Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamishna wa Polisi wa kanda hiyo, Suleiman Kova, alisema mwanamke huyo alinaswa Januari 18, mwaka huu katika eneo la Yombo Vituka, Wilaya ya Temeke.
Kova alisema mwanamke huyo alinaswa baada ya Ofisa Mhifadhi Wanyamapori mkazi wa Ukonga, kutoa taarifa kituoni hapo kwamba kuna mwananchi anauza ngozi za chui.
Alisema askari walifika eneo la tukio na kumkamata mtuhumiwa na walipompekua chumbani kwake, walimkuta na nyara hizo za serikali.
Wakati huo huo, jeshi hilo limesema limemuua jambazi sugu la uhalifu wa kutumia silaha katika majibizano ya risasi na polisi.
Alisema awali polisi waliweka mtego ili kuyanasa majambazi hayo Januari 22 baada ya kufanya tukio la uporaji wa sh milioni 29 kwa mfanyabiashara wa Mtaa wa Kariakoo, anayejulikana kwa jina la Shanys Abdalla, mkazi wa Mbezi.
Alisema wakati wakiyazingira ili kuyakamata, majambazi hayo yalishituka na kuanza kuwarushia polisi risasi nao walijibu mapigo na kumjeruhi jambazi mmoja sehemu za kifuani upande wa kulia aliyekuwa amebeba begi dogo.
Kwa mujibu wa Kova jambazi hilo lilipopekuliwa katika begi lake, lilikutwa na bunduki aina ya SAR iliyofutwa namba ikiwa imekatwa mtutu wa kitako pamoja na risasi 11, ambapo risasi moja ilikutwa chemba na nyingine 10 zikiwa zimefungwa kwenye karatasi la nailoni.
Hata hivyo alisema jambazi huyo alipoteza maisha akiwa njiani kwenda hospitali.
Aliongeza kuwa katika eneo la tukio, polisi imenasa vielelezo ambavyo ni pikipiki moja aina ya Fekon yenye namba za usajili T 514 CJT yenye rangi nyeusi iliyokuwa inatumika katika matukio ya ujambazi na maganda matatu ya bunduki aina ya SAR na mengine mawili ya bastola.
Katika tukio jingine, jeshi hilo limemkamata mwanamke mmoja raia wa Kenya Ester Nduta, mkazi wa Salasala Guest House ambaye anadaiwa kuwa mwizi sugu wa magari na aliwahi kufungwa jela miaka mitatu katika Mahakama ya Kinondoni.
Kova alithibitisha kuwa mtuhumiwa huyo alikutwa na vitambulisho mbalimbali, ikiwemo kadi ya Umoja wa Vijana wa CCM namba 1326266, iliyotolewa Julai 2, 2013 Wazo, Kinondoni yenye jina Xristine Phollip, ikiwa na picha yake na kitambulisho cha kazi cha Manzese Bridge Small Traders Organization (MABSTO) chenye namba 0001374, chenye jina la Esther Nduta.
Mtuhumiwa huyo pia alikutwa na kitambulisho cha uraia wa Kenya namba 23378272, Serial Namba 235099738, kilichotolewa Desemba 28, mwaka jana chenye jina la Ester Nduta Ng’ang’a, kitambulisho cha mpiga kura cha Tanzania namba 47413790 kilichotolewa Machi 23, 2010, Mwenge Kijitonyama chenye jina la Esther Nduta Ng’ang’a na kadi ya wageni (Visitor’s Card) namba 028 ya Mabibo Hostel – Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Jeshi hilo pia limefanikiwa kumkamata Grace Andrew (34), mama wa nyumbani, mkazi wa Bunju ‘B’ jijini Dar es Salaam kwa kosa la wizi wa mtoto mchanga wa kike mwenye umri wa mwezi mmoja aitwaye Veis Venus.
Mtoto huyo aliibwa Desemba 27 mwaka jana eneo la Mwenge, Kinondoni.
Kova alisema mtuhumiwa huyo alitenda kosa baada ya kumhadaa mama mtoto Salma Frank (29), mkazi wa Kawe Mji Mpya kwa kumuomba ambebee huku wote wakiwa abiria wa daladala wakitokea Hospitali ya Mwananyamala.
Kwa mujibu wa Kova, walipofika Mwenge kituoni, mtuhumiwa aliteremka haraka na kutoweka na mtoto wakati mwenye mtoto akikusanya vitu vingine alivyokuwa navyo ndani ya daladala hilo.
Kova alisema mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo kwa kushirikiana na Halima Alabi (46), mkazi wa Boko Maliasili, Kinondoni ambaye naye alikamatwa Januari 4 eneo la Boko Maliasili.
Kova alisema watuhumiwa wote baada ya kutenda kosa hilo waliondoka kwenda Sumbawanga, mkoani Rukwa ambapo Grace Chapanga alimdanganya mumewe kuwa ni mjamzito na angependa kwenda kujifungulia nyumbani kwao Sumbawanga.
Alisema upelelezi wa tukio hilo ulifanikisha kumkamata mume wa Grace Daniel James (38), mkazi wa Bunju ‘B’, mfanyakazi wa Uhamiaji Makao Makuu Dar es Salaam na kwenda naye Sumbawanga ambapo walimkuta mtuhumiwa akiwa na mtoto huyo.
“Inasemekana kwamba tangu wafunge ndoa mwaka 2010 hadi sasa wanandoa hao hawajapata mtoto, pia mwaka 2012 Grace alifanyiwa upasuaji wa uvimbe tumboni, ambapo daktari alimwambia kuwa hataweza kushika mimba tena, jambo ambalo Grace hakumweleza ukweli mumewe wala ndugu yake yeyote hadi alipopanga njama na hatimaye kufanikiwa kumuiba mtoto huyo,” alisema Kova.
Kova alisema upelelezi wa shauri hilo unaendelea kwa kufuatilia uchunguzi wa vinasaba (DNA) vya mama mzazi, mtuhumiwa na mtoto aliyeibwa. Mtoto amekabidhiwa kwa mama yake mzazi.
CHANZO TANZANIA DAIMA