Watu thelathini wamepoteza maisha katika moto uliowaka katika jengo mjini Odessa
REUTERS/Yevgeny Volokin
Na
Martha Saranga Amini
Zaidi ya watu thelathini wameuawa katika tukio la kiuhalifu huko mji wa Odessa kusini mwa Ukraine,wakati huu vurugu zikienea nchini humo na kuwa siku ya hatari zaidi tangu serikali ya Kiev inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi ishike madaraka.
Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani ya Ukrane ni kuwa takribani watu 31 walipoteza maisha ijumaa kwa kuungua moto,huku vyombo vya habari nchini humo vikiarifu kuwa makundi ya watu wanaounga mkono Urusi waaminika kuwepo katika jengo lililokuwa likiungua.
Wengi wa waliopoteza maisha walikosa hewa safi na kujikuta katikati ya moshi mkali wakati wengine wakipoteza maisha wakijitahidi kujiokoa kwa kuruka kupitia madirishani.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi imetoa wito kwa Ukraine na mataifa ya magharibi kuwajibika na kukomesha uharibifu dhidi ya waukraine huku ikilaumu Kiev kutowajibika kudhibiti uhalifu.
Hata hivyo Hapo jana Serikali ya Ukraine ilizindua operesheni ya kijeshi kuwasaka na kuwaondoa waasi wanaoiunga mkono serikali ya Urusi, na ambao wanadhibiti majengo ya serikali mashariki mwa nchi hiyo.
Operesheni hiyo imeanzia katika mji wa Slaviansk, ambao waasi wamekuwa wakikabiliana na maafisa wa usalama kwa wiki kadhaa sasa katika shinikizo la kuwataka waondoka katika mji huo.