Pepo la ajali lagubika nchi, Watu 21 wafa, tisa wajeruhiwa Rufiji , Kwa saa 24 wafa 33,16 wajeruhiwa

NA WAANDISHI WETU

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)

Kabla ya simanzi na majonzi kusahaulika miyoni mwa Watanzania baada ya watu 12 kufa papo hapo na wengine saba kujeruhiwa vibaya mkoani Kilimanjaro juzi, ajali nyingine mbaya imeangamiza maisha ya watu 21 na wengine tisa kujeruhiwa baadhi yao vibaya wilayani Rufiji, Pwani.

Watu hao 21 walikufa juzi saa 2:00 usiku wakiwamo saba papo hapo baada ya magari mawili aina ya Canter na Hiace na kugongano uso kwa uso na wengine 14 wakati wakiwaokoa majeruhi baada ya kugongwa na basi lililokuwa linatokea mkoani Lindi kwenda Dar es Salaam.

Ajali hizo zilizotokea ndani ya saa 24 zimesababisha vifo vya watu 33 na majeruhi 16.

Ajali hiyo iliyoua watu 21 ilitokea katika Kata ya Mkupuka, wilaya ya Rufiji barabara ya Dar es Salaam-Kilwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa idadi ya vifo na majeruhi iliongezwa na basi lililoparamia waokoaji na dereva na utingo wa Hiace inasadikiwa ni miongoni mwa waliokufa.

Alisema Hiace iliyokuwa ikitokea Ikwiriri kwenda Kibiti wakati ikitaka kulipita lori lililokuwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara, iligongana uso kwa uso na Canter na kuua watu saba papo hapo.

“Hadi sasa tunashindwa kuelewa dereva wa basi la kampuni ya Mining Nice alikuwa na tatizo gani kichwani, nadhani ni maruweruwe, tangu mbali alisimamishwa na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani waliokuwepo eneo la tukio, lakini hakusimama na kwenda kuwaparamia waokoaji na 14 kufapapo hapo,” alisema.

“Tumempima kama alikuwa amelewa tumekuta siyo, tumemhoji na tunaendelea kumhoji, hadi sasa anasema hajui kilichotokea alishtukia gari likiendelea kwenda,” aliongeza Matei.

Alisema kati ya 14 walioparamiwa na basi hilo, wawili ni wafanyakazi wa kituo cha Afya cha Mchukwi.

Mmoja wa wafanyakazi wa kituo hicho aliyekuwa katika eneo la tukio aliwaeleza polisi kuwa alinusurika baada ya kuruka akiwa na mwanaye pembeni mwa barabara huku akishuhudia wenzake wawili wakipoteza maisha.

“Hata mimi nilivyopata taarifa za awali nilishtuka kusikia watu 30 wote walikuwa ndani ya hiace, nimefika eneo la tukio na kuona mazingira ndipo nilibaini kuwa wengine walikuwa waokoaji akiwamo dereva na utingo wa gari aina ya lori lililokuwa limeegeshwa pembeni baada ya kuharibika,” alisema.

Kamanda Matei aliyataja magari yaliyohusika kwenye ajali hiyo kuwani lenye namba za usajili T 194 CUX aina ya Hiace lililokuwa kwenye mwendo kasi likitokea Ikwiriri kwenda Kibiti.

Akielezea chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa Hiace ambaye hajafahamika jina akiwa kwenye mwendo kasi kutaka kulipita lori lililokuwa limeegeshwa pembezoni kidogo mwa barabara lenye namba za usajili T 132 AFJ aina ya Tata.

Alisema dereva wa Hiace hiyo alilipita gari hilo bila uangalifu, hivyo kugongana uso kwa uso na Canter lenye namba za usajili T 774 CJW iliyokuwa ikitokea Mkuranga kuelekea Ikwiriri.

Kamanda Matei alisema baada ya ajali hiyo wakazi wa eneo la Mkupuka walijitokeza kuokoa majeruhi na kunasua miili ya watu waliokuwamo kwenye Hiace, lakini wakati wakiendelea na kazi hiyo, basi hilo likiwa kwenye mwendo kasi liliwaparamia na kusababisha watu wengi zaidi kufa na wengine kujeruhiwa na kuharibu zaidi miili iliyokuwa imelazwa barabarani.

