Mauaji ya kinyama tena,OLISI WA HUSIKA


NA TANZANIA DAIMA.
WAKATI kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Mwanza, Clement Mabina akiua naye kuuawa na wananchi kutokana na mgogoro wa ardhi, watu wengine watatu wameuawa na polisi jana, huku kituo cha polisi, baiskeli na gari vikichomwa moto katika mgogoro unaohusishwa na masuala ya ardhi katika Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro.

Akizungumza na Tanzania Daima juu ya tukio hilo, Diwani wa Malinyi, Said Tira, alisema kilichosababisha mauaji hayo ya jana kilianza wiki moja nyuma, baada ya wafugaji kumuua mwananchi anayedaiwa kutoa taarifa polisi juu ya kuwapo kwa mifugo katika eneo lisiloruhusiwa.

Alisema baada ya wafugaji wanaodaiwa kuwa watatu kumuua mwananchi huyo, wananchi nao walijikusanya na kwenda kuchoma moto nyumba za wafugaji hali iliyosababisha askari kuwakamata.

Aliongeza kuwa katika hali hiyo wananchi walitaka kujua sababu za wafugaji walioua kuachiwa, huku wananchi waliochoma nyumba za wafugaji wakiendelea kukamatwa na kuwekwa rumande.

“Ni kweli hapa nipo katika eneo la tukio na nimewashuhudia wananchi watatu wakiwa wamefariki, mmoja amepigwa risasi ya kichwani mwingine kifuani na mwingine begani,” alisema Tira.

Alisema wakati wananchi walipokusanyika kutaka kujua sababu za wakulima kukamatwa na wafugaji kuachiwa, askari wa kituo cha Malinyi walianza kurusha risasi hewani na kisha kuelekeza kwa wananchi na kwamba risasi zilipowaishia ndipo wananchi wakavamia kituo na kuchoma baadhi ya mali zilizokuwepo kituoni na kuwatoa watuhumiwa waliokamatwa.

Alitaja baadhi ya vitu vilivyochomwa kuwa ni ofisi iliyo katika kituo cha polisi Malinyi, pikipiki, baiskeli pamoja na gari.

Polisi washindwa kutunza siri

Taarifa nyingine kutoka Malinyi zinaeleza kuwa baadhi ya polisi ndio chanzo cha tatizo hilo kutokana na kushindwa kutunza taarifa za siri walizopewa na wakulima juu ya kuwapo mifugo iliyofichwa katika baadhi ya maeneo.

Mtoa taarifa alieleza kuwa baada ya polisi wa Malinyi kupewa taarifa hizo walikutana na wafugaji na kuwataja watu waliotoa taarifa za siri ambapo wafugaji hao waliamua kuwavamia na kusababisha kifo cha mwananchi mmoja kabla ya tukio la jana.

“Kuna mwananchi alitoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuwa licha ya zoezi hili la kuondoa mifugo kuonekana limekamilika, lakini bado kuna wafugaji wamehodhi mifugo mingi katika eneo lao. Jamaa wa usalama wakarejesha habari kwa wafugaji,” kilisema chanzo kingine kutoka Malinyi.

Alisema baada ya mauaji ya awali na wananchi kuamua kuchoma nyumba za wafugaji, Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Francis Miti alienda Malinyi Igawa na kuongea na wafugaji kwa faragha kisha akawafuata wakazi wa Malinyi na kukemea hulka za kujichukulia sheria mikononi.

“Alipokuja DC akasema kwa kuwa kila upande umejichukulia sheria mkononi anaomba hali hiyo iishe na isijirudie, lakini jana akaleta askari na kuwakamata wananchi wanaohisiwa kumchoma moto mfugaji, hili jambo liliwaudhi wananchi,” aliongeza mkazi mwingine wa Malinyi.

Mkuu wa Wilaya ya Ulanga alipoulizwa juu ya tukio hilo, alikataa kuzungumza na kusema jambo lolote aulizwe Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro.

Hata alipoulizwa juu ya kuwapendelea wakulima katika suala hilo, Miti aliendelea kushikilia msimamo wake na kusema kama kuongea ataongea leo.

Kamanda wa Polisai Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile hakuweza kuzungumzia hali ya Malinyi baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kupokewa kwa muda mrefu.

Polisi Makao Makuu yatoa ufafanuzi

Jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Jeshi la Polisi, SSP Advera Senso, alisema chanzo cha mauaji hayo ni wananchi kukataa kutii amri halali ya polisi na kutaka kuvamia kituo kwa ajili ya kuwatoa watuhumiwa waliokamatwa kwa tuhuma za mauaji.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Senso alisema tukio hilo lilitokea jana saa 3:00 asubuhi baada ya kundi la watu kutoka maeneo mbalimbali ya Malinyi kuvamia kituo cha polisi.

Senso alisema kutokana na tukio hilo, IGP Said Mwema ametuma timu maalumu inayoongozwa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja kwa ajili ya kuongeza nguvu katika msako wa kuwakamata watu waliohusika na tukio hilo.

“Tukio hilo linaashiria vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani na limesababisha vifo, majeruhi na kujenga hofu miongoni mwa jamii, na sisi hatuwezi kuvumilia hali hii. Tutawakabili wote waliohusika na kuwafikisha katika mkono wa sheria,” alisema Senso.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company