MWANASHERIA Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amesema kuwa watu wanaosema kwamba maamuzi ya Kamati Kuu ya chama hicho kuwavua nafasi za uongozi makada wake watatu limesababishwa na chuki binafsi, wanapaswa kufikiria mara mbili.
Amesema kuwa kueneza hoja hiyo dhidi ya maamuzi yalifoyanyika kwa kufuata misingi ya katiba ya chama hicho, wanatafuta huruma zisizo na sababu na kuendeleza ulaghai, huku akisisitiza kuwa chama hicho hakitaacha kusimamia taratibu zake, ikiwemo kuadhibu, kuonya na kusamehe wanachama na viongozi wanaokwenda kinyume.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara jana mchana katika kijiji cha Shelui, wilayani Iramba, mkoa wa Singida, Lisu alisema kuwa kila chama cha siasa kama ilivyo kwa taasisi yoyote ile kina katiba, kanuni, taratibu na makatazo yake, hivyo haiwezi kukubalika ndani ya chama hicho watu kuunda mitandao ya siri kwa madhumuni ya kutukana viongozi na kuvuruga chama.
“Hakuna suala la chuki binafsi katika suala hili linalowahusu hawa mabwana. Chama chenu cha CHADEMA kimechukua maamuzi magumu, sahihi na muhimu.
“Kimewavua nafasi za uongozi ndani ya chama Zitto Kabwe, Dk. Kitila Mkumbo (ambaye ni mtoto wenu nami ni mdogo wangu) na aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
“Kama kuna watu wanaanza kusema kuna chuki binafsi, wanapaswa kufikiria mara mbili. “Mdogo wangu Dk. Kitila, kijana wenu watu wa Iramba, alibambikiwa kesi na CCM kwa kisingizo cha kumkashifu au kumtukana mbunge wenu. “Tumeingia kumtetea kwenye ile kesi hatukuwahi kumwomba hata shilingi moja.
“Mdogo wangu Zitto…mwaka 2007 alipofukuzwa bungeni na hawa hawa ambao leo wanamshangilia na wakati ule walimtukana, wakimkebehi na kumpatia kila aina ya bezo, ni mimi na huyu baba hapa…Dk. Slaa…tulimsindikiza kwenda jimboni na nyumbani kwao Mwandiga Kigoma, kuwaambia wananchi wake kuwa alichofanya mbunge wao bungeni ni sahihi…mimi na Dk. Slaa.
“Mwaka 2009 huyu baba hapa…Dk. Slaa na mdogo wangu Zitto Kabwe waliposema mambo ya kweli bungeni kwa kutoa hoja bungeni juu ya ufisadi wa mabilioni ya NSSF, bilioni 87…fedha za wafanyakazi wa nchi hii zilizotumika kununua nyumba chakavu za Yusuf Manji, mfanyabiashara huyo aliwashtaki tofautitofauti kila mtu na kesi yake.
“Tuliingia kuwatetea…tulimtetea Dk. Slaa…tulimtetea Zitto…kwa sababu walikuwa wametoa hoja ya ukweli bungeni.
“Hatukuuliza shilingi hata moja. Tukaingia kwenye kesi hiyo, kesi zote zikasambaratika. Hakuna chuki binafsi katika suala la kina Zitto, Kitila na Mwigamba kuvuliwa nafasi zao,” alisema Lisu.
Aliongeza kusema kuwa makada hao walikuwa wameunda mtandao wa siri ndani ya chama hicho, wakiwachafua kwa kashfa za kutunga viongozi wakuu wa chama walioko madarakani sasa.
Lissu ambye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki alisema kuwa tangu amekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA hakuwahi kuwasikia Zitto na Dk. Mkumbo wakihoji au kupinga hoja yoyote ile kwenye vikao halali ikiwemo inayohusu taarifa ya fedha, bali siku zote walikuwa wakikubaliana na wajumbe walio wengi.
“Ndugu zangu kama tunataka kujenga chama cha siasa imara hatuwezi kuwa chama kinachoruhusu makundi ya siri siri na kimtandao kama ilivyo kwa CCM.
