NA MWANDISHI WETU
HATUA ya Marekani kudaiwa kufuatilia mawasiliano ya viongozi wa nchi washirika wake wa karibu, sasa ni wazi imeiacha Tanzania katika wingu la shaka, kama viongozi wake nao wanafuatiliwa kwa namna ile ile inayoelezwa na viongozi wa Ulaya. Shaka hiyo inatokana na urafiki wa muda mrefu uliopo kati ya Tanzania na Marekani, ambapo kwa nyakati tofauti, marais watatu wa taifa hilo kubwa duniani wamepata kuzuru nchini.
Kauli tofauti zilizotolewa ndani ya wiki hii na majasusi wa mataifa makubwa duniani, ikiwemo Marekani na Uingereza, wakati wakizungumzia madai ya Marekani kufuatilia mawasiliano ya Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, kwamba nchi zote duniani zinachunguzana, ndiyo ambayo baadhi ya wafuatiliaji wa mambo wanadai kuwa Tanzania bila shaka haiwezi kukwepa kufuatiliwa.
Mbali na hiyo, kauli ambayo imepata kutolewa na mfanyakazi wa zamani wa shirika la NSA, Edward Snowden, kwamba ujasusi huo wa Marekani haufanywi dhidi ya watuhumiwa wa ujasusi na wakazi wa nchi zenye ugomvi na Marekani tu, bali hata marafiki na waitifaki wa karibu kabisa na nchi hiyo, ndiyo ambayo inajenga mazingira ya Tanzania nayo kuwemo kwenye orodha hiyo ya kufuatiliwa.
Marais watatu wa Marekani, kwa nyakati tofauti wamepata kuzuru nchini. Maraisi hao ni pamoja na Bill Clinton, George W. Bush na Barack Obama, ambaye alitembelea nchini mwezi Julai, mwaka huu.
Ni kutokana na hilo, hulka ya vyombo vya usalama vya Marekani kuhakikisha usalama kwa viongozi wao haiwezi kuwatenga na suala zima la kufanya udukuzi kwa nchi ambazo zina ushirika nao, lakini pia viongozi wake wanatembeleana.
Kwa muktadha huo, tayari baadhi ya wachambuzi waliozungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini wanasema kuwa uwezekano wa Marekani kufuatilia mawasilino ya viongozi wa hapa nchini, akiwemo Rais wa sasa, Jakaya Kikwete ni mkubwa na ni jambo lisilo la kushangaza.
Wachambuzi hao wanazilinganisha taarifa za sasa za udukuzi wa mawasiliano unaodaiwa kufanywa na Marekani na mchezo ambao ulipata kufanywa huko nyuma na mtandao wa Weakleaks, dhidi ya Tanzania.
Mtandao huo umepata kuwagusa viongozi wa serikali, akiwemo Rais Jakaya Kikwete, kutokana na taarifa za siri ilizodai kuzinukuu kutoka kwa baadhi ya maofisa wa Ubalozi wa Marekani nchini.
Kwa takribani wiki mbili sasa, Marekani imejikuta katika mzozo wa kidiplomasia na baadhi ya mataifa ya Ulaya, baada ya kuibuka madai kuwa Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, simu zake zimekuwa zikifuatiliwa kwa karibu muongo mmoja sasa.
Kama ilivyo kwa Tanzania na pengine zaidi ni kwamba Marekani na Ujerumani, zimekuwa na ushirika wa karibu kwa muda mrefu sasa.
Juni mwaka huu, mwanausalama aliyeasi wa Marekani, Edward Snowden, alitoboa siri ya idara za usalama nchini humo kwamba zimekuwa zikifuatilia mawasiliano ya simu na barua pepe kwa watu mbalimbali duniani kote, wakiwamo viongozi wenye ushirika wa karibu na taifa hilo.
Hata hivyo, Marekani imekana kufanya udukuzi kwa namna ambayo imetafsiriwa na baadhi ya washirika wake na badala yake imedai kuwa udukuzi ambao imekuwa ikiufanya ni wa kawaida kwa ajili ya usalama na kwamba wamekuwa wakirejesha taarifa zote kwa nchi husika.
Mkurugenzi wa Idara ya Usalama ya Marekani, James Clapper, alisema upelelezi wa Marekani katika mataifa ya kigeni huwa haufanywi kiholela.
"Nia ya viongozi ndiyo moja ya sababu kuu ya kwanini tunafanya upelelezi na kuutathmini...washirika wa kimataifa wa Marekani pia huchunguza maofisa wa Marekani na mashirika mengine kama sehemu ya mipango ya serikali,"alisema Clapper.
Chanzo:Mtanzania mtandaoni