MAKALA; Kapteni Mstaafu Robert: Sitasahau nilipohukumiwa maisha jela




Rubani wa ndege aliyeonja kifo kwa ajali ya ndege na kifungo cha maisha, Rubani huyu ni Kapteni Mstaafu Rodrick Robert (69). Picha na Maktaba
Na Lauden Mwambona, Mwananchi

Nje kidogo ya Mji wa Songea, kipo kijiji kinachoitwa Mateka. Bila shaka jina la kijiji hicho lina historia yake, lakini kubwa ni kwamba ndiko anakoishi rubani wa ndege aliyeonja kifo kwa ajali ya ndege na kifungo cha maisha.
Rubani huyu ni Kapteni Mstaafu Rodrick Robert (69) mrefu, mweupe ambaye si mnene na wala si mwembamba akiwa na nywele laini zinazoashiria wazi kwamba mmoja wa wazazi wake alikuwa mtu wa nje ya Bara la Afrika.
Ni mara ya kwanza kumwona alipokuwa akifungua mlango, lakini anatoka na tabasamu baada ya kuona wageni nje wakiwa na mkewe aitwaye May Daud Robert aliyeniongoza kufika hapo mara ya pili baada ya kumwomba aachie kidogo kazi yake mjini Songea na kunipeleka nyumbani kwake nikaonane na mumewe.


Kwa kweli ilikuwa mara ya pili kwangu kufika pale saa 11.00 jioni baada ya mara ya kwanza ya saa 4.00 asubuhi ya siku hiyo kuwakosa nilipopelekwa na msamaria kwa pikipiki mbili.


Robert anatukaribisha ndani huku akisema alipata taarifa za kuwapo kwa wageni wanaomtafuta tangu asubuhi. Tunaingia ndani na kufika kwenye sebule ikiwa na makochi ya kawaida na hatimaye Robert, mkewe na mimi tunaketi.


Akiwa anamwangalia mkewe aliyeketi upande wa kushoto kwake, Rubani Robert ananikaribisha.


Anasimulia kidogo historia yake.


Rubani: Nilizaliwa Mtaa wa Mtini mjini Songea mwaka 1944 na baba yangu alikuwa mhandisi wa kujenga barabara na nyumba za Serikali na alishiriki kujenga Uwanja wa Ndege za Jeshi Dar es Salaam.


Nilisoma chekechea mjini Songea, Shule ya Msingi Songea na Peramiho baadaye Sekondari ya Wavulana Songea kabla ya kujiunga St Michael ya Iringa ambayo baadaye ikawa Mkwawa Sekondari na sasa ni chuo.


Baada ya kumaliza Mkwawa nilingia Chuo Kikuu cha Dar e Salaam kuchukua Sayansi ya Jamii, lakini nilisoma mwaka mmoja nikaacha.


Mwandishi:Ni sababu zipi zilikuachisha chuo?


Rubani: Sikumbuki.


Mwandishi:Baada ya kuacha chuo kikuu ulikuwa unafanya nini?


Rubani:Nilikuwa nyumbani nikijishughulisha na uandishi na pia kuchora jambo ambalo lilinifanya niitwe kwenye mafunzo ya siku sita kuhusu uandishi Chuo Kikuu cha Makerere ambako nikawa mmoja wa watu wa kwanza tulioandika jarida la kwanza la chuo hicho. Niliporudi nchini nilipata kazi kwenye Shirika la British America Tobacco Company (BAT) ambako nilifanya kazi karibu mwaka mmoja na baadaye niliacha.


Mwandishi: Ni kwa nini uliacha?


Rubani: Sikumbuki.


Mwandishi: Baada ya hapo ulikwenda wapi?


Rubani: Nakumbuka mwaka 1970 nikiwa nyumbani Songea, alikuja Jenerali Luis ambaye alikuwa mwenyeji wa Mkoa wa Rukwa na kuniambia kwamba walikuwa wakihitaji vijana waliosoma ili wawe marubani wa jeshi. Hoja hiyo niliipenda na nikakubali, hivyo aliniandikisha na kunitaka niende kwenye mafunzo ya kijeshi (TMA) Dar es Salaam kwa ajili ya uofisa.


Nilimaza mafunzo kwenye kikosi cha anga Dar es Salaam na baada ya hapo pamoja na wenzangu karibu 14 tuliendelea na mafunzo ya kuendesha ndege kwa chini (Ground School) kwa mwaka mmoja na baada ya hapo tulianza mafunzo ya awali ya kurusha ndege.


Mwandishi: Tangu mafunzo hadi kuanza kazi, je uliwahi kupata ajali?


Rubani: Ndiyo, nilipata ajali mwaka 1978 nikiwasafrisha askari 26 kutoka Dar es Salaam kwenda Beira Nover Freesco Msumbiji ingawa sikujua askari wale walikuwa wakienda nchi gani. Sijui walikuwa wa Zimbabwe au Angola sijui. Injini ya kushoto ilizimika ghafla na baadaye injini ya kulia ikazima hivyo nililazimika kutua kwenye shamba dogo porini na askari wote tulitoka salama isipokuwa mmoja alipata michubuko kutokana na bawa la ndege kugonga kichuguu. Kipande hiki (anainuka kuchukua na kukionyesha kichuma cha bawa la ndege) nilipewa kama kumbukumbu.


Baada ya ajali hiyo, mwishoni mwa mwaka 1978 nilikwenda Uingereza kusoma utaalamu wa ndege aina ya Hauca Cidre748.


Mwandishi:Je, vita dhidi ya Idd Amin Dada ulishiriki?


Ruban: Tangu mwanzo hadi mwisho mimi nilikuwa mmoja wa walioshiriki mchana na usiku hadi vilipoisha.


