CHAMA cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeutaka umoja wa vijana wa Vyama vya
Kidemokrasia Duniani (IYDU) kupiga kelele kote duniani ili kuwanusuru
Watanzania wanaouawa hovyo kwa sababu za tofauti za siasa hapa nchini.
Akizungumza
na uongozi wa umoja huo (IYDU) jijini Dar es Salaam wiki hii, Mnadhimu
Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni Tundu Lissu alisema ni wakati wa
vijana kuwaokoa wenzao wa Tanzania ambao kujiunga kwao na siasa
kumesababisha wachukiwe na watawala.
“Watu
wanauawa hadharani na hakuna hatua zinazochukuliwa…nendeni katika nchi
zenu katika mabunge yenu mkapige kelele katika haya yanayotokea
Tanzania; inaweza kusaidia na mkawa mmewasaidia Watanzania,” alisema
Lissu.
Tundu Lissu
alisema viongozi wengi wamekamatwa na kufunguliwa kesi nyingi
mahakamani, na hivyo kuifanya CHADEMA kuwa katika wakati mgumu kuliko
mwingine wowote katika uendeshaji wa siasa za vyama vingi hapa nchini.
Chama hicho
kimedai kuwa hali ya kisiasa hususan kwao na baadhi ya wapinzani nchini
ni ngumu, kutokana na ukandamizaji mkubwa unaofanywa na serikali kwa
kutumia vyombo vya dola.
Lissu
alisema viongozi wa upinzani wamefunguliwa kesi za ugaidi kwa lengo la
kuwafanya watumie muda mwingi katika kesi hizo, badala ya kuishughulikia
serikali pale inaposhindwa kutimiza wajibu wake.
Mbali na
kesi hizo, kumekuwa na matukio ya kikatili ya kuteka, kutesa na hata
mauaji dhidi ya watu wanaoshabikia upinzani na wale wanaoikosoa serikali
katika mambo ya msingi na yenye maslahi ya nchi.
Lissu
amesema wabunge wa CHADEMA licha ya uchache wao, wakiwemo baadhi wa
vyama vingine vya upinzani, wamejitahidi kupambana bila woga bungeni
kutetea wananchi lakini wamekuwa wakizidiwa na wingi wa wenzao wa CCM,
ambao wamekuwa wakipitisha maamuzi mengi ya hovyo na yasiyo na manufaa
kwa nchi.
Mapema
akiwaaga vijana hao, Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe, amewataka
vijana kutokata tamaa kutokana na mambo yanayotokea nchini.
Mbowe
alisema CHADEMA haitarudi nyuma katika harakati za kutwaa madaraka ya
dola hata kama watawala waliopo madarakani hawapendelei nafasi zao
kuwaponyoka.
“Tunafahamu
katika siasa kuna magumu mengi lakini niwahakikishieni kuwa ninyi mna
nafasi kubwa ya kuleta mageuzi sehemu yoyote kama mtakuwa na dhamira na
kuvishinda vitisho mbali mbali dhidi yenu,” alisema Mbowe.
Katika ziara
yao hapa nchini vijana hao wa IYDU walitembelea ofisi mbali mbali
ikiwamo Wizara ya Mambo ya Nje na ubalozi wa nchi za Ulaya nchini (EU).
Mkurugenzi
wa masuala ya Mashariki ya Mbali, Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Simba
Yahya, alikiri kuwa watumishi wa umma wanashindwa kutofautisha utendaji
wa serikali na chama kilichoko madarakani.
“Itachukua
muda kwa wafanyakazi kutenganisha hali hii….. kiuhalisi wanatakiwa wawe
watendaji kwani wapinzani wa leo wa serikali ndio wanaweza kuwa mabosi
wao wa kesho,” alisema Yahya.