LONGIDO
VIJANA nchini wameonywa na kutakiwa kuwa makini kwa kutokujihusisha na makundi yanayoweza kuwashawishi wajiunge na vikundi vya kigaidi kama Al-Shabaab.
Aidha, vijana wametakiwa kutokutumika vibaya na wanasiasa “uchwara” wakati huu kuelekea Uchaguzi Mkuu ambapo baadhi yao wamekuwa wakitumiwa na wanasiasa kwa manufaa yao binafsi.
Hayo yalisemwa juzi na Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, alipokuwa akizungumza kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa miundombinu ya maji katika Shule ya Sekondari ya Longido, iliyokwenda sambamba na mahafali ya 10 ya kidato cha sita shuleni hapo, Mkoa wa Arusha.
“Niliguswa na matukio ya vijana wale wa Dodoma na Zanzibar, waliohusishwa na mauaji kule Garisa, Kenya, hivyo nawasihi vijana hasa nyie mnaomaliza shule, muwe makini kutokuingia tamaa ya ushawishi, jihadharini na makundi ya ushawishi,” alisema na kuongeza:
“Tunasimama kwenye wakati mgumu sana, vijana tambueni umuhimu wenu wa kuliletea taifa maendeleo, watu wanawashawishi eti ukiua, utapata thawabu, hiyo si kweli, hao wanaowaambia mkaue si wakaue wenyewe au wao hawataki hiyo thawabu?”
Akizungumzia siasa, aliwataka wanafunzi hao ambao wana umri wa kupiga kura kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Kupiga kura pamoja na kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuchagua viongozi bora.
“Vijana msitumike vibaya kisiasa, kuweni makini na wanasiasa uchwara wanaotaka kuwatumia nyie kwa manufaa yao binafsi, ukifika wakati wa kujiandikisha jitokezeni kwa wingi pamoja na kujitokeza kupiga kura kuchagua viongozi bora na siyo bora kiongozi," alisema Ridhiwani.
Katika harambee hiyo, zaidi ya Sh milioni 34.9 zilipatikana kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo ya maji. Ili kukamilika kwa ujenzi huo, zinahitajika Sh milioni 100.
Awali Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Daniel Temu, alisema shule hiyo ina wanafunzi 1,639, ambapo inakabiliwa na tatizo kubwa la uhaba wa maji, hali inayosababisha wanafunzi kutumia muda mwingi kutafuta maji, hivyo kuchangia taaluma ya shule hiyo kushuka.
TAIFA STARS HAZARANI
-
Kaimu kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Etiene Ndairagije ametangaza
kikosi cha timu ya taifa chenye wachezaji 30 ambao wanajiaandaa na mchezo
wa kuwania ...
5 years ago