Mwandishi: Unakumbuka nini kwenye vita hivyo?


Rubani: Nakumbuka siku moja nilikuwa off (napumzika kidogo), nikaamua kunywa bia. Na ratiba ilikuwa ikionyesha nitakuwa kazini kesho yake. Lakini ghafla kiongozi wangu alinijia na kunitaka nirushe ndege. Mimi nilikataa katakata kwa sababu nilikuwa nimekunywa pombe. Niliwahi kumwendesha Nyerere.


Mwandishi: Je, ni kweli ulimwendesha Nyerere? Na kazi ya jeshi iliendelea hadi lini?


Rubani: Ni kweli baada ya vita vya Amini niliendelea kurusha ndege za jeshi na pia kufanya kazi ya kuendesha ndege ya Rais Nyerere. Mwaka 1983 Januari 7, nilikamatwa na wanajeshi wengine wengi kwa tuhuma za uhaini. Tulidaiwa tulitaka kumuua Rais Julius Nyerere. Nilikamatwa nikiwa eneo la Airwing Dar es Salaam. Tulikaa kizuizini hadi Julai mwaka 1983 Mahakama ilipotangaza kwamba hatukuwa na kesi ya kujibu. Lakini cha kushangaza mwaka 1985 watu tisa kati ya wale walioshikiliwa mara ya kwanza, tulikamatwa tena na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kutaka kumuua Rais Nyerere.


Mwandishi: Je, kiukweli mpango huo ulikuwapo?


Rubani. Aaa...ulikuwapo haukuwapo, ‘it was planned by high official (ulipangwa na baadhi ya maofisa za ngazi za juu)’, unajua baada ya vita vya Uganda nchi ilikuwa imefilisika. Haikuwa na unga, sabuni, sukari na hata nguo, karibu kila kitu hakikuwapo. Hivyo Watanzania wengi walikuwa wamechanganyikiwa na hali ile.


Mwandishi: Kwa maana hiyo mpango huo ungefanikiwa je bidhaa hizo zingeonekana?


Rubani: Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi aliiokoa nchi baada ya kuruhusu kila kitu kiingie nchini hata bila ya kutoza kodi. Mwinyi aliituliza nchi. Pia Serikali iligundua kwamba waliokamatwa walitaka mfumo wa vyama vingi vya siasa ili kuishtua CCM ambayo ilikuwa imejisahau na hivyo kuanzishwa kwa vyama vingi jambo ambalo lilitekelezwa baadaye.


Mwandishi: Matatizo yaliyokuwapo enzi hizo na sasa unatofautishaje?


Rubani:Kama nilivyosema, enzi za Nyerere nchi ilifilisika, Mzee Mwinyi aliiokoa nchi, Rais Mkapa akaweka msingi wa kukusanya kodi, hivi sasa sijui kinachoendelea kwa kuwa sisomi sana magazeti kwani sina fedha za kununua.


Mwandishi: Mama Robert ulifanikishaje safari yako kurudi Songea. ?


Mkewe: Mimi niliposikia anafungwa maisha nilipigwa na butwaa na simanzi kubwa. Hivyo sikuwa na nguvu, lakini cha ajabu, baada ya saa 12 kupita, mkuu wa kikosi aliniita na kunitaka niondoke kwenye nyumba ndani ya saa 24. Kumbuka wakati ule mimi nilikuwa nafundisha Chuo Cha Utumishi Magogoni Dar es Salaam, hivyo nilihitaji kupata nafasi ya kuomba uhamisho na kufunga mizigo. Lakini mambo ya jeshi ni amri na nilitolewa mizigo ili nisafirishwe kwa ndege ya Jeshi ambayo nayo iliharibika. Lakini kwa bahati ilipona kabla ya saa 12 kumalizika, nikatakiwa nitaje niende wapi.


Suala hilo lilinifanya nitaje Songea kwa vile nilikuwa na watoto sita na Robert na watoto walikuwa wakiwafahamu ndugu wa Songea.


Hivyo mizigo na watoto walisafiri kwa ndege mimi nikabaki Dar es Salaam nikiomba uhamisho wa kwenda kufundisha Shule ya Sekondari ya Songea Wasichana.


Kwa kweli ilikuwa fedheha kubwa. Serikali inampenda mfanyakazi mzuri, lakini huyohuyo akiteleza kidogo ni takataka. Ipo haja ya kubadilisha msimamo huo.


Mwandishi: Kwako rubani, je unalo neno kwa Serikali?


Rubani:Aaaa , tangu nifike huku sijapata na wala sina senti ya Serikali. Wapo wenzangu waliosema eti Serikali inafikiria kutupatia chochote, lakini mpaka sasa sijasikia lolote.


Mwandishi: Kwa sasa afya yako ikoje na unajishughulisha na nini?


Rubani. Afya yangu nashukuru Mungu naendelea vyema, mambo mengine Mungu anasaidia.


Kapteni Mstaafu Rodrick Robert anasema ni suala la msingi kwa watu kuwa na moyo wa kulitumikia taifa kwani ndio msingi wa kuhakikisha tunakuwa na taifa lenye maendeleo makubwa.


“Jambo la msingi ambalo napenda kusisitiza ni moja tu kwamba kwa kila kitu ambacho mtu anafanya, anapaswa kuweka mbele maslahi ya taifa kwanza,” anasisitiza akiwaasa Watanzania kujenga tabia ya kuheshimu mila na tamaduni za taifa, pia kujali maadili ya uongozi.


Aidha anawashauri vijana kufanya kazi kwa bidii ili kuharakisha maendeleo nchini, kwani vijana ndio tegemeo kubwa kwa taifa na ulimwengu kwa ujumla kwa vile wana nguvu za kutosha.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company