Chama cha wafanyakazi wa vyuma nchini Afrika Kusini chajiondoa ndani ya chama cha ANC


Katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi wa vyuma nchini Afrika Kusini, Numsa, Irvin Jim
Reuters
Na Emmanuel Richard Makundi

Juma moja likiwa limemalizika toka kufanyika kwa mazishi ya aliyekuwa rais wa kwanza wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, chama cha ANC kimeingia kwenye mzozo kufuatia chama cha wafanyakazi wa vyuma nchini humo Numsa kutangaza kujiondoa kwenye chama hicho.
Numsa ni moja kati ya vyama vikubwa vya wafanyakazi nchini Afrika Kusini ambacho kiko chini ya mwavuli wa chama cha Cosatu ambapo kujitoa kwake kukiunga mkono chama tawala kumeelezwa ni pigo la kisiasa kwa chama hicho kongwe nchini humo.

Hatua ya kujiondoa kwa chama hicho kwenye chama tawala ilitarajiwa na wachambuzi wengi wa masuala ya siasa ambao wanaona kuwa chama cha ANC kwa siku za hivi karibuni kimepoteza umaarufu wake kwa vyama vya wafanyakazi ambapo kwa sehemu kubwa hushiriki kuchagua rais wa taifa hilo.

Kiongozi wa chama hicho, Irvin Jim ndiye aliyetangaza uamuzi wa chama hicho na kuongeza kuwa chama chake hakitakiunga mkono chama chochote kwenye uchaguzi mkuu ujao wa urais.

Kwenye taarifa yao baada ya kikao cha kamati kuu ya chama cha wafanyakazi wa vyuma nchini humo, imemtaka pia rais Jackob Zuma kujiuzulu nafasi yake ya urais kabla ya kuelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Kujiondoa kwa chama hicho kunakuwa pigo kwa ANC ambapo mara zote kimekuwa kikishinda chaguzi zake za urais na ubunge kutokana na mchango wa vyama vya wafanyakazi toka kumalizika kwa ubaguzi wa rangi nchini humo mwaka 1994.

Chama hicho kinamtaka rais Zuma ajiuzulu kwa kile ilichodai kuwa ni kushindwa kwa Serikali yake kuleta maendeleo kwa wananchi na badala yake viongozi wake wamekithiri kwa vitendo vya rushwa na ubadhilifu wa mali za Serikali.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company