Wagombea kiti cha rais Tanzania waanza kujitokeza.

Waziri mkuu wa zamani wa Tanzania Sumaye

Wakati ambapo Tanzania inaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani mwaka 2015, baadhi ya wanasiasa maarufu ndani ya chama tawala CCM, wamekuwa wakipigana vikumbo na vijembe kwa kile kinachoonekana kama harakati za kujisafishia njia kuwania uongozi wa nchi katika nafasi mbalimbali.
Siku ya Jumatatu mjini Dodoma kwenye kikao cha bunge kinachoendelea, waziri mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa alijipambanua na kuwashambulia baadhi ya watendaji serikalini kwa kutowajibika ipasavyo, Jumanne mwanasiasa mwingine waziri mkuu mstaafu Frederick Sumaye ameunguruma jijini Dar es salaam kuzungumzia masuala anayodai yamekuwa kikwazo kwake ikiwemo rushwa kuchafuana na utendaji mbovu.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Jumanne, Bw. Sumaye ambaye kwa kipindi chote cha miaka kumi cha awamu ya tatu ya uongozi wa rais mstaafu Benjamin Mkapa alikuwa waziri mkuu, ameelezea kukerwa na wanasiasa anaosema wamekuwa wakimchezea rafu kwa wao kujisafishia njia kwa kumchafua wengine kwa kutumia rushwa na ufisadi.

Hata hivyo Bw. Sumaye, hakuwa wazi ni njia ya kwenda wapi hiyo anayowekewa vikwazo licha ya kukiri kwamba anao uwezo wa kugombea Urais katika uchaguzi mkuu ujao na kwamba chama kimekataza kutangaza nia mapema.

Bw. Sumaye pia ametangaza kuunga mkono uamuzi wa mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi, Jakaya Kikwete wa kupambana na rushwa na kumtaka mbali ya kushughulikia rushwa ndani ya chama aishughulikie pia ndani ya serikali huku akionya kwamba ikiwa CCM itapitisha wagombea uongozi wenye tuhuma za rushwa na ufisadi, basi chama hicho kinachoshikilia dola kitaanguka na pia yeye hataweza kukaa nao.

Miongoni mwa wanasiasa wengine wanaotajwa kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao kupitia chama tawala CCM ni waziri wa sasa wa mambo ya nje Bernard Membe, Samwel Sita, Emmanuel Nchimbi na wengineo.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company