Umoja wa Mataifa umetaka kupelekwa askari zaidi na helikopta zinazohitajika kwa ajili ya kikosi chake nchini Mali ili kurejeshwa amani nchini huko na kuwalinda raia dhidi ya waasi.
Mwakilishi wa UN nchini Mali Bert Koenders ameliambia Baraza la Usalama kwamba wanakabiliwa na changamoto kadhaa ambapo jeshi la MINUSMA halina suhula muhimu kama helikopta kwa ajili kutekeleza majukumu yake.
Mpango wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali ulianza operesheni zake nchini humo Julai Mosi na Baraza la Usalama liliamua jeshi hilo liwe na askari 12,600. Hadi hivi sasa kuna askari 5,200 katika kikosi hicho. Mgogoro nchini Mali ulishadidi baada ya Ufaransa kuvamia nchi hiyo kijeshi kwa kisingizio cha kupambana na waasi wa kaskazini.