CCM yaliteka Bunge la Katiba


Sasa ni wazi kwamba serikali mbili zimeonyeshwa taa za kijani baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukamata uongozi wa Bunge Maalumu la Katiba.
Jana kamati 14 za Bunge hilo ziliwachagua viongozi wake; Mwenyekiti na Makamu na 12 kati yake zilichukuliwa na wajumbe kutoka CCM, chama ambacho tayari kimeweka wazi msimamo wake kuunga mkono Muungano kuwa ni serikali mbili.
Miongoni mwa waliochaguliwa wenyeviti ni Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Sera na Uratibu), Steven Wassira na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Ummy Mwalimu ambao wamekuwa mstari wa mbele kupigia chapuo mfumo huo badala ya serikali tatu zinazopendekezwa kwenye Rasimu ya Katiba.
Wengine ni Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango – Malecela, Naibu Spika wa Bunge la Muungano, Job Ndugai, Mbunge wa Viti Maalumu, Kidawa Khamid Salehe, Mbunge wa Kuteuliwa, Shamsi Vuai Nahodha na Mbunge wa Mlalo, Hassan Ngwilizi.
Wengine wa CCM ni Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah na aliyewahi kuwa Waziri katika serikali zilizopita Paul Kimiti. Pia wamo Mbunge wa Wawi ambaye alifukuzwa uanachama na chama chake cha CUF, Hamad Rashid Mohamed na Mwenyekiti wa kundi la wajumbe 201 wa kuteuliwa na Rais, Francis Michael.
Katika uchaguzi wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge, aliyekuwa mwenyekiti wa Muda na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho alichaguliwa mwenyekiti na makamu wake, Dk Susan Kolimba.
Kamati ya Uandishi wa Katiba ilimchagua Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na makamu wake, Mgeni Hassan Juma. Kwa kupata nafasi hizo ni dhahiri kwamba ‘mapishi’ ya uendeshaji wa Bunge hilo yatafanywa na CCM kwani mwenyekiti wake Samuel Sitta na makamu mwenyekiti Samia Suluhu Hassan pia ni makada wa chama hicho.
Wenyeviti hao wataungana na Sitta pamoja na Hassan kuunda Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu, ambayo ndiyo itakuwa na mamlaka ya kupanga ratiba na miongozo mbalimbali ya uendeshaji wa Bunge hilo.
Waliochaguliwa kuwa makamu wenyeviti ni Profesa Makame Mbarawa, Shamsa Mwangunga, Fatma Mussa Juma, Dk. Sira Ubwa Mamboya, Assumpter Mshama, Dk. Maua Daftari na Waride Bakar Jabu. Wengine ni Biubwa Yahya Othaman, William Ngeleja, Salimin Awadh Salimin, Yusuf Massauni na Thuwayba Kisasi.
Mbowe atimuliwa
Katika uchaguzi huo, mjumbe wa Bunge hilo, Freeman Mbowe alitimuliwa katika kamati alikokwenda kushiriki uchaguzi kwa madai kwamba hakuwa mjumbe.
Mbowe alisema kabla ya uchaguzi huo alimfuata Mwenyekiti Sitta kumwomba wafanye marekebisho katika kamati tatu za Bunge.
Alisema waliafikiana kuwa Godbless Lema aliyekuwa Kamati namba saba ahamieKamati namba mbili na AnnaMary Stella Mallac aliyekuwa Kamati namba mbili ahamie Kamati namba sita.
Alisema kwa makubaliano hayo yeye (Mbowe) alihamia Kamati namba saba akitokea Kamati namba sita.
“Nilivyoingia katika ukumbi wa Igada, wajumbe walianza kuguna mara wakaanza kuzozana wakitaka wajumbe ambao hawakuwamo kwenye orodha ya kamati hiyo kutoka nje,” alisema na kuongeza;
“Waliamua kuitana majina, lakini hawakuona jina langu wakanitaka nitoke nje, nikawaeleza makubaliano kati yangu na Mwenyekiti (Sitta) lakini hawakuafiki walisisitiza nitoke ndani ya ukumbi huo.”
Alisema hatua hiyo iliwafanya makatibu wasaidizi kuitwa na kuelezwa kilichotokea ambapo waliwasiliana na Katibu wa Bunge hilo, Yahaya Khamis Hemed ambaye aliwajibu kuwa bado hajapokea taarifa za mabadiliko hayo na kuwataka wasubiri awasiliane na Sitta.
“Wakati nikiendelea kusubiria
jibu, mmoja wa wajumbe aliendelea kupaza sauti akitaka niondolewe ili waweze kupiga kura,” alisema.
Alisema hali hiyo ilimfanya yeye na baadhi ya wajumbe kutoka vyama vya upinzani, akiwamo Profesa Abdallah Safari kususia uchaguzi huo na kuondoka.
Mbowe alisema baada ya muda walifuatwa na makatibu wakiwaomba samahani warudi ukumbini kwa sababu wamepokea maelezo kutoka kwa Sitta. Sitta alithibitisha tukio hilo, lakini alisema halikuathiri matokeo ya uchaguzi kwa sababu kuondoka kwao hakukuathiri akidi inayotakiwa.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company