MWENYEKITI wa Chama cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, amesema chama chake kinaandaa taratibu za kwenda mahakamani ili kumshtaki mgombea urais mteule wa CCM, Dkt. John Magufuli na mgombea urais wa CHADEMA, Bw. Edward Lowassa.
Alisema wagombea hao kwa nyakati tofauti, wameshiriki kuiingizia Serikali hasara ya mabilioni ya fedha ambapo wanasheria wa chama hicho wapo katika hatua za mwisho ili wafunguliwe mashtaka mahakamani.
Mchungaji Mtikila aliyasema hayo Dar es Salaam juzi, alipozungumza na waandishi wa habari akisisitiza kuwa, wagombea hao wamepoteza sifa za kuwania nafasi hiyo akidai hawana vigezo kwa mujibu wa sheria.
Aliongeza kuwa, Bw. Lowassa, anahusishwa na sakata la kampuni ya Kufua Umeme ya Richmond na kuishangaa CHADEMA akidai chama hicho kilipata umaarufu wa kupinga vitendo vya ufisadi lakini wamempokea Bw. Lowassa ana tuhuma kama hiyo.
"Kipindi cha nyuma, CHADEMA walianzisha operesheni nyingi ikiwemo ya Sangara na Movement for Change zikiwa na lengo la kupinga ufisadi, kwanini wamempokea Lowassa waliyemuita fisadi.
"Hii ina maana kuwa, ndani ya CHADEMA hakuna siasa, nawapongeza baadhi ya viongozi wa chama hicho na wanachama wao ambao kimsingi hawakubaliani na matakwa ya viongozi wa juu," alisema.
Akimzungumzia Dkt. Magufuli, alimhusisha na tuhuma ya uuzwaji wa nyumba za Serikali akidai kitendo hicho kimeisababishia hasara Serikali lakini hakupelekwa mahakamani kwa kutumia madaraka yake vibaya kama ilivyokuwa kwa Basil Mramba, Daniel Yona ambao hivi sasa wanatumikia kifungo gerezani.
Alisema nyumba hizo zilikuwa makazi ya viongozi kama Majaji, Makatibu Wakuu na Watendaji waandamizi serikalini ambao wengi wao walilazimika kuishi hotelini kwa gharama za Serikali.