TANZANIA imetimiza masharti yote ya kupatiwa raundi ya pili ya fedha za maendeleo kutoka Shirika la Maendeleo ya Milenia (MCC) la Marekani, hivyo itaanza kupata na kunufaika na mabilioni hayo ya fedha baada ya wajumbe wa Bodi ya MCC kupiga kura ya kuidhinisha kutolewa kwa fedha hizo chini ya Mpango wa MCC-2.
Habari hizo njema zilitangazwa juzi kwa Rais Jakaya Kikwete na Mtendaji Mkuu wa MCC, Dana J. Hyde katika mkutano uliofanyika katika Hoteli ya JW Marriot Essex House, New York, na kuhudhuriwa na watumishi waandamizi wa MCC akiwamo Kamran Khan, Makamu wa Rais wa Operesheni za MCC.
Rais Kikwete yuko New York kuhudhuria shughuli za mwaka huu za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
“Hongera Mheshimiwa Rais kwa sababu nchi yako, Tanzania, imetimiza masharti yote ya kupata fedha nyingine chini ya mpango wa MCC - 2 ikiwa ni pamoja na uongozi wa MCC kuridhika kuwa Tanzania inachukua hatua za dhati kupambana na rushwa,” Hyde alimwambia Rais Kikwete na viongozi wengine wa Tanzania akiwamo Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Yusuf Omar Mzee.
Hyde alimwambia Rais Kikwete kuwa Bodi ya MCC, katika mkutano wake wa Septemba 17, mwaka huu na chini ya Mwenyekiti wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, imeafiki kuhusu kipengele pekee kilichokuwa kimebakia katika masharti ya kupata fedha za MMC kuwa ni kweli Tanzania inakabiliana ipasavyo na rushwa na kuchukua hatua stahiki kukabiliana na tatizo hilo.
MCC ilitoa taarifa ya kuthibitisha kuwa Tanzania imetimiza masharti ya kuiwezesha kufaulu kupata raundi ya pili ya fedha za maendeleo na pia ilitoa taarifa ya kuthibitisha kuwa ni kweli Bodi ya MCC imeridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Tanzania katika kukabiliana na rushwa.
Tofauti na fedha nyingi zinazotolewa na wafadhili wengi duniani, fedha za MCC hazitakiwi kurudishwa na nchi inayopewa fedha hizo na pia nchi husika hupewa uhuru wa kuchagua aina ya miradi ya maendeleo ambayo inaitaka igharimiwe na fedha hizo.
Miongoni mwa wajumbe wengine wa Bodi ya MCC ni Waziri wa Fedha wa Marekani ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Mwakilishi wa Biashara wa Marekani duniani, Mwendeshaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), nafasi ambayo kwa sasa anaikaimu Alfonsi Lenhardt, Mtendaji Mkuu wa MCC, Hyde na Rais wa Taasisi ya International Republican Institute (IRI), Balozi Mark Green.
Mabalozi Lenhardt na Green walikuwa mabalozi wa Marekani katika Tanzania wakati wa majadiliano, upitishaji na utekelezaji wa MCC–1.
Hyde alisema sasa linalobakia ni kwa wajumbe wa Bodi kupelekewa muhtasari wa kuidhinisha mabilioni hayo kwa Tanzania ambayo chini ya mpango wa uwekezaji wa MCC–2 yatakwenda katika kuboresha huduma za umeme nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na kusambaza umeme katika vijiji vingi zaidi.
Kiasi cha asilimia 46 ya Watanzania kwa sasa wanapata umeme kutoka asilimia 10 ya mwaka 2005 na sehemu kubwa ya asilimia hiyo imetokana na msaada wa MCC-1. Chini ya Mpango huo wa pili wa MCC, Tanzania itapatiwa Dola za Marekani milioni 472.8 (sawa na Shbilioni 992.80).
Kwa kutilia maanani kiasi cha dola milioni 698 (sawa na Sh trilioni 1.46) ambazo zilitolewa chini ya MCC-1, Tanzania itakuwa imepata jumla ya dola za Marekani trilioni 2.45 za maendeleo kutoka Marekani katika kipindi cha miaka 10 tu iliyopita. Fedha za MCC-2 zitaanza kutolewa mwakani, 2016.
Kiasi kilichotolewa kwa Tanzania wakati wa MCC-1 ndicho kilikuwa kiasi kikubwa zaidi ambacho kimepata kutolewa na Marekani chini ya mpango huo, na kwa kupita MCC-2, Tanzania itakuwa ni nchi ambayo itakuwa imepata kiasi kikubwa cha fedha za maendeleo chini ya MCC duniani.
Fedha zilizotolewa chini ya MCC -1 zilitumika kujenga Barabara za Tunduma-Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo-Songea- Mbinga.
Aidha, fedha hizo zilitumika kujenga upya mfumo wa huduma za maji kwa ajili ya miji ya Dar es Salaam na Morogoro na zilitumika kusambaza umeme katika vijiji vya mikoa 10 ya Tanzania Bara.
Fedha hizo vile vile zilitumika kutandaza njia ya pili ya kusafirisha umeme chini ya Bahari ya Hindi kati ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani na pia zilitumika kujenga barabara zote kuu za Kisiwa cha Pemba na baadhi ya barabara za Unguja kwa kiwango cha lami.
TAIFA STARS HAZARANI
-
Kaimu kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Etiene Ndairagije ametangaza
kikosi cha timu ya taifa chenye wachezaji 30 ambao wanajiaandaa na mchezo
wa kuwania ...
5 years ago