Pia yupo samaki tuliyemwita ‘Wino’ Huyu alimwaga rangi kwenye maji mara tu alipohisi hatari. Unapotaka kumkamata, anayachafua maji kiasi cha kukupoteza nuru, kisha anatoroka. Unaposubiri wino uishe, yeye anakuwa ameshafika kilometa tano kutoka ulipo.
Kadhalika yupo mwingine tulimwita ‘Shoti’ lakini wengine walimwita ‘Electrical Fish’. Huyu unapomgusa tu anakupiga shoti kama uliyegusa nyaya za umeme zilizo uchi. Namkumbuka pia mdudu mdogo ambaye ukimgusa anakunyea shuzi ukae ukinuka kutwa nzima. Sikuumiza sana akili yangu kuchunguza ni vipi viumbe hao waliweza kutenda miujiza hiyo kwa sababu jibu lilikuwa wazi kabisa.
Wakati fulani niliwahi kusimulia nilichokuwa nikifahamu kuhusu Dinosauria. Mijusi wenye ukubwa hadi kufikia ghorofa, waliowahi kuishi miaka mingi sana iliyopita. Tofauti na miili yao, vichwa vyao vilikuwa vidogo, kitu kilicholazimisha bongo zao kuwa ndogo hivyo ziwe na mzunguko mdogo sana wa damu.
Kwa jumla, ikawa ni vigumu zaidi kwao kupambanua hisia zinazoletwa na mishipa ya fahamu. Kwa mfano anapokanyaga moto, inamchukua muda mrefu kuhisi na kuelewa kuwa anapaswa kuondoa mguu hapo alipokanyaga. Hatima ya yote, wote walikufa kutokana na kutokula kwa kutokuhisi njaa, kuzama baharini na kuangukia kwenye miamba ya mabondeni.
Yaani linaingia baharini maji ya ugoko, mara maji ya goti, linakwenda tu; maji ya paja, ya tumbo, ya kifua, shingo hadi linazama bila kujua kuwa litakosa pumzi hadi kufa. Ni kwa sababu hakukuwa na uwiano kati ya ubogo wake na mwili wake. Ni sawa na mtu anayemiliki ardhi yenye ukubwa wa nchi nzima. Hataweza kujua kwa wakati mmoja linalotokea Tunduru na Karagwe.
Kwa hiyo utaona kuwa yule ambaye kiatu kinamtosha ndiye atakayekivaa. Hata kofia: mimi nikikupa ya kwangu nawe unipe ya kwako tutaonekana wote ni machizi. Sikutishi, lakini chukua kisu ukate kichwa chako unipe mimi, kata na changu ukivae wewe. Haki ya nani, utabutuka kama bomu. Sisemi kuwa ati mimi nawaza mengi kuliko wewe, ila inawezekana wewe huwazi kama mimi.
Fikiria wakati huu bado tuna foleni vibarazani kwa waganga. Tatizo? “Ati kwa nini sipati mtoto? Kwa nini ndoa zangu zinavunjika mapema? Kwa nini sina hamu ya tendo la ndoa? Kwa nini sina pesa?” Yaani kwa nini zinazojitokeza, zinaweza kufikia 100 kila dakika. Jibu ambalo ni ‘kwa sababu’ linaweza lisitoke hadi nasi tutakapotoweka kama dinosauria.
Kipindi kile nilipozuga kuwa mimi ni mganga, nilijiwa na bibie mmoja. Akanipa hadithi ya kuhuzunisha sana, kuwa majuzi ameachika tena baada ya kuolewa mara ya nne (vyuo vinne)! Ndoa zake zote zilidumu kwa muda mfupi wa miezi miwili, mitatu na minne.
Kabla sijampigia “ramli” (utafikiri kweli vile), akaanza kuwashutumu shangazi zake kwa kukichezea kitovu chake. Anazikumbuka ndoa zake zote zilivyoacha gumzo jijini kwa jinsi zilivyofana. Anawakumbuka pia waume zake wote jinsi walivyokuwa wa daraja za juu. Lakini hapati picha ni vipi akaishi nao kwa wastani wa miezi mitatu tu na kila mmoja wao, kabla ya kutwangwa talaka isiyo ya rejea.
Kwanza nilimuonya kuwa akinidanganya nami nitamdanganya. Kenge hawezi kuibeba nyumba ya kobe; je, alipokuwa tayari kuolewa alijua anahitaji mume wa aina ipi? Na je, alikwisha kujitayarisha kwa ajili ya mume aliyemtaka? Jibu ni mume wa daraja ya juu kwani yeye alitokea kwenye familia ya daraja la juu. Kazi kwelikweli.
Mimi sikutaka kumwibia. Nilimwambia wazi kuwa maisha anayopenda kuishi siyo ya aina yake, bali anaigiza. Nilimtazama kisura chake kilivyochoka kwa kuvuliwa magamba, vijiguu vyake vilivyokwishaenda kilometa nyingi bila viatu na kamwili kalikobeba tani nyingi bila kujali uchakavu. Kama angelikuwa gari, hakuna askari wa barabarani ambaye angliruhusu kwenda.
Sisi Waafrika tuna mfumo wetu wa kuishi. Tunaishi kama wanyama, na ndiyo mfumo bora kwa wanyama akiwemo binadamu. Wageni nao wana mifumo yao, ambayo ukimpa Mwafrika aiishi utamuua. Wewe ukijigonga gotini, usitake kupuliziwa dawa aliyopuliziwa mchezaji Messi ili upone papo hapo. Kwa sababu huwezi kuendana na sumu ya mionzi ya dawa hiyo kwa maisha unayoishi.
Siyo ajabu leo ukienda ufukweni kwa wageni ukawakuta wapo kwenye sauna. Watupu kama walivyozaliwa, tena miongoni mwao kuna wazee na watoto. Hawa wameshajiamria kuikosa hamu ya tendo la ndoa kwa sababu wameshajiandalia kuzaliana kwa chupa.
Tunataka kuwaiga. Lakini kila tunapojaribu kwenda uchi ufukweni kuna mtu atabakwa. Ni kwa nini uvae kofia isiyokutosha