
MBUNGE wa Moshi Mjini, Philemon
Ndesamburo (CHADEMA),
amesema matatizo yanayokikumba
chama hicho kwa sasa yanatokana
na kundi la watu wachache wenye
uchu wa madaraka, ambao pia
wanatumiwa na Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Ndesamburo alisema kuwa
wanaosababisha hali hiyo ni vijana
ambao hawana uchungu na
CHADEMA, na hivyo kushauri
uongozi uchukue hatua stahiki ya
kinidhamu kwa watu hao.
Mbunge huyo ambaye pia ni
Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa
wa Kilimanjaro, alikuwa akijibu
maswali ya wananchi kwenye
mikutano yake ambapo walitaka
kujua nini hatima ya mzozo
unaoendelea kwenye chama hicho.
Alisema kuwa kiongozi yeyote wa
CHADEMA ambaye anakubali
kuhongwa na kusaliti chama ni
msaliti mkubwa na anahujumu
maisha ya Watanzania milioni 45
ambao wanakitegemea chama.
Ndesamburo alisisitiza kuwa
uongozi wa chama lazime ufanye
uamuzi mgumu kwa wanachama
na viongozi wengine ambao
hawatakuwa na nidhamu ndani ya
chama, kwamba bila kufanya
hivyo watajiamulia watakalo.
“CHADEMA lazima iwe tofauti na
vyama vingine, kwanza kwa
kuwawajibisha wale wote ambao
hawatakuwa na nidhamu ndani ya
chama ili kuwepo tofauti, na kwa
sasabu ni chama cha upinzani,
hatuwezi kuwa kama CCM ambao
wanakumbatia mafisadi,” alisema.
Ndesamburo aliongeza kuwa
CHADEMA kwa sasa ni sawa na mti
wenye matunda, hivyo CCM
haiwezi kuacha kuupiga mawe ila
akaonya kuwa wao wataendelea
kupigana na kuhakikisha chama
kinafanya vizuri.
Kuhusu uchaguzi wa serikali za
mitaa, alisema chama hicho
kimejipanga kuimarisha msingi
wake kuanzia ngazi ya mabalozi,
matawi mikoa hadi taifa.
CHANZO; TANZANIADAIMA
