Ndugu Zangu,
TUMEKUWA tukitamka; Ukistaajabia ya Mussa , utayaona ya Filauni! Si wengi wenye kuyajua ya Mussa ni yepi na ya Filauni pia.
Kuna simulizi niliyopata kuipokea. Kuwa alipata kutokea bwana mmoja. Yeye na mkewe walisubiri kwa miaka mingi kupata mtoto. Ikafika siku mkewe akatunga mimba. Na katikati ya kuilea mimba hiyo, bwana yule akapata safari. Naam, akasafiri kwenda mbali. Nyumbani kamwacha mkewe mjamzito.
Huku nyuma mke akapata maumivu. Mganga akamwambia; ili mimba isalimike, basi, ni sharti ale maini ya mbuzi, na afanye hivyo kila anapopata mimba.
Nyumbani hakukuwa na mbuzi wa kuchinja. Mama yule akaenda kwa ndugu wa mumewe mwenye zizi la mbuzi. Akamweleza shida yake.
Bwana yule mfuga mbuzi akakataa katakata. Kuwa hawezi kuchinja mbuzi wake kwa ajili ya kupata maini ya tiba tu. Mama mjamzito akarudi nyumbani akiwa mnyonge. Na mimba ile ikaharibika.
Mume aliporudi akasimuliwa na mkewe. Hakuamini masikio yake. Iweje nduguye amfanyie hivyo? Alijiuliza. Akafunga safari mpaka kwa Mussa, kwenda kuomba ushauri.
Alipofika kwa Mussa akasimulia kisa chake. Mussa alimsikiliza kwa makini. Na kwa vile aliombwa kutoa ushauri, basi, Mussa akamwambia; " Hayo yameshatokea, msamehe nduguyo!"
Bwana yule akaushangaa sana ushauri wa Mussa. Kwamba amsamehe tu mtu aliyesababisha mimba ya mkewe iharibike! Basi, akafunga safari hadi kwa Filauni , alikwenda huko kupata ushauri wake. Filauni naye akasikiliza kwa makini kisa chote.
Na kwa vile aliombwa kutoa ushauri, basi, akatamka; " E bwana ee, mimi naona umsamehe tu nduguyo!"
Bwana yule akaupinga ushauri ule. Akamtaka Filauni aje na ushauri ulio na busara zaidi. Basi, kwa vile Filauni aliombwa aje na ushauri tofauti na wa mwanzo, naye akatamka;
" Basi, mimi naona ni vema ukamkabidhi mkeo kwa nduguyo aliyekataa kumchinja mbuzi ili maini ya tiba yapatikane. Na akae na mkeo hadi atakapompa mimba. Na kwa vile mimba itakuwa ya kwake, basi, nduguyo atalazimika kumchinja mbuzi ili ipatikane tiba. Na mtoto akizaliwa, we nenda kamchukue mkeo na mtoto!"
Naam, ndio hayo ya kustaajabia ya Mussa na kuyaona ya Filauni! Na siye tuliokulia pwani mtu akikwambia; " Acha Ufilauni!" Basi, ujue amekasirika.
Ndio, na hata katika jamii yetu, na hususan kwenye fikra zetu, kuna mahali ambapo akina Mussa Na Filauni wamechangia katika kutufikisha tulipo sasa. Na hili nitalijadili zaidi huko twendako.
Maana, kama nilivyoandika jana, kuwa mara nyingi, kama wanadamu, makosa tuyafanyao hutokana na makosa ya wengine. Tunachofanya ni kuyarudia makosa.
Na je, unafanyaje pale kipofu anapokuvamia na kukusababishia maumivu makali? Jibu; Utakasirika kwa sababu ya maumivu uliyoyapata. Hiyo ni hali ya kibinadamu.
Lakini, ukiamua kulipiza kisasi, kwa wewe kujitoboa macho na kumvamia kipofu, basi, hapo utakuwa umetenda lisilo na busara. Na hilo ni Neno la Leo.Tafakari!
Maggid Mjengwa.
Iringa