Waasi wa Seleka mjini Bangui
Wanajeshi wa Ufaransa wameanza kuwapokonya silaha waasi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Leo asubuhi makabiliano yalitokea kati ya wanajeshi hao na wapiganaji wa serikali mjini Bangui, wakati shughuli hiyo ilipoanza.
Masemaji wa jeshi la Ufaransa, alisema kuwa wanajeshi waliwakamata wapiganaji kadhaa na kunasa silaha walizokuwa wanatumia.
Kikosi cha wanajeshi 1,600, kimepelekwa nchini CAR baada ya siku kadhaa za mapigano yaliyosababisha vifo vya watu 400.
Kiongozi wa waasi, Michel Djotodia, aliingia mamlakani mwezi Machi kwa usaidizi wa wapigajani wake ambao wengi wao ni waasi wa zamani. Djotodia amechukua mamlaka baada ya kumpindua aliyekuwa Rais Francois Bozize.
Wanajeshi wa Ufaransa, sasa wanashika doria katika barabara na mitaa ya mji mkuu Bangui.
Walikwenda Bangui siku ya Ijumaa baada ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuunga mkono azimio la kurejesha utulivu nchini humo kwa kutumia njia yoyote itakayofaa, hata kama ni kwa nguvu.
Nyumba zimeharibiwa kwa maguruneti kufuatia makabiliano makali kati ya waasi hao na wanajeshi na pia kutokana na vita vya kidini ambavyo vimetokana na vurugu hizo.
Wakati wa mapigano, mamia ya waumini wa kiisilamu walikimbilia katika nyumba ya Imamu mmoja ambako walikwenda kutafuta hifadhi.