Wanamgambo waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameishambulia kambi ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa MONUSCO nchini humo. Kiongozi mmoja wa jeshi la taifa la Afrika Kusini 'SANDF' amesema kuwa, wanajeshi watatu wa nchi hiyo wamejeruhiwa kwenye shambulio hilo lililofanyika mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kiongozi huyo amesema kuwa, wanajeshi hao wamehamishiwa hospitalini katika mji wa Goma kwa minajili ya kupata matibabu. Wakati huohuo, wanajeshi sita wa jeshi la Kongo wameuawa baada ya kujiri mapigano kati ya majeshi ya serikali ya Kinshasa na wanamgambo waasi wa kundi la APCLS katika eneo la Nyiabondo lililoko katika jimbo la Kivu Kaskazini. Inafaa kuashiria hapa kuwa, mapigano nchini Kongo yamesababisha karibu watu milioni mbili na nusu kuyahama makazi yao na wengine wasiopungua laki tano kukimbilia nchi za Rwanda na Uganda, kutokana na kushadidi mapigano nchini humo.