Kambi ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini imeshambuliwa na wapiganaji wa kabila la waNuer ambalo ni la pili kwa ukubwa nchini humo.
Inaripotiwa kuwa, wapiganaji hao walikuwa wamewalenga watu wa kabila la waDinka. Jumla ya watu 32 walikuwa wamepewa hifadhi kwenye kambi hiyo wakati shambizi hilo lilipotokea. Umoja wa Mataifa umesema umepoteza mawasiliano na kambi hiyo na unahofia huenda shambulizi hilo limesababisha vifo vya watu kadhaa.
Farhan Haq ni msemaji wa Umoja wa Mataifa. Amesema:
"Mapigano yametokea na hatujathibitisha hali ilivyo. Tonahofia huenda tukio hili limeshasababisha vifo vya watu kadhaa, lakini kwa sasa hatuwezi kuthibitisha wangapi wamefariki, na ni nani. Tume ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS itaondoa wafanyakazi wake wasio wa kijeshi kutoka Akobo, na wakati huohuo, itaimarisha kambi hiyo kwa kuongeza vikosi vingine 60 kutoka Malakal."
Habari nyingine zinasema, wafanyakazi wenyeji 14 wa kampuni ya mafuta nchini Sudan Kusini wameuawa jana katika mapigano kati ya makundi ya wapiganaji kutoka makabila ya waDinka na waNuer.