qaeda. Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani, hata Ayman al Dhwawahir ambaye anasemekana kuwa ni kinara wa al Qaeda hana nguvu na ushawishi kwenye makundi hayo. Kutokana na tadbiri na uendeshaji mbovu wa Marekani, kumejitokeza vijikundi vya wanamgambo katika maeneo mbalimbali duniani, vikundi ambavyo hakuna nchi yoyote inayoweza kuvidhibiti; na kwa kuzingatia hali hiyo iliyopo, hakuna matumaini yoyote ya kudhibitiwa makundi hayo ya wanamgambo magaidi katika siku za usoni.
CHANZO http://kiswahili.irib.ir/