Wanamgambo wa Al Shabaab nchini Somalia
Na
Flora Martin MwanoWatu zaidi ya sita wamepoteza maisha kufuatia shambulizi la kigaidi lililotekelezwa jana ijumaa jioni na watu wanaodhaniwa kuwa wanachama wa kundi la wanamgambo wa Al Shabaab katika hoteli ya Maka al Mukarama mjini Mogadishu nchini Somalia, Polisi wameimarisha usalama katika eneo hilo ambalo hutembelewa zaidi na Maofisa wa serikali na wafanyabiashara maarufu.
Msemaji wa serikali Ridwan Haji Abdiwali amesema mtu mmoja anashikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na shambulizi hilo na uchunguzi zaidi unaendelea ili kuwabaini wahusika wengine.
Taarifa toka nchini humo zinesema polisi wanne na Ofisa mmoja wa serikali ni miongoni mwa watu waliouawa.
Mogadishu imeendelea kukumbwa na mashambulizi ya kujitoa mhanga na yale ya kutegwa yanayotekelezwa na kundi la al-Shabaab ambalo ilitimuliwa kutoka katika ngome zao muhimu.
Shambulizi hilo limekuja wakati huu ambapo kikosi cha Umoja wa Afrika AU kilichopo nchini humo AMISOM kikilitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC kuliongezea nguvu jeshi lao kwa kuongeza idadi ya wanajeshi kama jitihada za kulitokomeza kabisa kundi la al-Shabaab.