WIKI hii ilikuwa ya wabunge kuijadili bajeti kuu ya serikali iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha, William Mgimwa.
Lakiti tofauti na utaratibu wa miaka yote, bajeti ya kambi rasmi ya upinzani bungeni inayoongozwa na CHADEMA, haikuweza kusomwa bungeni kutokana na wabunge wote wa chama hicho kutokuwepo.
Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe aliyepaswa kusoma bajeti hiyo, naye aliongozana na wenzake mkoani Arusha kuomboleza vifo vya wafuasi wa chama chao waliolipuliwa na bomu wiki iliyopita.
Licha ya bajeti hiyo kutowasilishwa bungeni na kuingizwa kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge (hansard), CHADEMA waliona vyema waisambaze kwenye vyombo vya habari na mitandoo ya kijamii ili wananchi waone mawazo na mapendekezo yao mbadala.
Kwa kifupi CHADEMA imeainisha vyanzo vingi vipya vya mapato, vipaumbele na kufuta misamaha ya kodi zisizo na tija kwa taifa.
Zitto anasema kutokana na ongezeko kubwa la matumizi yasiyo ya lazima katika bajeti ya serikali, kambi rasmi ya upinzani imependekeza kupunguza asilimia 30 ya gharama za posho za vikao, semina, usafiri, viburudisho, mafuta na vilainishi.
Katika mchanganuo huo, Zitto alisema wanalenga kuondoa mikopo yenye masharti ya kibiashara ili kulipunguzia taifa mzigo wa madeni wakati bajeti ya serikali ni yenye mikopo ya sh trilioni 1.156 yenye masharti ya kibiashara.
“CHADEMA inajikita katika utekelezaji wa mpango wa maendeleo kwa kutenga zaidi ya asilimia 41 ya mapato ya ndani kugharimia miradi ya maendeleo, huku CCM inapingana na mpango wa maendeleo wa taifa kwa kutenga asilimia 22.4 kinyume na matakwa ya mpango wa serikali ambao unahitaji asilimia 35.
“Bajeti yetu imeanzisha kodi maalumu ya michezo na Wakala wa Maendeleo ya Michezo wakati ile ya Serikali ya CCM haijali michezo na wala sio kipaumbele chake,” alisema.
Zitto anaongeza kuwa CHADEMA inalenga kulipa pensheni kwa wazee wote kuanzia miaka 60 na kuendelea huku bajeti ya serikali haina mfumo wa pensheni kwa wazee.
Alisema kuwa wanapendekeza kushusha kiwango cha chini cha kodi ya mapato (PAYE) kutoka asilimia 14 hadi 9, lakini serikali katika bajeti yake imeshusha kodi hiyo kwa asilimia moja.
Zitto katika mchanganuo huo wa utofauti wa bajeti ya CHADEMA na ile ya serikali, anaongeza kuwa wanakusudia kuondoa matumizi yasiyo ya lazima kwa asilimia 30 wakati serikali ina matumizi yasiyokuwa ya lazima sh bilioni 214.
“Bajeti yetu inajitegemea kwa makusanyo ya mapato ya ndani ya asilimia 75.8, ile ya serikali ni tegemezi kwa asilimia 37.8 kutokana na kukopa kwa kiwango kikubwa.
“Sisi bajeti yetu ina punguzo la misamaha ya kodi na kufikia asilimia moja ya pato la taifa, serikali ina misamaha ya kodi kiasi cha asilimia 4.3 ya pato la taifa, sawa na sh trilioni 1.922,” alisema.
Kuhusu mfumuko wa bei, Zitto alionesha kuwa CHADEMA itakabiliana nao kwa bidhaa muhimu, kwamba bajeti ya serikali ya CCM hazingatii mfumuko wa bei.
Alisema kuwa wakati CHADEMA wakionesha maslahi bora kwa wafanyakazi kwa kuongeza kima cha chini cha mshahara kuanzia sh 315,000, serikali ina kima cha chini cha sh 170,000 kisichoendana na gharama za maisha kwa sasa.
Zitto alifafanua kuwa bajeti yao inafuta ongezeko la kodi kwenye mafuta ya dizeli na petroli, huku ile ya serikali inaongeza kodi kwenye mafuta; dizeli asilimia 6.1 na petroli asilimia 8.5.
“Tutaondoa ongezeko la kodi kwenye ngano na hivyo bidhaa za ngano kama mikate, maandazi, chapati kutopanda bei, wao serikali wameongeza bei ya ngano kwa asilimia 10 na hivyo kutowajali wananchi wa kipato cha chini wanaotumia bidhaa hizi kwa wingi.
“Tunasema CHADEMA inafuta ongezeko la kodi kwenye matumizi ya simu za mkononi, lakini Serikali ya CCM inaongeza kodi kwenye simu za mkononi na hivyo mtumiaji kutakiwa kulipa kodi/tozo/ushuru wa asilimia 36.5,” alisema.
Zitto alivitaja vyanzo vyao vya mapato kuwa ni kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, marekebisho ya kodi za misitu na kupunguza misamaha ya kodi.
Pia watatoza kodi ya asilimia 0.5 kwenye mauzo na ya asilimia moja ya manunuzi ya nje kwa ajili ya kujenga reli na kuzuia ukwepaji kodi unaofanywa na kampuni za kimataifa.