Lowassa aitesa CCM, Yaunda tume kuwakabili wanaotangaza nia mapema

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeunda timu ya kuwachunguza makada wake wanaodaiwa kutangaza nia ya kuwania uongozi kabla ya wakati, na wanaomwaga fedha kwa wajumbe wa mkutano mkuu ili kuwashawishi wawaunge mkono katika nia zao.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Makamu Mwenyekiti wa CCM taifa, Philip Mangula wakati akifungua kikao cha kwanza kwa mwaka huu cha tawi la ofisi ndogo za CCM jijini Dar es Salaam kilichokuwa na ajenda ya kutoa uongozi wa siasa katika eneo husika.
Ingawa Mangula hakutaja majina ya makada wa CCM wanaodaiwa kukiuka kanuni kwa kutangaza nia mapema, lakini kwa kauli hiyo ni dhahiri kwamba alikuwa akimlenga Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ambaye juzi alitangaza nia kiaina.

Lowassa katika hotuba yake ya kufunga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka mpya 2014 nyumbani kwake Monduli, alikaririwa akisema ameanza rasmi safari aliyoiita ya matumani ya ndoto zake, ambayo pia itatimiza ndoto za Watanzania za kupata elimu bure, maji safi na maendeleo ya uhakika.

Lowassa ambaye amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa wagombea wa nafasi ya urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, aliyasema hayo katika ibada ya shukrani ya kuupokea mwaka mpya, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Monduli.

Katika hafla hiyo, Lowassa anadaiwa kuwasafirisha baadhi ya wajumbe wa vikao muhimu vya maamuzi vya chama na kuwapa fedha, malazi na kadi za Krismasi ambazo zinadaiwa kuambatanishwa na fedha.

Kauli ya Mangula kumuonya Lowassa na wengine wanaodaiwa kuvunja kanuni, inafanana na ile ya Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye ambaye jana alikaririwa akisema Lowassa amevunja kanuni, hivyo kupoteza sifa ya kugombea nafasi za uongozi ndani na nje ya chama hicho.

Akizungumza katika mkutano wa jana, Mangula alisema baadhi ya makada wa chama hicho wameanza kampeni na kutoa zawadi, jambo ambalo alisisitiza kuwa sio sahihi.

Mangula aliyeambata na Katibu taifa wa Tume ya Udhibiti na Nidhamu ya CCM, Masoud Mbengula alilazimika kusoma kanuni za chama hicho.

Alisema kuwa vurugu zinazotokea katika nchi nyingi zinasababishwa na rushwa.

“Rushwa ni dhambi kubwa, na kanuni zinakataza rushwa katika ibara ya sita kifungu cha kwanza na cha pili kipengele moja hadi tatu.

“Lakini watu wameshaanza kununulia watu kadi za uanachama, huku wakijua kuwa jambo hili lilisababisha chama kushindwa katika uchaguzi uliopita, wanaanza kuamini kampeni zimeanza.

“Wanasafirisha wenyeviti, kuwapa mahitaji yao, wakati hakuna kikao chochote kilichoamua ama kutangaza kampeni wao wanatimka kabla ya uchaguzi na atakayethibitika atachukuliwa hatua,” alisema Mangula.

Alisema kanuni za CCM zinakataza kwa kiongozi kutumia dini, kabila, rangi ama eneo analotoka kama sifa ya kushawishi wapiga kura wamchague ikiwemo kujenga na kudumisha makundi yenye sura ya kuvuruga umoja na mshikamano.

“CCM haiwezi kuongozwa na watu wenye makundi, maana wanavuruga umoja ili kutaka uongozi.

“Watu wanaofanya kinyume na kanuni za CCM ni waasi na wasaliti, hatuko tayari CCM isiwepo tena kwa ajili yao, hatuwezi kuacha uasi uendelee, hatukubaliani na uroho wao wa madaraka,” alisema.

Alisema CCM haiko tayari kuingizwa moja kwa moja katika mivurugano ya ndani na waasi wachache.

Mangula aliendelea kusema kuwa anashangazwa na huruma ya hela inayotolewa na watu hao, akihoji inatoka wapi na kwanini katika kipindi hiki.

