Ajali nyingine yaua 13,Wengine wamejeruhiwa.


NA TANZANIA DAIMA
WATU 13 wamefariki dunia papo hapo na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka Itigi kwenda mkoani Singida kupata ajali katika Kijiji cha Isuna, Wilaya ya Ikungi, mkoani hapa.
Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Geofrey Kamwela, alisema kuwa ajali hiyo imetokea eneo la Singida Kusini, mkoani humo.

Kamanda Kamwela alisema kuwa ajali hiyo ilihusisha gari namba T 730 BUX Noah, ambalo liligongana uso kwa uso na lori T 687 AXD Scania, lililobeba samaki likitokea jijini Mwanza.

Kamanda Kamwela alisema kuwa ajali hiyo imetokea saa 1:32 asubuhi kwenye barabara kuu ya Singida-Dodoma, ambapo kati ya maiti 13, watatu ni wa familia moja waliokuwa katika gari dogo aina ya Noah.

Alisema kati ya maiti hizo wawili ni wanawake na wanaume ni 11, huku abiria wengine watatu wakinusurika na kupata majeraha madogo madogo, ambapo wamekimbizwa katika hospitali ya mkoa huo.

Kamanda Kamwela alisema kuwa miili ya abiria 10 imetambuliwa na ndugu zao huku miili ya abiria watatu bado haijatambuliwa.

Aliwataja waliotambuliwa ni watu wa familia moja, Omari Shabani (44), mkewe Salma Omari na mtoto wao, Nyamumwi Omari (10), wote wakazi wa mji mdogo wa Itigi.

Wengine ni Haji Mohammed (29) (Msisi), Mtunku Rashidi (68) (Sajaranda), Salehe Hamisi (28) (Sajaranda), Samiri Shabani (20) (Puma), Mwaleki Nkuwi (35) (Ikungi), Athumani Kalemba (38) na Ramadhani Mkenga (Sajaranda).

Kamanda huyo alisema kuwa lori hilo lilipopishana na Noah lilihama kutoka upande wake na kuifuata Noah ambayo ilikuwa upande wake wa kushoto, hivyo kuligonga na kisha kuliburuza umbali wa zaidi ya mita 15.

“Bado hatujajua chanzo cha ajali hiyo mbaya, ingawa baadhi ya watu wanadai huenda dereva wa lori alisinzia, hivyo kusababisha lori hilo kuhama upande wake na kuifuata Noah na kwamba uchunguzi utakapokamilika tutatoa taarifa hiyo,” alisema.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya mkoa huo, Dk. Deogratius Banuba, alikiri kupokea miili ya abiria hao 13 na kwamba kati yao miwili ni ya watoto.

Ajali hii imetokea ikiwa ni zaidi ya wiki moja tangu watu wenye hasira mkoani humo walichome moto basi la Kampuni ya Mtei Express, baada ya kugonga pikipiki iliyobeba watoto watatu wa familia moja na baba yao.

Katika tukio hilo, watoto watatu waliokuwa katika pikipiki hiyo walifariki dunia, huku abiria waliokuwa kwenye basi hilo hakuna aliyeumia wala kupoteza. maisha

Waliokufa katika ajali hiyo ni watoto Stamili Shabani (23) na Kassimu Shabani (19), ambao walikufa papo hapo, wakati Hamza Shabani (15), alifia katika hospitali ya mkoa wakati madaktari wakiendelea kuokoa maisha yake.

Huku baba mzazi wa watoto hao, Shabani Bunku (45), alidaiwa kuvunjika mguu na mkono wa kulia pamoja na kupata jeraha kubwa kichwani.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, SACP Geofrey Kamwela, alisema wanafamilia hao walikuwa wakienda shamba kwa ajili ya palizi, ambapo basi lililohusika na ajali hiyo ni aina ya Scania, namba T 742 ACU.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company