Waziri wa Mkapa awakingia kifua wagombea urais

Mwanasiasa mkongwe na aliyewahi kuwa waziri katika Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa, Njelu Kasaka
Na Brandy Nelson, Mwananchi

Mbeya. Mwanasiasa na mkongwe aliyewahi kuwa waziri katika Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa, Njelu Kasaka amekishauri chama chake cha CCM kuwaruhusu wanachama wanaotaka kuwania urais kujitangaza ili kutoa muda wa kutosha kwa wananchi kuwachambua na hatimaye kumpata kiongozi bora mwenye uwezo wa kuongoza nchi.

Chama hicho tawala, kimewapiga ‘kufuli’ makada wake sita, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja kwa madai ya kufanya kampeni mapema.

Lakini ushauri huo wa Kasaka, aliyewahi pia kuwa mkuu wa mkoa, umetulipiwa mbali na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye ambaye amesisitiza kwamba hawawezi kufuata maoni hayo, bali wataendelea na utaratibu wa vikao katika kumpata mgombea wake.

Nape alisema: ‘‘Chama kina utaratibu wa vikao na ndiyo utakaofuatwa. Maoni ya Njelu Kasaka ni haki yake.” Alipoulizwa ni lini vikao vya uteuzi vitaanza, alijibu kwa mkato “bado.”

Akizungumza kwa simu jana, Kasaka alisema hivi sasa hatua ya kujitangaza imecheleweshwa na kwamba kinachotakiwa ni ifikapo Julai mwaka huu, mgombea urais awe ameshapatikana baada ya wananchi kumpima uwezo wake.

“Hatuwezi kuambiwa na mtu mwingine uwezo wa mgombea urais, bali tunataka kusikia kutoka kwake kwani atatakiwa kututhibitishia yeye mwenyewe na wananchi wakamsikiliza na kumpima kuona kama anakidhi kuendesha nchi na kukabiliana na matatizo tuliyonayo,” alisema.

Kasaka alisema hatua ya wagombea kuchelewa kujitangaza italeta athari itakayokigharimu chama chake na nchi kwa ujumla huku akisema ni vigumu kumpata kiongozi bora atakayekuwa ameteuliwa na viongozi pekee.

Kauli ya Kasaka imekuja siku chache baada ya Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula kusema chama hicho ndicho kinachomwandaa na kumwangalia mgombea.

Alisema kuwa CCM itamtoa mgombea anayekubalika, aliyefuata maadili, taratibu na kanuni za chama katika utekelezaji wa majukumu yake.

Hata hivyo, Kasaka aliyewahi kukihama kwa muda chama hicho na kujiunga na CUF kabla ya kurejea alisema uongozi wa CCM ngazi ya Taifa unapaswa kuliangalia suala hilo kwa umakini na kutoa uamuzi wa haraka kuruhusu watu kujitangaza ili kuepuka kumpata bora kiongozi dakika za mwisho badala ya kiongozi bora.

“Kwani kiongozi anayetakiwa kuiongoza nchi hii anapaswa kuwa na uwezo wa kujielewa na kuilewa nchi yetu ilivyo hata akiulizwa masuala ya uchumi wa nchi aweze kutoa maelezo ya kina na watu waweze kumuelewa,” alisema.

Alisema anaweza akawepo mtu ambaye hana kashfa na akawa mwadilifu, lakini akawa hana uwezo wa kuongoza nchi, hivyo umakini unahitajika katika kumpata mgombea urais.

“Ni kweli tunahitaji mtu asiye na kashfa, lakini kisiwe kigezo pekee cha kumpata mgombea urais kwani ni lazima kuangalia historia yake ya nyuma kama aliwahi kuwa kiongozi na uwajibikaji wake ulivyokuwa wakati huo,” alisema.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company