hakileo
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ameshinda kiti cha urais wa taifa
hilo kwa muhula mwingine wa saba. Matokeo rasmi yanaonesha
kuwa Mugabe ameibuka na asilimia 61 za kura dhidi ya mpinzani
wake, Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai ambae amepata asilimia 34.
Tsvangirai amesema uchaguzi huo wa rais na wabunge uligubikwa
na vitendo vya udanganyifu na ametoa kauli ya wazi akisema
atachukua hatua za kisheria. Amesema chama chake cha MDC
hakitashirikiana tena na chama cha Mugabe, Zanu-PF. vyama hivyo
viwili vilifanya kazi pamoja katika serikali ya muungano iliyoundwa
2008. Kwa upande wao Umoja wa Ulaya umeonesha wasiwasi wake
kuhusu madai ya kufanyika mambo kinyume na utaratibu katika
uchaguzi huo. Mugabe mwenye umri wa miaka 89, amekuwa rais wa
Zimbabwe tangu taifa hilo lipate uhuru wake kutoka kwa Waingereza
1980.