“Vikundi hivi vinafikiri namna ya kupata uongozi ni kuchafua na kutukana au kupindua uongozi halali uliopo-hadharani wanakishangilia chama hiki, lakini sirini wanakiponda.
“Vikundi hivi ni vya watu ambao vinafikiri kwamba ili mimi niwe mwenyekiti ni lazima mwenyekiti aliyepo nimchafue. Mwenyekiti achafuke ili mimi niingie…hata CCM haifanyi hivyo, mbunge wenu angefanya hivyo kwa Kikwete angebaki salama kwenye chama chao?” aliuliza Lisu huku wananchi wakiitikia: “Hapana habaki…!”
Akisistiza hotuba yake katika mkutano wa pili eneo la Kyengege, Lisu alisema kuwa chama hicho siku zote kimesisitiza umuhimu wa viongozi kuwa mfano katika suala la nidhamu na uadilifu, ili wanachama waweze kufuata nyayo hizo na kujenga taasisi imara.
Alisema kuwa haikuwa kazi rahisi kufanya maamuzi hayo, ndiyo maana Kamati Kuu ya chama hicho ililazimika kukaa siku mbili mfululizo, usiku na mchana, akisema kama CHADEMA inataka kuaminiwa na watu, lazima isimamie na kufuata mila na desturi ya siasa za vyama.
“Tunataka viongozi wenye nidhamu ili tuwe na wanachama wenye nidhamu. Tusipofanya hivi viongozi hawatakuwa na nidhamu, hivyo wananchi watakosa imani na chama kinakufa.
“Demokrasia si utovu wa nidhamu hata siku moja. Tutafanya tena na tena na tena kama ikibidi. Ikibidi tutakanya, tutaadhibu na kusamehe, ili mradi hatumunei wala kumpendelea mtu yeyote,” alisema Lisu.
Mwanasheria huyo pia alitumia fursa ya jana ambayo ilikuwa mara ya kwanza kuhutubia jimboni humo, akiwa ameshafika majimbo mengine yote ya mkoa wa Singida, kuwaambia wananchi wa jimbo hilo namna ambavyo wilaya ya Iramba inavyopangiwa mafungu ya bajeti lakini hayatumiki ipasavyo, hali inayosababisha wakazi hao kukosa huduma za msingi kama elimu, afya na maji.
Slaa: Huu ni mpango wa Mungu
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa amesema kuwa matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu yaliyofanyika wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili yana mkono wa Mwenyezi Mungu ambaye ameamua kuipofusha serikali ya CCM kufanya matendo ya kihalifu dhidi ya wananchi wake.
Akihitimisha ziara yake ya siku 22, katika majimbo 17 katika mikoa ya Shinyanga, Kigoma, Tabora na jana akamalizia Singida, Dk. Slaa amesema kuwa sasa Watanzania hawana haja ya kuambiwa zaidi juu ya uovu wa chama kilichoko madarakani kutokana na unyama mkubwa wanaotendewa raia akidai mwingine ni zaidi ya uliofanyika wakati wa Afrika Kusini ya Makaburu.
“Yaliyofanyika kwenye operesheni hiyo kama ambavyo Lisu ameeleza hapa, mwanamke amekamatwa na kupigiliwa msumari wa nchi sita sikioni kisha wakasema amekufa kwa presha…wengine wamebakwa na kuwekewa chupa sehemu za siri. Jamani unyama uliofanyika ni mkubwa mno!
“Watu wanaosoma vitabu vya dini, Korani na Biblia, wanajua kuna wakati Mungu huwa anaamua kuachia mambo fulani yatokee ili kuwapatia watu wake somo.
“Operesheni hii ambayo kwa kweli ilikuwa ni tokomeza wananchi, imeiweka CCM na serikali yake peupe, kila mtu anajua uovu wao sasa,” alisema Dk. Slaa alipokuwa akizungumza na wananchi maeneo ya Shelui na Kyengege, wilayani Iramba Singida.
#USOPEN_VIGOGO CHALI
-
SIKU Safi kwa Muaustralia Nick Kyrgios baada ya ushindi dhidi Johnson na
kutinga raundi ya Pili.
- Rafael Nadal akimchapa Millman Seti Tatu zote mfululi...
5 years ago