www.hakileo.blogspot.comWakati kukionekana kuwapo kwa mvutano mkali kati ya Jeshi la Polisi nchini na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), chama hicho kimesema kuwa hakitakubali kukaa kimya wakati baadhi ya watumishi wa jeshi hilo wakitumiwa vibaya kwa maslahi ya kisiasa kukandamiza raia.
Chama hicho kimesema hakina ugomvi na jeshi hilo kwa ujumla wake, isipokuwa askari wachache kiliodai wanatumiwa vibaya kuhujumu haki za binadamu na demokrasia nchini, kikisema hao ndiyo wanalipaka matope jeshi hilo na kuzidi kulikosesha imani kwa wananchi.
Akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara Tabora mjini, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema chama hicho hakitarudi nyuma kutetea haki na matumaini ya Watanzania.
Mkutano huo uliofanyika katika Uwanja wa Chipukizi, ukiwa ni sehemu ya kukamilisha kuzindua Kanda ya Magharibi (mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi), ikiwa ni mkakati wa chama hicho wa kujiendesha kwa kanda.
“Ndugu zangu watu wa Tabora, wanachama na wapenzi wetu wa Kanda ya Magharibi, katika mapambano haya ya kuing’oa CCM na kuleta mabadiliko makubwa ya mfumo na utawala ndani ya nchi yetu, tumefika mahali utetezi wa haki na matumaini ya wananchi umegeuzwa kuwa ni vurugu au fujo…kila leo mnasikia chama chenu ambacho kimezidi kuwa na ushawishi miongoni mwa Watanzania wengi wenye kiu kubwa ya mabadiliko, kinafanyiwa vituko, kimoja baada ya kingine,” alisema.
Alisema hivi sasa wafuasi na wapenzi wa chama hicho wanatekwa, wanateswa, kupigwa na hata kuuawa.
“Matukio ya namna hii yanazidi na sisi tumesema hatuwezi kuendelea kulalamika na kulialia kwa vyombo husika. Tutajilinda,” alisema.
“Tunatambua umuhimu wa vyombo vya ulinzi na usalama. Taifa linawahitaji wawe waadilifu, watimize wajibu na kutenda haki kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi. Chadema tunawatetea hawa ndani na nje ya Bunge, lakini hatutakubaliana na askari wanaotumika vibaya, kwa kupewa amri za hovyo, kama kwenye tukio la bomu Arusha,” alisema Mbowe.
Akizungumzia suala la mjadala wa rasimu ya Katiba Mpya, Mbowe alisema mapema mwezi Agosti, mwaka huu, chama hicho kitaanza kuzunguka nchi nzima kwenye operesheni M4C-Katiba Mpya; na kitaendesha mabaraza yake kwa uwazi kwenye mikutano ya hadhara.