“Sina ugomvi na mtu, kama tungetaka mtu mwenye pesa nyingi ndio awe kiongozi wa nchi hii, basi tungetangaza tenda ili tushindanishe nani ana pesa nyingi awe kiongozi,” alisema Mangula.

Alisema kuwa anawashangaa watu hao wanafuata ilani ipi katika kampeni zao kwani ajenda ya CCM ni kutekeleza ilani ya uchaguzi hadi mwaka 2015.

“Unamkosesha raha aliyeko madarakani asimamie yapi sasa, hii ni ilani ya chama lazima ifuatwe, na kama mtu hawezi kusimamia kanuni za chama ataweza kweli kuongoza nchi?” alihoji Mangula.

Alisema kuwa katika uchaguzi wa mwaka 2012 ndani ya CCM walipokea malalamiko 94.

Mangula alisema kuwa tayari malalamiko 33 yameshafanyiwa kazi na kuongeza kuwa Kamati Kuu (CC) iliongeza muda wa miezi sita kuyashughulikia.

Akizungumzia rasimu ya pili ya katiba, hasa suala la serikali tatu ambalo CCM wanapingana nalo, Mangula alisema kuwa kazi ya katiba haijaisha na vyema matawi ya chama hicho yakaendelea kuelimisha wanachama na kufanya majadiliano.

Alisema kwa kuwa mchakato wa katiba mpya haujaisha wataijadili kwani bado wako njiani na wenye mamlaka ya uamuzi wa mwisho ni wananchi.

Guninita amtetea Lowassa, amvaa Nape

Wakati Mangula na Nape wakimshughulikia Lowassa kwa nyakati tofauti, kada mkongwe na maarufu wa CCM, John Guninita amemvaa Nape na kumtaka kutumia vikao halali kutoa msimamo wa chama.

Guninita alitoa kauli hiyo jana kujibu hoja za Nape aliyesema mwanachama anayevunja kanuni, anapoteza sifa ya kuwania uongozi, pia alibeza kauli ya Nape kuwaita mawaziri wazembe kuwa ni mizigo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Guninita ambaye amepata kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, alisema kuwa kauli za Nape hazina baraka za chama, hivyo ni bora awe anatoa msimamo na kauli za chama baada ya vikao.

Akitolea mfano wa kauli za Nape, Guninita alisema kiongozi huyo wa CCM juzi alimhukumu moja kwa moja Lowassa kwamba kitendo chake cha kutangaza nia ya kuwania urais, amepoteza sifa ya kuwa kiongozi.

“Kauli hiyo hamtendei haki Lowassa na baadhi ya wanachama, ikizingatiwa kuwa wapo mawaziri kadhaa ambao tangu miaka miwili nyuma wamekwishaanza kujipitisha katika majimbo huku wakitumia magari ya serikali kuusaka urais,” alisema Guninita.

Alisema umefika wakati wa baadhi ya wanasiasa kuacha kulifanya suala la urais kuwa la mizengwe kwani kuna umuhimu kwa Watanzania kuwajua wanaotaka urais mapema.

Huku akijihami, Guninita alisema kuwa yote aliyoyasema Nape, hajatumwa na chama bali ametumia vibaya nafasi yake kama mwanachama anayekerwa na makada anaowahukumu kwamba hawana sifa.

Guninita alisema kazi ya katibu huyo sio kuzungumza maneno yake mwenyewe, bali anapaswa asubiri apangiwe na Mwenyekiti wa CCM taifa ambaye ni Rais Jakaya Kikwete namna ya kuzungumza.

“Mnalijua neno mzigo? Mzigo ni sawa na mtu aliyekufa, hivyo wakati mwingine kumwita mtu mzigo anaweza kuja kushitakiwa, chama hakiwezi kumtuma Nape awaite mawaziri mizigo,” alisema.

Guninita alisema kutokana na kiongozi huyo kutumia maneno yake na kufanya chama kama mali yake, ndiyo maana hata kauli yake ya kuwaita mawaziri mizigo ilipojadiliwa kwenye Kamati Kuu, ilipuuzwa kwani hadi leo hakuna kilichoamuliwa.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company