Na Maggid Mjengwa,
Ndugu zangu,
Tuanze na bashraf kwa maana ya mrejesho;
"Vijana wale walimchinjia Mandela mbuzi kwa heshima yake. Naye Mandela aliongea nao. Akawaambia;
" Mafunzo ya kijeshi sharti yaende sambamba na mafunzo ya kisiasa. Maana, kufanya mapinduzi haina maana ya kufyatua risasi tu, bali, kutengeneza jamii ya haki na usawa."
Na baada ya maelezo hayo kwa vijana wale makuruta, Mandela anasimulia
kitu alichokifanya kwa mara ya kwanza;
" It was my first time that I was ever saluted by my own soldiers!"
Kwamba ikawa ni mara yake ya kwanza kupigiwa saluti na askari wake.... Endelea...
Naam, akiwa Dar es Salaam, Nyerere alimpa Mandela ndege maalum impeleke Mbeya na baadae aunganishe kwenda Afrika Kusini kwa kutua kwanza Lobatse kwenye nchi ya Botswana.
Mandela anasimulia juu ya safari yake hiyo ya kutoka Tanganyika kurudi nyumbani Afrika Kusini, anasema, kuwa Julius Nyerere alimkodishia ndege binafsi kumrusha kwenda Mbeya. Baada ya hapo naye akaendelea na safari yake hadi Lobatse.
Akiwa kwenye ndege kutoka Mbeya kuelekea Lobatse, Botswana, rubani alimweleza Mandela, kuwa wangetua kwanza Kanye. Jambo hilo lilimshtua Mandela. Akajiuliza, ni kwa nini mpango wa safari yake umekatishwa.
Akiwa Kanye, Mandela akakutana na hakimu wa eneo hilo akiwa na askari wa usalama, wote wawili walikuwa ni Wazungu. Hakimu yule akamtaka Mandela ataje jina lake.(P.T)
" David Motsamayi" alijibu Mandela.
" Hapana, alisema hakimu yule.
" Tafadhali nieleze jina lako halisi"
Mandela akarudia tena kutamka, kwamba anaitwa David Motsamayi.
Mwanasheria yule hakimu akamsisitiza Mandela ataje jina lake halisi kwa kudai kuwa, naye ameagizwa kukutana mahali hapo na mtu anayeitwa Nelson Mandela ili amsaidie na usafiri. Kisha akasema;
" Kama wewe si Nelson Mandela, basi, nitalazimika nikukamate kwa vile huna ruhusa ya kuingia nchini. Je, wewe ni Nelson Mandela?"
Kwa Mandela hilo lilikuwa ni swali la mtego, maana, majibu yote, ndio au hapana yumkini yangepelekea akamatwe.
Mandela akasema;
" If you insist that I am Nelson Mandela and not David Motsamayi, I will not challenge you" ( Nelson Mandela, Long Walk To Freedom, pg.365)
Bwana yule hakimu alimwangalia Mandela akitabasamu, akatamka;
" Tulikutarajia uwasili jana. Kisha akampa lifti ya gari Mandela kuelekea waliko wanaharakati wengine wapiganaji wa ANC. Huko Mandela alikuwa akisubiriwa kwa hamu. Wakafika mji wa Lobatse ambapo Mandela alikutana na Joe Modise na mfuasi mwingine wa ANC aliyeitwa Jonas Matlou ambaye aliishi mahali hapo.
Hakimu yule alimweleza Mandela, kuwa polisi wa Afrika Kusini tayari wanazo taarifa kuwa yeye Mandela alikuwa njiani kurudi Afrika Kusini. Hivyo, akamshauri Mandela aondoke siku ya pili yake.
Hata hivyo, Mandela mashaka yakamwingia, alipofika nyumbani kwa Matlou akamwambia mwenyeji wake, kuwa angeondoka usiku huo huo. Ikapangwa Mandela aondoke na Bwana Cecil Williams, Mwafrika Kusini mweupe na ambaye alikuwa mwanaharakati wa Umkhoto We Sizwe.
Mandela akaondoka usiku huo akiwa na Cecil Williams kwa kuendesha gari hilo kuelekea Johannesburg. Mandela aliendesha akijifanya ' Dereva wa Mzungu'!
Ni nini kilimtokea Mandela baada ya kuvuka mpaka wa Botswana na kuingia ndani ya ardhi ya Afrika Kusini?
Jibu utalipata mchana wa leo
Asubuhi njema.
0754 678 252
NA BLOGU YA MJENGWA.