Alisema watu 20 walikufa papo hapo na mmoja alifia njiani wakati akipelekwa hospitali huku tisa wakijeruhiwa, sita kati yao wakiwa wamejeruhiwa vibaya sehemu za vichwa, kuvunjika miguu na mikono.

Alisema kati ya marehemu hao 19 ni wanaume na wawili ni wanawake na miongoni mwao yupo mama, Asha Subini na mtoto wake, Wasabi Subini.

Alisema majeruhi tisa hali zao ni mbaya na walikimbizwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

Majeruhi hao ni Frank Sixmundi (31); Mohamed Salehe (42), wafanyakazi wa Maliasili Kibiti; Charles Rogasian (23), Mkazi wa Kibiti na Mohamed Mengine (44), Mkazi wa Dar es Salaam.

Wengine Mniko Magige (54), Mkazi wa Mkuranga Pwani; Khalid Salum (32), Mkazi wa Dar; Ahemed Yusuph (23), Mkazi wa Kigamboni Dar es Salaam; Shomari Yusuph (42), Mkazi wa Mburahati Dar es Salaam na Abdalah Issa (25), Mkazi wa Mkuranga.

Hata hivyo, alisema taarifa za awali zinaonyesha dereva na utingo wa magari ya Hiace na lori ni miongoni mwa waliokufa na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha ajali, majina yao na umri wao.

Alisema majeruhi hao baada ya ajali hiyo walipatiwa matibabu ya awali katika kituo cha afya cha Mchukwi.
Alisema maiti 21 wamehifadhiwa Kituo cha Afya cha Rufiji na majina yao yametambulika.

MAJERUHI WAFIKISHWA MUHIMBILI
Muunguzi wa zamu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini, kwa maelezo kuwa si msemaj,i alithibitisha kupokelewa kwa majeruhi watano.

Alisema majeruhi Charles aliyefanyiwa upasuaji mkubwa kwenye tumbo na kulazwa katika wodi namba 11 na anaendelea vizuri ingawa bado hajapata fahamu na Issa, Mengine, Magige na mmoja ambaye jina lake halijafahamika wanaendelea na matibabu.

Mganga Mkuu wa kituo hicho, Hawa Mteza, aliwataja waliofariki kuwa ni Nassoro Mohamed; Juma Kitangulile; Juma Salehe; Shafih Shite; Abrahamu Kimke; Abraham Massod; Mohamed Abadalah na Herman Msharafu.

Wengine ni walitambulika kwa jina moja moja ambao ni Japhet; Fikiri; Said Ally; Salum Boma; Hassan Wadi; Ramadhani Mangosongo; Ramadhani Chochote; Shabani Bakari; Sophia Mussa na Sikitu Mtanga.

Katika hatua nyingine, Kamanda Matei alisema wanamshikilia dereva wa basi hilo.

WA AJALI YA SAME WAZIKWA
Wakati huo huo; miili ya waombolezaji 12 ambao ni ndugu wa familia moja waliofariki Jumamosi iliyopita kwa ajali ya gari nje kidogo ya mji wa Hedaru, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro ilizikwa jana.

Ndugu hao, walipoteza maisha Ijumaa usiku majira ya saa 2:00 katika barabara kuu yaTanga-Moshi, baada ya magari matatu kugongana uso kwa uso ikihusisha lori aina ya Fuso lenye namba za usajili T 299 ANM lililokuwa likitokea Moshi kwenda Dar es Salaam, Toyota Hilux (Pick Up) lenye namba T 170 AKZ na Scania namba T 737 AKW lenye tela namba T 776 CCN ambalo lilikuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Moshi.

Ofisa Habari wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Gabriel Chiseo, alisema hali za majeruhi wawili waliolazwa hospitalini hapo zinaendelea kuimarika.

Imeandikwa na Yasmine Protace na Julieta Samson, Pwani; Salome Kitomari na Samson Fridolin, Dar; na Godfrey Mushi, Same.
CHANZO: NIPASHE
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company