Marais wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jana walikutana mjini Arusha, Tanzania ambapo walipitia mapendekezo na maoni kadhaa kuhusu uundaji wa shirikisho la kisiasa kati ya nchi wanachama. Marais walioshiriki mkutano huo walipendekeza kuanzishwa mchakato wa kuandika rasimu ya katiba kwa ajili ya kuundwa shirikisho hilo hapo baadaye. Mkutano huo mbali na Rais Jakaya Mrisho Kikwete ambaye alikuwa mwenyeji, ulihuhuriwa na Marais Yoweri Museveni wa Uganda na Uhuru Kenyatta wa Kenya huku Burundi ikiwakilishwa na Makamu wa Rais Prosper Bazombaza na Rwanda ikiwakilishwa na Waziri Mkuu Dakta Pierre Damien Habumuremye.
Vilevile mkutano huo wa viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulipitia ombi la kujiunga Sudan Kusini na jumuiya hiyo, lakini majadiliano zaidi juu ya suala hilo yameakhirishwa hadi Oktoba mwaka huu. Viongozi wa Afrika Mashariki pia kwa mara nyingine wamesisitiza kupambana na ugaidi na kuzuia kutokea tena mauaji ya kimbari kwenye nchi za eneo hilo kama yale yaliyojiri nchini Rwanda mwaka 1994.