Serikali inapoteza Sh700 bilioni kwa risiti za mkono




Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu (PAC), Zitto Kabwe.
Na Mwandishi Wetu, kwa isani ya Mwananchi

Dar es Salaam. Serikali hupoteza zaidi ya Sh700 bilioni kwa mwaka kutokana na utaratibu wa kukusanya mapato kwa kutumia stakabadhi zinazoandikwa kwa mkono.


Taarifa iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu (PAC), Zitto Kabwe imesema kwa sasa Serikali hukusanya Sh741 bilioni kwa mapato yasiyo ya kikodi ambayo ni nusu tu ya mapato ambayo Serikali ingestahili kupata.


Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), ameishauri Serikali itumie risiti za elektroniki kwa kukusanya maduhuli.


“Utaratibu wa kutumia risiti za elektroniki utaongeza maradufu mapato ya Serikali na kuifanya kuachana na mtindo wa kupandisha kodi kwenye bidhaa muhimu kwa wananchi.


“Uamuzi wa Kamati za Bunge za Hesabu wa kuitaka Serikali kukusanya maduhuli yake kwa kutumia risiti za elektroniki unapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania,” ilisema taarifa hiyo ya Zitto.


Alisema walipitia mpango wa Serikali na kugundua kuwa mapato yasiyo ya kikodi yamekadiriwa kuwa ni Sh741 bilioni kutoka wizara, idara na mikoa.


“Serikali inapata Sh383 bilioni kutoka kwenye halmashauri za wilaya, miji na manispaa. Hatukuweza kupata mapato ya mashirika ya umma maana hayaletwi kwenye Bajeti za Serikali,” alisema.


Wizara zinazoongoza kwa mapato (mapato kwenye mabano ni Nishati na Madini (Sh220 bilioni), Fedha (Sh126 bilioni), Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (Sh100 bilioni), Maliasili na Utalii (Sh84 bilioni), Mambo ya Ndani (Uhamiaji Sh92 bilioni na Usalama Barabarani Sh17 bilioni), Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi (Sh19 bilioni), Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (Sh16 bilioni).


Hata hivyo, Zitto alisema mapato ya Serikali yameongezeka kwa asilimia 60 kutoka Sh500 bilioni mpaka Sh800 bilioni.


Maazimio


Pia kamati tatu zinazosimamia hesabu za Serikali zimetoa maazimio 14 baada ya kumalizika kwa mafunzo yaliyofanyika Bagamoyo wiki iliyopita.


Kamati hizo za PAC, Bajeti na ile ya Serikali za Mitaa (LAAC), zimeagiza kuwapo kwa mkutano kati ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Hazina, Hesabu za Bunge, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ili kupata usahihi wa deni la taifa.



Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company