Ndugu zangu,
Si wengi wenye kufahamu, kuwa Yoweri Museveni alianza masomo yake ya Chuo Kikuu, Dar es Salaam, mwaka 1967. Kijana Museveni alitoka Uganda kuja Dar es Salaam kwa garimoshi ikiwa ni safari yake ya kwanza nje ya Uganda.
Kwenye kitabu chake, ' Sowing The Mustard Seed', Museveni anasimulia, kuwa pale Railway Station , Dar es Salaam, alipokewa na Mganda mwenzake Martin Mwesigwa aliyemwonyesha njia ya kufika Ubungo na Chuo Kikuu.
Uhanarakati wa Museveni ulianza kujitokeza hapo Mlimani. Akiwa hapo, Museveni na baadhi ya wanafunzi wenzake walianzisha jumuiya ya USARF- University Student's African Revolutionary Front. Uanachama wake ulikuwa ni wa PanAfricanism. Kulikuwamo na wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali. Alikuwamo pia marehemu Andrew Shija.
Museveni akiwa Mlimani, alipangiwa kuishi hall lililoitwa ' Biafra'. Maana, lilijitenga kidogo na mengine. Na wakati huo ndio kulikuwa na vuguvugu la Biafra kujitenga kutoka Serikali ya Shirikisho, Nigeria, na Julius Nyerere, alianza kwa kuitambua Biafra kabla ya kubadili mtazamo baadae.
Pale Mlimani Museveni alisoma Political Science. Uhanarakati wa Museveni unathibitishwa pia na ndugu yangu BAP-' Born Again Pagan'. Hili si jina lake halisi. Huyu ni mmoja wa ' wanakijiji wa Mjengwablog' wa miaka mingi. Naye alisoma Chuo Kikuu enzi hizo. Anamkumbuka Yoweri Museveni aliyekuwa mbele yake mwaka mmoja. Kuwa alikuwa ni mtu mwenye msimamo, na kuwa , alikuwa akiingia kwenye lectures za wahadhiri aliowakubali tu kimisimamo.(P.T)
Kwenye ' Sowing The Mustard Seed', Museveni anaelezea jinsi jumuiya yao ya USARF, ambaye yeye ndiye alikuwa Rais wake, ilivyojipambanua kwenye masuala yenye kuhusiana na itikadi na mapambano ya ukombozi. Waliunda kikundi chao wenyewe cha kujisomea na kujadiliana. USARF ilikuwa na akina Eriya Katageya, James Waphakhabulo, Andrew Shija na hata John Garang, aliyekuja kuwa kiongozi wa SPLM ya Sudan.
Waliawaalika pia baadhi ya wahadhiri kujadiliana nao. Walter Rodney, alikuwa mmoja wa wahadhiri hao. Wakati huo, Walter Rodney, mwandishi wa kitabu cha ' How Europe Underdeveloped Africa' alikuwa kwenye harakati ya kukusanya materials za kitabu chake.
Kikundi cha USARF kilifikia hata kuwaalika wageni mbali mbali waliopita hapo chuoni kwa mijadala. Ikiwamo viongozi wa mataifa ya nje.
USARF ya Museveni na wenzake ilifika mahali wakawashambulia hata vijana wa TANU, tawi la Chuo Kikuu kwa kuacha harakati za kiuanafunzi na badala yake kujipendekeza kwa viongozi wa TANU mjini, ili waje wapewe vyeo baadae.
Jambo hilo lilifanya USARF na akina Museveni watengenezewe ' zengwe' ama fitina kutoka viongozi wa TANU- Youth League Mlimani kwenda kwa viongozi wa TANU Lumumba. Kosa la USARF? Kwamba wanaeneza kampeni dhidi ya sera za TANU.
Na TANU Youth League wakaenda mbali zaidi, wakawachongea USARF na akina Museveni kwa Julius Nyerere mwenyewe.
Kikatoka kivumbi. Nyerere akaamua ashuke mwenyewe Mlimani kukutana na hao wanaojiita USARF. Museveni akawapanga watu wake, na akawa tayari kuongoza mapambano. Nini kilitokea kwenye mpambano wa hoja kati ya Nyerere na Museveni pale Mlimani?
Tukutane kesho, panapo majaliwa.
Maggid,
Iringa.
#USOPEN_VIGOGO CHALI
-
SIKU Safi kwa Muaustralia Nick Kyrgios baada ya ushindi dhidi Johnson na
kutinga raundi ya Pili.
- Rafael Nadal akimchapa Millman Seti Tatu zote mfululi...
5 years ago