Daima mwanadamu yoyote hawezi kujihisi mkamilifu wakati mahusiano yake na wengine hayako vizuri. Kila mmoja ameumbiwa uhitaji wa ndani wa kuona anahusiana na wengine vema, ingawa wengi wetu inatushinda
na kila mara tunajikuta tukifukuza marafiki wanaotuzunguka kuliko uwezo
wetu wa kuwatafuta na kuwatunza marafiki wapya. Makala au mada hii itakusaidia kukupa uwezo na ujuzi wa kuweza kuhusiana kwa busara na kwa akili na wale wote wanaokuzunguka. Kati ya mambo mahimu utakayoweza kuyapata ni ni pamoja kujua jinsi ya kufanya mahusiano yenye afya na watu wote na pia kufahamu jinsi ya kujiweka kuwa rafiki wa kila mtu na kuchagua marafiki bora wenye manufaa.
1. Jifunze kuutengeneza na kuuendeleza mtazamo bora kwa wengine
Wakati
wowote na popote, unahitajika kuwa na mtazamo mruri kwa watu wengine.
Kuwa na uhusiano mzuri na wenye afya ni kule kuelewa ukweli kuhusu
binadamu na maisha wanayoyaishi, bila uelewa huu utakuwa na hila na hofu
katika maisha yote.
Nimejaribu
kuchagua badhi ya mambo halisi kuhusu maisha ya mwanadamu ambayo ni
muhimu ukiyajua ili ikusaidie kutokuwa mwenye hofu na hila, na
ikujengee mayo na upendo wa kuhusika na maisha ya wengine.
a) Fahamu kwamba wanadamu wote wana thamani sawa.
Uthamani
wa kila mmoja wetu unatokana na kwamba kila mmoja ameumbwa na Mungu.
Tena vitabu vitakatifu vinasisitiza kuwa tumeumbwa kwa mfano wa Mungu.
Pale unapofahamu kuwa kila unayemuona anathamani sawa na wewe kamwe
hutomdharau yeyote, na wala hutajiona usiye na thamani ukijilinganisha
na yeyote. Mtazamo huu wenye afya juu yako na kwa wengine unafaa sana
kwa mafanikio yako binafsi.
b) Matendo ya kila mmoja huathiri ujumla wa utu
Matendo
yangu au yako huweza kuathiri jamii ya binadamu wanaonizunguka.
Matendo yetu na matokeo yake huenea kama vile mawimbi yaeneavyo baharini
pale kitu kinapodondoshwa majini. Mfano unapofanya tendo fulani,
linaweza kuamshawishi vizuri au vibaya yule aliyeliona au kulisikia,
yule mtu pia atawaathiri wengine wengi. Tena utakapolijua hili,
utatambua kuwa, tendo lako au matendo yako haijalishi ni madogo au
makubwa kiasi gani, yanaweza kua muhimu kwa ulimwengu mzima. Katika
hili utajivunia kufanya lolote jema uwezalo kwa jamii inayokuzunguka.
Sasa hii itakuwezesha kujifahamu kuwa wewe sio mnyonge kuliko wengine,
wala wewe siyo wa juu zaidi kuliko wengine, lakini zaidi utafahamu kuwa
uko sawa na yeyote. Ufahamu huu pia ni muhimu kwa mafaniko yako
binafsi.
c) Fahamu kuwa watu ni rasilimali kwako
Hii
inamaanisha kuwa, haijalishi tunaimani kubwa kiasigani, lakini mafaniko
yetu hayapo wala hayatoki kokote isipokuwa kwa watu wanotuzunguka.
Pale utakapoangalia historia ya mafanikio yako utaona kuwa watu ndio
wamekuwa rasilimali yako muhimu kufikia hapo ulipo.
Ukifikiria
utoto wako, utaona jinsi ambavyo watu wengi hata wale wasio ndugu zako
walivyo husika katika kukulea. Fikiri vile watoto wakubwa zaidi yako
walivyokuwa wakikusaidia njiani ukienda shule na kurudi nyumbani, au
hata darasani. Fikiria kuhusu walimu wako, wa shule ya msingi au
sekondari ambao mara nyingine walikupa changamoto nyingi za maisha.
Vilevile
inaendelea hata katika mustakabali wako, kama unatamani kuwa daktari
wa binadamu, lazima utahitaji watu walio wagonjwa ili ufanikiwe katika
taaluma yako. Kama utataka kuwa mfanyabiashara, utahitaji watu kama
wateja ili ufanikiwe katika biashara yako, hivi hivi pia kwa chochote
utakachotamani kukifanya.
Pale
utakapolielewa hili utajifunza kumtakia mema kila mtu. Utatamani kila
mtu afanikiwe kwasababu unajua kuwa mafanikio yake yatawezesha kwa
nammna moja au nyingine kunyanyua mafanikio yako.
d) Kila mtu unayekutana nae anahitaji kutiwa moyo
Kila
mmoja anahitaji kutiwa moyo katika safari ya maisha. Ingawa siyo vyema
kulazimisha kutiwa moyo na wengine kama vile ni hitaji la lazima, sote
tunajisikia vema tunapotiwa moyo.
Habari
njema ni kwamba, sio jambo gumu kumtia mtu moyo. Hauhitaji kufanya
jambo kubwa kumtia mtu moyo bali ni vitu rahisi tu. Mfano kutoa salamu,
tabasamu, mazungumzo ya shukrani, kutoa ushuhuda fulani wa ushindi,
kumwimbia mtu au kumchagulia wimbo pamoja na vitu vingine vingi.
Pale
utakapojua kuwa kila unayekutana naye anahitaji kutiwa moyo sawasawa
na vile wewe unavyomhitaji yeye katika kukutia moyo, kamwe hautakuwa na
woga wala hofu kwa yeyote, zaidi utakuwa unafurahia kutoa msaada wowote
unaouweza.
Itaendelea Wiki Ijayo.............................