SOMA HII TAHARIRI YA GAZEETI LA TANZANIA DAIMA KUHUSU TTANESCO.

WAKATI maeneo ya Manispaa ya Kindondoni Dar es Salaam yakikabiliwa na migogoro ya ardhi, baadhi ya watendaji wa manispaa hiyo hawako tayari kuepusha migogoro hiyo.

Hali hiyo inatokana na hivi karibuni Kampuni ya Trans Auto Express Ltd, kuliboresha eneo la barabara kuwa la biashara ya maegesho ya magari kinyume na taratibu za mipango miji.

Eneo hilo lililoko Tindiga Mtaa wa Mikocheni ‘A’, kiwanja namba 269, 270, 271 na 272, linadaiwa ni sehemu ya barabara inayoanzia nyuma ya Shule ya Awali ya Feza kupitia nyumbani kwa Rais Ally Hassan Mwinyi na kutokezea Kawe.

Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni ya Machi 8 mwaka huu na kusainiwa na mhandisi wa Manispaa hiyo, Uriyo G. A, imeonyesha mwekezaji huyo ameruhusiwa kuboresha eneo lililo nyuma ya kiwanja namba 270, kama eneo la wazi.

Kwa mujibu wa barua hiyo eneo hilo ni la wazi, hivyo linabaki kuwa mali ya manispaa na kwamba litakapohitajika kwa matumizi ya umma, litatakiwa kuachiwa bila ya pingamizi.

Barua hiyo inafafanua kuwa gharama za kuboresha eneo hilo kwa mujibu ramani iliyowasilishwa na mwekezaji huyo zitakuwa juu yake na haruhusiwi kujenga ‘structure’ yoyote ndani ya eneo hilo la wazi.

“Kabla ya kazi kuanza na wakati kazi ikiendelea mwekezaji anatakiwa kuwasiliana na Ofisi ya Mhandisi wa Manispaa kwa ukaguzi na ushauri,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, mwekezaji huyo, amejenga ukuta ambao umeziba barabara hiyo kuanzia upande wa kutokea shule hiyo kiwanja namba 269 na upande wa pili wa kuelekea kwa kiwanja namba 272 kinyume na maombi yake ya kuboresha eneo la wazi lililo nyuma ya kiwanja namba 270.

Barua ya maombi iliyosainiwa na Ephraem Mrema kwa niaba ya Trans Auto Express Ltd, inaonyesha kwamba kampuni hiyo ni ya wazalendo na inamiliki kiwanja namba 270 Keko Avenue, Mikocheni ambapo hapo awali waliipangisha nyumba hiyo kwa Shirika la Kimataifa la Misaada Oxfam na baadaye Taasisi ya Moyo (Tanzania Heart Institute).

Inaeleza kwamba nyuma ya eneo hilo upande wa mashariki kuna eneo la Tindiga ambalo kwa muda wote limetelekezwa si tu na walio na viwanja vinavyopakana na eneo hilo bali pia na Manispaa ya Kinondoni.

Barua inaonesha kuwa Kampuni ya Trans Auto Express Ltd, imeiomba manispaa kibali cha kuliboresha eneo hilo la wazi kwa kulisafisha, kuchimba na kutupilia mbali udongo wa juu kwa kina cha mita moja, kuweka mawe na tabaka gumu, kusindika na kuweka ‘paving blocks’ pamoja na mifereji ili kutoa maji na kuyapeleka kwenye mkondo wake wa asili.

Eneo linaloombwa lina ukubwa wa takribani mita za mraba 2,300, wamekadiria kuwa litawagharimu sh milioni 200 kwa kazi za awali na sh milioni 12 kila mwaka kwa ajili ya kulitunza.

Vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya ofisi za pande hizo mbili, vikidai kwamba kuna makubaliano mengine ya malipo ya kila mwezi kwa mwekezaji kuilipa manispaa sh 1,960,000 kama kodi ambayo haijabainishwa katika barua ya manispaa kumjulisha mwekezaji.

Baadhi ya majirani wa eneo hilo nao wanahoji inakuwaje mwekezaji atumie zaidi ya sh milioni 200 kwa ajili ya kuliboresha eneo hilo tu na sh milioni 12 kila mwaka kulitunza na sh 1, 960,000 kila mwezi kama kodi.

Majirani hao wanahoji, inakuwaje manispaa iruhusu kampuni moja kulipatia eneo hilo kwa ajili ya kuliboresha, wakati kama ingetoa ruhusa ya kila mwenye nyumba afanye maboresho ingewezekana na wangeweza kuilipa manispaa sh 100,000 kwa kila nyumba kwa mwezi na wangeweza kukusanya sh 400,000 kwa mwezi, tofauti na mwekezaji huyo anayelipa sh 163,000 kwa mwezi.

Wapo pia wanaodai kuwa hakuna makubaliano ya mkataba ulioingiwa kati ya Manispaa ya Kinondoni na Kampuni ya Trans Auto Express Ltd, juu ya masharti waliyopeana, na wala hakuna majibu ya barua ya Machi 8, 2013 ya kukubali masharti waliyokubaliana.

Inadaiwa kuwa mradi huo unawashirikisha mmoja wa kigogo wa cheo cha juu wa Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) na mwingine wa ngazi ya juu wa serikali jambo linalosababisha manispaa kukubali kwa urahisi kulitoa eneo hilo la barabara na kuligeuza eneo la wazi.

Kampuni hiyo inahusika na kupakua na kupakia mizigo inayoingia na kutoka nje ya nchi (clearing na forwarding).

Uchunguzi umebaini kuwa eneo hilo linataka kugeuzwa kuwa sehemu ya kuhifadhia makontena na magari madogo yatakayoingizwa nchini na ya nchi za jirani yanayotolewa bandarini.

Ephraem Mrema alipoulizwa kuhusu barua hiyo ya maombi kwa niaba ya Kampuni ya Trans Auto Express Ltd, anasema hahusiki na kitu chochote, kwa maelezo zaidi atafutwe Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni.

“Mimi sihusiki na kitu chochote nimeshamaliza na watu wa manispaa na wala mimi si Mkurugenzi wa Kampuni hiyo ni mwajiriwa tu kama anavyoajiliwa mtu yeyote yule,” anasema Mrema.

Akizungumizia suala hilo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mussa Natty, anasema ni vema viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Mikocheni, kusimamia sheria za ujenzi katika maeneo hayo ili kuepuka migogoro kati ya wananchi na serikali.

Natty anasema watendaji hao hawapaswi kukaa kimya pindi wanapobaini mwekezaji anajenga maeneo ya wazi au barabarani kwa matumizi yake binafsi, kwa kuwa sheria zipo wazi na kila mmoja anapaswa kuzitii bila shuruti.

Anasema iwapo kuna yeyote amejenga katika eneo la wazi na kusababisha adha kwa wengine, ni muhimu watendaji wakachukua hatua kutokana na mwekezaji huyo kuvunja sheria.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company