Rais wa Uganda Yoweri Museveni katika picha.
Jeshi la Uganda UPDF linasema litashambulia watu au makundi yanayotupa mabomu nchini Uganda kwenye maeneo yaliyo karibu na mpaka wa Uganda na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo katika mji wa Bunagana. Msemaji wa jeshi aliyasema haya baada ya bomu moja kutupwa nchini Uganda wiki iliyopita na mabomu mengine sita kutupwa jumatatu ya wiki hii.
Serikali ya Uganda inasema imetijahidi kadri ya uwezo wake kuwasaidia wakongomani wanaokimbilia nchini Uganda na pia imejaribu iwezavyo kama mpatanishi kwenye mazungumzo ya amani kati ya waasi wa M23 na serikali ya Kinshasa, kuhakikisha kuwa utulivu unarejea nchini Congo na hivyo, sio haki kutupiwa mabomu.
Mabomu haya yalitupwa na nani na yalikuwa yakimlenga nani? Luteni kanali Paddy Ankunda ni msemaji wa jeshi la Uganda, alihoji.
Kufikia sasa luteni kanali Ankunda anasema serikali ya Congo haijasema chochote licha ya kuwa Uganda iliwasilisha rasmi malalamiko yao. Ili kuhakikisha kuwa hakuna mabomu mengine yanayotupwa nchini Uganda, jeshi la UPDF tayari limewatuma wanajeshi wake karibu na mpaka wa Uganda na Congo wa Bunagana.
Kwingineko, kufuatia kushambuliwa kwa ngome za waasi wa M23 mashariki mwa Congo kuanzia wiki jana na wanajeshi wa serikali ya Congo, baadhi ya wanajeshi hawa walikimbilia nchini Uganda kuyanusuru maisha yao.
Kikundi cha waasi wa M23 jana kilitangaza kuwa kimesitisha vitendo vyao vya uasi na kitafuata njia za kisiasa ili kupata suluhisho la matatizo yalipelekea kuundwa kwa kundi hilo.