Bunge Katiba mwamuzi wa mwisho, asema Kikwete



“Lengo ni kuunda katiba yenye masilahi ya nchi na si watu au kikundi cha wachache, jukumu lililobaki ni la wananchi wenyewe kupitia kwa wawakilishi wao kabla ya kupigwa kura ya maoni,” Kikwete
Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi
Zanzibar. Rais Jakaya Kikwete, amesema Bunge la Katiba ndilo litakalotoa uamuzi wa mwisho kuhusu Katiba Mpya kabla ya kupigiwa kura ya maoni na wananchi.
Rais Kikwete alitoa msimamo huo jana katika viunga vya Maisara Suleiman.


Msimamo huo umekuja huku vyama vikuu vya siasa visiwani Zanzibar vikitofautiana kuhusu yaliyoko katika Rasimu ya Katiba Mpya.


Kwa upande wake, CCM inapinga mfumo wa Serikali tatu wakati CUF inaunga mkono mapendekezo hayo.


Rais Kikwete alisema Tume ya Jaji Warioba imemalizika kazi zake na kwamba kazi ya msingi sasa imeanza.


Alisema wananchi bado wana nafasi ya kutoa maoni yao kupitia kwa wabunge na wawakilishi wao na kwamba uamuzi wa mwisho ni wao kwa kupiga kura ya maoni.


“Kazi ndiyo kwanza imeanza, mkoko ndiyo unaalika maua, wananchi wenyewe wataamua kwa hiari yao lipi litafaa na lipi halihitajiki kuwekwa kwenye kwenye Katiba Mpya, hebu kaeni na wabunge wenu mjitosheleze, semeni bila ya kificho, mnataka lipi na lipi hamkubaliani nalo,” alisema Rais Kikwete.


Aidha, alisema kuna baadhi ya watu bila aibu wanapita mitaani wakipotosha kwamba Katiba Mpya imekamilika jambo ambalo si la kweli.


Alisema baada ya kuwasilishwa kwa rasimu ya pili, hatua inayofuata ni rasimu hiyo kutajadiliwa na Bunge la Katiba na kufuatiwa na kura ya maoni.


Rais Kikwete alisema wananchi wana nafasi ya kuendelea kutoa maoni yao ili kupata katiba safi na kwamba si lengo la taifa kuunda Katiba itokanayo na kundi fulani.


“Lengo ni kuunda katiba yenye masilahi ya nchi na si watu au kikundi cha wachache, jukumu lililobaki ni la wananchi wenyewe kupitia kwa wawakilishi wao kabla ya kupigwa kura ya maoni,” alifafanua Rais Kikwete.


Akizungumzia Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Rais Kikwete aliwahimiza vijana kuyathamini na kuyaenzi kwa kuzingatia kuwa yameondosha dhuluma na ukandamizaji uliofanywa na utawala wa kisultan.


“Mapinduzi ya Zanzibar ndiyo ukombozi na uhuru kamili, hata waliokuwa wakikandamiza wenzao nao walikombolewa na kujitambua. ASP ilijenga nchi isiyokuwa na uonevu wala ukandamizaji, kikaleta usawa na uhuru kamili,” alisema.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM, Sadifa Khamis Juma alimkumbusha Rais Kikwete kuwa nia njema ya CCM ya kukubali maridhiano ya kisiasa haijaheshimiwa na wapinzani wao Zanzibar.


Alisema hali hiyo inadhihirishwa na kejeli dhidi ya mapinduzi na watu kutaka kuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Sadifa alisema UVCCM haitakubali kusimama na kiongozi yeyote wa kisiasa au kiserikali mwenye nia ya kuvunja Muungano au kuyasaliti Mapinduzi ya Zanzibar.
Akisoma taarifa fupi, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka alisema maoni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Warioba hayakubaliki na yamekosa mashiko, uzalendo na nguvu ya kudumisha umoja wa Kitaifa.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company