RAIS Jakaya Kikwete, amesema hamshangai mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk.John Magufuli kwa kukosoa utendaji kazi wa Serikali yake katika mikutano yake ya kampeni inayoendelea.
Rais Kikwete, alitoa kauli hiyo juzi, wakati akizungumza na wafanyakazi wa Taasisi ya NDI yenye uhusiano na Chama cha Democratic, IRI yenye uhusiano na Chama cha Republican, IFES na United States Institute of Peace (USIP) mjini Washington nchini Marekani.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu mjini Dar es Salaam jana, ilisema Rais Kikwete anaunga mkono mwenendo wa kauli za Dk. Magufuli kwa sababu kila kiongozi anapoingia madarakani anakuwa na aina yake ya uongozi.
“Wamepata kuja watu kwangu,wakaniambia mgombea wetu wa CCM anashutumu na kusahihisha Serikali yangu na utendaji wake kwenye mikutano ya kampeni. Niliwaambia hivi anavyofanya mgombea wetu ni jambo sahihi kabisa,lazima afanye hivyo.
“Niliwaambia nchi yetu, inahitaji mawazo mapya na mwelekeo mpya ulio tofauti na uongozi wangu. Niliwaambia tusiporuhusu jambo hilo kufanyika, nchi yetu itabakia pale pale ambako nimeifikisha mimi.
“Haya yatakuwa na makosa makubwa kwa sababu nchi yetu lazima isonge mbele kwa mawazo mapya,uongozi na staili mpya ya uongozi.
“Haya ndiyo anayosema mgombea wetu. Vinginevyo ni jambo lisilokuwa na maana kubadilisha uongozi kama hatuko tayari kukubali, kila kiongozi lazima awe na staili yake ya uongozi na namna ya kuongoza na kuendesha nchi yetu,” alisema.
Katika mikutano yake Dk. Magufuli amekuwa akieleza namna asivyoridhishwa na uwepo wa huduma mbovu katika sekta mbalimbali ikiwamo afya na maji, hali inayowafanya wananchi waendelee kutaabika.
Dk. Magufuli amekuwa akishangaa kuona dawa zinakosekana katika hospitali za Serikali huku dawa hizo zikipatikana katika maduka binafsi na kuahidi kupambana na majizi na mafisadi.
Mgombea huyo pia amekuwa akishangaa pale ambapo baadhi ya watumishi wanapoharibu aidha kwa kuiba fedha za umma au uzembe kazini kuhamishwa vituo vya kazi, badala ya kufukuzwa na kushitakiwa.
Atamani kupumzika
Katika hatua nyingine,Rais Kikwete alisema anatamani muda uende kwa kasi zaidi ili akabidhi madaraka kwa rais wa awamu ya tano.
“Natamani muda uende nikabidhi madaraka kwa rais wa tano ili nipate muda wa kumpumzika,baada ya kazi ngumu ya miaka 10 ambayo ni kama mzigo mkubwa,”alisema Rais Kikwete.
Miswada Kandamizi
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete aliwataka watu binafsi ama taasisi yoyote wenye matatizo na Sheria ya Takwimu au Muswada wa Habari, wawasilishe mapendekezo serikalini ili yafanyiwe kazi.
Alizitaka taasisi hizo kuacha kulalamika pembeni au kupitia vyombo vya habari.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo, baada ya kuulizwa swali kuhusu madai ya Sheria ya Takwimu na Muswada wa Habari, kuwa inavuruga sifa za kidemokrasia chini ya uongozi wake.
“Nimelizungumza hili siku za nyuma, napenda kurudia tena. Sheria ya Takwimu inahusu takwimu rasmi za Serikali tu na wala si takwimu zote.
“Pili sheria hii, inatokana na matakwa na taratibu za Umoja wa Mataifa na sheria yetu imetungwa kwa kutilia maanani matakwa ya kimataifa…kwa nini hili linakuwa tatizo kwa Tanzania pekee ni jambo gumu kueleza,”alisema Rais Kikwete.
Kuhusu Muswada wa Sheria ya Habari, Rais Kikwete alisema.“Nimelisema hili huko nyuma,inaelekea halijaeleweka. Nilipata kusema pale Dar es Salaam na hata wakati nazungumza na wabunge wa Sweden mjini Stockholm kuwa kama mtu ana tatizo ama maoni na maudhui ya muswada ule, ayafikishe serikalini tutafanyia kazi.
“Hatuna tatizo na jambo hili, ajabu nasikia wanalalamika tu na hakuna yeyote ambaye amefikisha maoni yake kwetu.
“Jambo muhimu ambalo lazima sote tuelewane hapa ni kwamba muswada wowote, uwe wa habari ama wa jambo jingine, lazima ulinde maslahi ya nchi yetu,umoja,utulivu na usalama.
“Haya ni mambo ambayo hatuna haja ya kujadiliana na yeyote kwa sababu nchi zote duniani zinalinda kwa namna hii na zinaendeshwa namna hii,”alisema Rais Kikwete.
#USOPEN_VIGOGO CHALI
-
SIKU Safi kwa Muaustralia Nick Kyrgios baada ya ushindi dhidi Johnson na
kutinga raundi ya Pili.
- Rafael Nadal akimchapa Millman Seti Tatu zote mfululi...
5 years ago